Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Amb. Khamis Mussa Omar (2 total)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali kwa hatua ambazo inazichukua katika kuhakikisha kwamba utumiaji wa huduma za kidijitali kwenye utumiaji wa fedha unakuwa na unafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu mimi lililenga kwenye huduma ya simu kwa simu, sikuwa na tatizo kati ya benki na simu, simu na benki, lakini ni mtu kwa mtu. Simu moja kwenda simu nyingine. Ukituma unakatwa fedha, ukipokea unakatwa fedha; mwananchi hana unafuu. Swali langu ni kwa nini kusiwepo na bei elekezi kutoka Benki Kuu kuweka kikomo kama ilivyoweka kikomo kwenye huduma za benki na simu? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni kwa nini Serikali isifikirie kuondoa angalau upande mmoja, kwamba ukituma unaweza ukakatwa, lakini wakati wa kupokea, wapokee bure, ili fedha ziweze zikazunguka na kuwasaidia wananchi wetu kuwaondolea mzigo? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, ninamshukuru sana Mheshimiwa Tarimba Abbas, kwenye swali lake na ni kweli kulikuwa na sehemu muhimu hii ambayo ameitaja ya huduma ya fedha za moja kwa moja, mtu na mtu. Kwenye hili ndiyo nilisema kwamba sera yetu hasa ilikuwa ni kuendelea kuwa na soko huria, lakini kwa kujali masilahi ya mlaji. Kwa sasa hivi hakukuwa na bei kwenye ukomo wa bei, lakini Benki Kuu imeendelea kufuatilia kwa ukaribu gharama ambazo zinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki Kuu imeendelea kutoa mwongozo; na imetoa mwongozo wa ada hizi ambazo zinatozwa na kampuni za simu kwenye huduma za mobile service, imetoa mwongozo mwaka 2024, imesisitiza kuwepo kwa uwazi na disclosure. Kwa hiyo, kila mtoa huduma za malipo ya fedha analazimika kuweka bei ambazo atazi-charge ambazo tunazitumia kwenye huduma za kutuma na kutolea pesa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Benki Kuu imeweka kiwango cha ulinganisho, kimeweka kwenye portal, na pia imeweka na kiwango cha ulinganisho, wenyewe wanaita plus comparator ambayo inasaidia watumaji na watoaji wa huduma kuweza kuona zile charge zenyewe. Kwa hiyo, kwenye ukomo hakujawekwa, lakini kumetolewa mwongozo wa namna ya kuweka chargers mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Tarimba lile la kuondoa upande mmoja, tulichukuwe, lakini kwa sasa hivi bado mtumaji na mtoaji vilevile wanachajiwa kwa sababu wote wawili wanapata huduma.
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Tangu kuanzishwa kwa kodi hii, idadi ya kontena za vinea ambazo zimekuwa zikisafirishwa zimepungua kutoka kontena 3,765 mpaka kontena 2,110 mwaka 2026 hadi mwezi huu Machi. Je, Serikali imefanya tathmini ya kulinganisha mapato inayopata kupitia kodi hii dhidi ya ajira zilizopotea kwenye viwanda vya misitu?
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kunakuwa kuna haja ya kufanya tathmini kwenye athari ambazo zimetokeza kutokana na hatua hizi. Hata hivyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, dhamira moja ya hatua hii ilikuwa ni kupunguza usafirishaji nje ya nchi. Kwa hiyo, kutokana na alichokisema Mheshimiwa Mbunge, inaonekana kweli upande mmoja tumefanikiwa, lakini upande wa pili tunahitaji kufanya tathmini kuona sasa zile faida ambazo zilitarajiwa kama zimepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama ambavyo imesemwa hatua hii ilianza kutekelezwa mwezi Julai, 2025, vipindi ni vifupi kufanya tathmini. Tunalipokea na kwamba tutafanya tathmini kama nilivyosema awali, sisi kwa ushirikiano na Wizara ya Utalii na Maliasili.