Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii uliyonipa ili niweze kutoa mchango wangu katika Sekta ya Madini. Kwanza ninaanza kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa sana alioonesha katika Sekta ya Madini kwa kuendelea kulisaidia Shirika la STAMICO kuendelea kununua mitambo ya kuchoronga na kusaidia wachimbaji wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Antony Mavunde, Naibu Waziri wa Madini, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Madini kwa kuendelea kufanya kazi ya kusaidia Watanzania kujiendeleza kupitia Sekta ya Madini. Pongezi za mwisho ninamalizia kwa kumpongeza Rais wa Wachimbaji Wadogo, Ndugu John Wambura Bina, leo yuko hapa kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo na kuwasaidia kupata exposure ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa ninapitia mitandao ya kijamii, nimeona baadhi ya wachimbaji wadogo wameelekea Canada kwa ajili ya kujifunza uchimbaji wa madini ili waweze kuleta tija ndani ya Taifa letu. Hongera sana ndugu Rais wa Wachimbaji Wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo nitachangia jambo moja tu kuhusiana na Sekta ya Madini na jambo hili linahusu shughuli za utafiti katika Sekta ya Madini. Shughuli za utafiti katika Sekta ya Madini ni sawa na kupanda mbegu kwa wale wakulima. Kadri unavyoongeza utafiti, ndivyo tunavyopanda mbegu ya uvunaji wa madini na kuleta maendeleo yenye tija ndani ya Taifa letu. Hata hivyo, Sekta ya Utafiti ina changamoto kubwa. Sekta ya Utafiti inakabiliwa na ukosefu wa Bodi ya Wajiolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi hii tumeanza kuipigania tangu 2017, Waheshimiwa Mawaziri wengi tumewaalika kwenye TGS, Mheshimiwa Waziri Mkuu pia amefika na kila Mheshimiwa Waziri aliyefika pale aliahidi kwamba jambo hili la msingi kwa maslahi mapana ya Taifa na watahakikisha linasajiliwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami Januari mwaka huu swali langu mojawapo la kwanza kuuliza ndani ya Bunge hili, lilikuwa ni lini Serikali itaweza kusajili Bodi hii ya Wajiolojia. Majibu yaliyotoka ni kwamba Bodi hii inatarajiwa kusajiliwa na bado Wizara inaendelea kukusanya maoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hivi, Wizara tunawaomba sana muda wa kukusanya maoni umekwisha na maoni waliyonayo yanatosha, huko mtaani hali si shwari. Sasa hivi huwezi kutofautisha Mjiolojia na vishoka walioko huko, wananchi wanatapeliwa sana. Wapo watu wanaojiita wao ni wataalam wa utafiti wa madini, wananchi wanatumia fedha kubwa kuwalipa, wanaandaa ripoti feki, wanakula fedha ya utafiti na wananchi wale wanawekeza fedha nyingi kwenye maeneo ambayo yamefanyiwa utafiti feki, hivyo wanakula hasara kubwa sana na kupelekea kufilisika kwa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mifano hai ya watu wengi ambao wameandikiwa taarifa feki za kiutafiti na wakawekeza fedha nyingi na wengine wamekopa. Ukitembelea kwa mfano Mkoa wa Geita maeneo ya Nyarugusu, kuna mradi mkubwa sana ulianzishwa na mchimbaji mdogo, lakini ulikufa kwa sababu wataalam walimwandalia taarifa feki za kiutafiti. Ukienda maeneo mengine ya Bukombe kule, kuna mradi ulikufa kwa sababu wataalam walimwandalia taarifa feki ya kiutafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, taaluma hii ya Wanajiolojia inasaidia sana katika nyanja zifuatazo:- Utafiti wa maji; sasa hivi ukiangalia kwenye majimbo yetu, tunachimba visima vingi vya kuchoronga lakini visima vingi pia tunapata maji na vingine hatupati maji. Hii ni kutokana na kwamba taarifa za kijiolojia zinazofanyika pale zinakuwa hazina uhalisia. Hivyo Serikali inaingia gharama kubwa ya kuchoronga visima visivyotoa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo takwimu mbalimbali za uwepo wa mafuta, gesi na kadhalika. Kazi hizo zinafanywa na hawa Wajiolojia, lakini bahati mbaya sasa ukosefu wa hii Bodi umepelekea wale Wajiolojia ambao ni halisi wanaojua kazi, wanakuwa siyo waadilifu, kuna wakati wanafoji data.