Contributions by Hon. Juma Ramadhani Mustafa (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu yenye mwelekeo na mapitio ya kazi za Serikali kwa mwaka 2026/2027. Kwanza kabisa, ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya njema na ametujalia Wabunge wote kufika hapa siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu za kipekee nazipeleka kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri na maono yake mazuri anayoendelea kulitumikia Taifa hili. Hakika uzalendo wake hauna mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa hotuba yake nzuri inayoakisi mwelekeo chanya kwa kazi nzuri za Serikali na ziara zake anazoendelea kuzifanya ndani ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninaomba niwashukuru wananchi wa Jimbo la Igalula kwa heshima kubwa waliyonipa na kunichagua kuwa Mbunge wao wa Jimbo la Igalula. Ninaahidi hapa sitawaangusha, na sitakubali kuona Igalula haipigi hatua za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie. Ninaanza kwenye sekta ya afya. Serikali imeendelea kuwekeza miradi mingi ndani ya sekta ya afya. Hotuba inaeleza miradi 113 inatekelezwa, miradi 45 inatekelezwa ndani ya hospitali za mikoa, na miradi 48 inatekelezwa ndani ya hospitali za halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi 5,000 wameajiriwa ndani ya siku 100 za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali imewekeza kwenye vifaatiba na dawa kutoka 80% mwaka 2024 mpaka sasa 89% mwaka 2026. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zifuatazo ndani ya Jimbo langu la Igalula. Upungufu na ukamilishaji wa vituo vya afya na zahanati, uhaba wa wataalamu wa afya, na umbali mrefu wa wananchi kufuata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Igalula, ninapenda kuishauri Serikali yafuatayo: kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya katika ngazi ya kata zenye upungufu ikiwemo Kata ya Igalula, Goweko, Kizengi, Loya, Tula na Lutende; na ujenzi wa vituo vipya katika kata ambazo hazijafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupeleka watumishi wa afya ngazi ya msingi kwenye kata, vijiji na vitongoji, kuboresha upatikanaji wa dawa hususan katika vituo vya afya na zahanati, na kupandisha kituo cha afya walau kimoja katika Jimbo la Igalula kuwa na hadhi ya hospitali ya wilaya ili kuweza kuepuka adha za akina mama na watoto kutembea umbali mrefu kufuatana na nature ya Wilaya ya Uyui jinsi ilivyo kimuundo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI, Serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI. Takwimu zinaonesha kwamba watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ni takribani milioni 1.7. Uelewa wa watu wa hali ya maambukizi juu ya UKIMWI umefikia 92%, matumizi ya dawa za ARV yamefikia 98.5%, ufanisi wa dawa umefikia 98.1%, na vituo vya kutibu magonjwa ya UKIMWI vimeongezeka kutoka 7,803 mpaka 82,005. Dawa za ARV zinatolewa bure kwa 100%. Serikali pia imekusanya fedha shilingi bilioni 26.8 kupitia Mfuko wa Hifadhi ya UKIMWI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mafanikio, ninapendekeza yafuatayo kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Igalula. Serikali kuongeza utoaji elimu kwa vijana juu ya masuala ya UKIMWI, Serikali kutoa elimu kwa vijana juu ya masuala ya UKIMWI, kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya maendeleo, kuunganisha huduma za VVU na huduma za magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, presha, moyo na afya ya akili, na Serikali kuongeza kwa kasi kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa Kiwanda cha kutengeneza ARV kilichopo Arusha - TPI ili kuendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa za ARV ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali kuwapatia support (moral and material support) watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wanaotengeneza vifaa mbalimbali ili kutambulika na TBS na bidhaa zao kupata soko kwa uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, magonjwa yasiyoambukiza. kama vile Kisukari, Shinikizo la Damu, Saratani, na Afya ya Akili yanaongezeka kwa kasi hapa nchini na kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi wetu. Jambo la kupongeza ni kwamba Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuwekeza kwenye vifaatiba na dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninaiomba Serikali kutengeneza mkakati maalumu wa kitaifa wa kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, kuanzisha uchunguzi wa mara kwa mara katika vituo vya afya, kutoa elimu ya lishe bora na mtindo wa maisha kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie sekta ya miundombinu. Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya miundombinu ya nishati na huduma za kijamii. Hadi kufikia Februari 26 vitongoji 39,003 sawa na 61% vimeunganishwa na umeme. Hii ni hatua kubwa, lakini bado maeneo mengi ya Jimbo la Igalula hayajafikiwa kikamilifu na huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kuhakikisha upanuzi wa umeme vijijini ikiwemo jimbo la Igalula, kuboresha barabara kupitia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini ikiwemo barabara ya Isuli – Miyenze, Misole – Miyenze – Nyahua, Malongwe – Mabeshi, Goweko – Kigwa, Miswaki – Loya, Goweko – Igalula Mpakani na Igalula – Kigwa. Kujenga madaraja maeneo korofi ikiwemo eneo la Loya, Vumilia Kata ya Igalula, Mbulumbulu Kata ya Mmale, Mdaki kata ya Kizengi na Tulieni, Kata ya Tula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vijana na ajira, Serikali imetoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwekeza kwa vijana kiuchumi. Aidha, zaidi ya vikundi takribani 12,977 vimepatiwa mikopo ya 10% na ajira zimeongezeka kwa 31.4%. Pamoja na mafanikio hayo ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umemalizika.
