Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Amb. Khamis Mussa Omar (2 total)

MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali haitoi bei elekezi kwa makato ya huduma za Mobile Money ili kuwapunguzia gharama wananchi?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu Swali Na. 198 la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa huduma za miamala ya fedha kwa mitandao ya simu zinapatikana kwa gharama nafuu. Hatua hizi zimejikita katika kupunguza gharama za miamala ya kielektroniki, kuimarisha miundombinu ya mifumo ya malipo na kuweka mazingira rafiki ya kisera na kikanuni ili kuchochea matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali na kupunguza gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zifuatazo zimechukuliwa kwa kipindi cha mwaka 2024 na 2025: -

(i) Mwezi Aprili, 2024 Benki Kuu ya Tanzania iliweka kikomo cha juu cha gharama ya muamala kwa Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo na Mfumo wa Tanzania Automated Clearing House (TACH) kwa miamala kati ya benki na benki, ambapo gharama ya juu kwa muamala mmoja ni shilingi 2,000.

(ii) Mwezi Aprili, 2025, Benki Kuu ya Tanzania iliendelea kupunguza gharama za miamala ya kutuma fedha kidijitali, ikijumuisha miamala ya kuhamisha fedha kutoka simu kwenda akaunti za benki na kutoka benki kwenda simu kupitia mfumo wa malipo madogo na ya haraka. Gharama za miamala zimepunguzwa na kuwekwa ukomo wa shilingi 5,000 kwa miamala yote inayozidi shilingi 500,000, kwa miamala isiyozidi shilingi 500,000, mwongozo wa ukomo wa gharama kwa kiwango tofauti umeainishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kutoa leseni kwa watoa huduma mbalimbali ili kuhakikisha ushindani katika sekta ya mifumo ya malipo ya kielektroniki. Hadi kufikia mwezi Machi, 2026, watoa huduma 113 walikuwa wameshapata leseni ya kutoa huduma za mifumo ya malipo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kushirikiana na watoa huduma wa mifumo ya malipo ya kielektroniki katika kufanya tathmini ya gharama za miamala na kuchukua hatua zinazofaa za kupunguza gharama ziada, bila ya kuathiri uthabiti na usalama wa mfumo wa malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ya ziada tu ni kwamba, kwa ujumla bado Serikali inaendelea kutumia Sera ya Soko Huria na kuhimiza ushindani wa haki unaozingatia haki ya mlaji na uwazi wa kupatikana taarifa za bei kupitia Benki yetu Kuu, ambayo pia inatoa mwongozo wa bei na tozo mbalimbali.
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa Kodi ya 30% katika export ya Mazao ya Misitu ambayo imeua kabisa Viwanda?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya marekebisho ya Sheria, kulikuwa na usafirishaji mkubwa wa mazao ya misitu nje ya nchi yasiyochakatwa au yaliyochakatwa kidogo na ni mfano wa magogo na Veneer sheets. Hivyo, mwaka 2025 Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Usafirishaji wa Bidhaa Nje ya Nchi, Sura 196 ili kutoza ushuru kwa kiwango cha 30% au shilingi 150 kutegemeana na kiwango kitakachokuwa kikubwa kwa kila kilo moja ya vinia inayotambulika kwa Tariff Heading 44.08 inayosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya marekebisho hayo ili kulinda viwanda vya ndani katika kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za viwanda vyetu vya ndani vinavyotengeneza bidhaa za mbao ikiwemo plywood na marine board. Pamoja na marekebisho hayo, Serikali pia ilifanya marekebisho kwa kuongeza ushuru wa forodha kwa marine board zinazoingizwa nchini kutoka 25% hadi 35% ili kuviongezea viwanda vyetu vya ndani ushindani dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imepokea changamoto aliyoieleza Mheshimiwa Mbunge kuwa hatua hii imeathiri baadhi ya Viwanda. Viwanda vinavyoweza kuathirika ni vile vinavyochakata mazao ya misitu bila kufikia hatua za mwisho za uzalishaji wa bidhaa za misitu kwa matumizi yaliyokusudiwa. Hivyo, Serikali inaendelea kujielekeza kwenye kutafuta suluhu ambayo haitaleta athari hasi kwenye sekta hii ndogo kutokana na hatua zinazochukuliwa ili kuilinda sekta hii muhimu katika uchumi wetu, na pia kwa kuhakikisha kuwa kuna uongezaji thamani wa mazao ya misitu kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Fedha ili kuona namna ya kurekebisha kodi hii pale itakapothibitika kuwa inazuia ukuaji wa viwanda badala ya kuvilinda, ili kuhakikisha mnyororo wa thamani wa misitu unamnufaisha mwekezaji na Taifa kwa ujumla.