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sekta ya Utafiti pia kuna fraud kubwa sana huwa inaendelea. Kwa mfano, ili uweze kupata taarifa sahihi, kuna namna ambayo unatakiwa ufanye katika kupata taarifa hizo iwe geophysics, iwe kwenye ku-drill na kadhalika. Kwa hiyo, kuna wakati mtu anakuja anakuletea ripoti amechoronga mashimo 20, lakini kiuhalisia mtu yule amechoronga mashimo 10. Mashimo 10 mengine ameandika data feki na bado analipwa fedha ya mashimo 20. Madhara yake ni kwamba utakapoenda kutekeleza mradi huo, lazima utafeli kwa sababu utakuwa ni mradi ambao hauna taarifa za kujitosheleza kuweza kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uwepo wa hii Bodi ambayo Wizara ya Madini wakiweza kuisajili, itahakikisha kwamba Wajiolojia wote ama wataalam wa Sekta ya Utafiti ndani ya Sekta ya Madini wanakuwa waadilifu. Wale ambao hawatakuwa waadilifu, bodi hii itawajibika kuhakikisha kwamba inawafutia leseni za utafiti kwa sababu tutakapokuwa na hii Bodi, ili uweze kutafiti katika nchi hii tutaweka utaratibu wa kwamba mradi wowote lazima usajiliwe na ukisajiliwa mradi ule, ni lazima utalipiwa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha ile itatumika katika uendeshaji wa Bodi hii lakini kuna baadhi ya fedha itaingia Serikalini kama vyanzo vya mapato, ili mteja aliyefanyiwa utafiti atakapoleta malalamiko ya kwamba utafiti ule aliambiwa hapa kuna dhahabu kilo 10 akachimba shimo lake pale akakuta hakuna dhahabu mfano, anayo fursa sasa ya kulalamika kwenye hiyo Bodi na yule mtu aliyemfanyia utafiti wa kumdanganya akachukuliwa hatua za kisheria na kulipa gharama alizotumia mchimbaji huyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuchangia katika Fungu la Utafiti wa Madini kupitia GST, STAMICO na TPDC. Ninashauri Serikali kupitia Wizara ya Madini, waweke utaratibu kama ambavyo tumeweka utaratibu kwenye Mifuko mingine kama Road Fund kwamba kila lita ya mafuta yanayoingia hapa nchini kuna shilingi 100 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, waweke pia utaratibu kwamba kila gramu moja inayouzwa ya dhahabu ama ya madini yoyote yale, kiasi fulani cha fedha kiingie kwenye Mfuko wa Utafiti wa Madini ndani ya Taifa letu. Kwa kufanya hivyo tutahakikisha kwamba tunapata fungu la kutosha wakati wote wa uzalishaji wa madini yetu ambalo fungu hilo litatumika sasa katika kuziwezesha taasisi zinazohusika na masuala ya utafiti ndani ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kuchangia suala la CSR, kumekuwa na changamoto kubwa katika jamii yetu. Unakuta eneo hilo linazalisha madini mengi sana, hata hivyo, mazingira ya eneo hilo ikiwemo barabara, shule, hospitali zinatia huruma sana na wawekezaji hawawajibiki kusaidia maendeleo ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, ninapendekeza Wizara ya Madini ije na mkakati, waje na sheria na sisi Waheshimiwa Wabunge tutaunga mkono sheria hiyo, waweke kwamba, CSR kuanzia sasa tuanze kulipa kwa asilimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tujue kwamba kwa kila kiwango fulani cha madini unachozalisha, kuna asilimia fulani ya CSR ambayo italipwa moja kwa moja kwenye masoko yetu ya madini na fedha ile itaweza kuingia kwenye Mfuko huo ili iweze kusaidia wananchi wetu...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. JOHN S. LUHENDE Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo mengine, lakini kutokana na uchache wa muda, nitayachangia kwa njia ya maandishi. Hata hivyo, ninakushukuru sana na niwapongeze Wizara ya Madini kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya. (Makofi)