Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Enock Zadock Koola (2 total)

MHE. ENOCK Z. KOOLA aliuliza :-

Je, lini Serikali itajenga skimu za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha chakula katika Jimbo ya Vunjo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji katika Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo Jimbo la Vunjo. Kwa mwaka 2025/2026, miradi mitano inaendelea kutekelezwa katika Jimbo la Vunjo ikihusisha mradi wa ujenzi wa Skimu ya Mawala wenye ukubwa wa hekta 2,500 unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.1.

Mheshimiwa Spika, vilevile, miradi minne imepangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao wa 2026/2027 inayojumuisha skimu nne za Mananga, Ndekambeko, Masaera na Masaga ambapo mkandarasi ameshapatikana.
MHE. ENOCK Z. KOOLA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha kukodi vifaa vya kilimo katika Wilaya ya Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kutekeleza mpango wa uanzishaji wa vituo 1,000 vya kutoa huduma ya zana za kilimo kwa wakulima katika ngazi ya Kata ifikapo mwaka 2030, lengo likiwa ni kusogeza na kuwawezesha wakulima, kupata huduma za zana za kilimo kwa wakati na gharama nafuu ili kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza hilo, Wizara imeanzisha vituo 79 katika Halmashauri mbalimbali nchini, ikiwemo Halmashauri ya Moshi ambapo jumla ya matrekta madogo ya mkono (Power tiller) 29 na zana zake zimepelekwa ili kutoa huduma ya zana za kilimo kwa wakulima wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kufungua vituo vya zana za kilimo nchini ikiwemo Wilaya ya Moshi vijijini kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.