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Pamoja na mafanikio hayo ninapenda kushauri, kwa ujumla ninaipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo. Hata hivyo, utekelezaji wake unapaswa kulenga zaidi wananchi wa vijijini ili kuleta usawa wa maendeleo mijini na vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, ninaunga mkono hoja kwa 100%.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amejaalia asubuhi hii tumekutana hapa ukumbini Bungeni, lakini Mwenyezi Mungu huyo huyo ambae amejaalia amani na utulivu ndani ya Taifa letu limeendelea kuimarika.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu wa Taifa hili kwa juhudi zake ameendelea kuhakikisha Tanzania yetu amani na utulivu imeendelea kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpongeza Waziri wa Wizara hii na viongozi wote wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanahakikisha mipaka yetu ya nchi imeendelea kuwa na amani na amani na utulivu wa nchi yetu umeendelea kuimarika.
Mheshimiwa Spika, sisi sote tunakubaliana hapa hakuna maendeleo bila amani na hakuna amani bila ya kuwa na jeshi imara. Jeshi letu limekuwa ni mfano wa kuigwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na uwekezaji wa muda mrefu ambao umeendelea kufanywa ndani ya jeshi letu. Hii inatuonesha nini sisi kama Waheshimiwa Wabunge, inabidi tuendelee kulipa ushirikiano jeshi letu ili liendelee kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama za kisasa. Kwani changamoto za ulinzi na usalama za kisasa ni ugaidi, uhalifu wa kimitandao, uuzaji wa haramu wa binadamu, lakini hii inatuonesha nini; sisi kama Wabunge inabidi tuendelee kulipa support jeshi letu kwa kulisemea na kuishauri Serikali, ihakikishe bajeti tutakayoipitisha hapa, fedha hizi zinakuja kwa wakati, kusudi jeshi letu liendelee kufanya kazi kwa weledi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio haya, lakini bado kuna changamoto mbalimbali ambazo tunatakiwa tuziangalie ndani ya jeshi letu. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge inabidi tuendelee kuiomba Serikali, iendelee kuboresha makazi ya askari wetu, maeneo ya kufanyia kazi, maeneo ya maisha yao maaskari wetu, lakini matibabu ya askari wetu pamoja na kununua dhana za kisasa za kijeshi. Kwa sababu tunafahamu bila kuiomba Serikali iongeze bajeti na bajeti itakayopangwa iletwe kwa wakati, isipoletwa wanajeshi wetu hawa hawawezi kufanya kazi kwa weledi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi ninaiomba Serikali bajeti hii ambayo tutaipitisha hapa siku ya leo Serikali ijitahidi bajeti yote ije kwa ajili ya kuweza kuimarisha weledi na ufanisi wa jeshi letu. Kuna Jeshi la Kujenga Taifa, jeshi hili ni jeshi ambalo linafundisha uzalendo, linafundisha nidhamu, lakini pia linawawezesha vijana kuweza kuwafundisha mbinu mbalimbali za kuweza kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, mimi ninaiomba Serikali iongezee bajeti Wizara hii, kusudi tuweze kuwa-accommodate vijana wengi waweze kujiunga na jeshi hili. Ikiwa ni pamoja na kurekebisha makambi, kuweza kuongeza makambi yawe na uwezo mkubwa wa kuweza kuchukua vijana wengi na mimi vijana wangu wa Jimbo la Igalula wawe pamoja ambao watakaochukuliwa kwa wingi na kuweza kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jeshi hili la JKT tukilitumia vizuri linaweza likatusaidia kupunguza upungufu wa ajira kwa vijana...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Juma, muda wako umekwisha, ahsante.
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Spika, ninaunga hoja kwa 100%, ahsante ninashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nichangie bajeti ya Wizara ya Kilimo 2026/2027. Kwanza kabisa ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amejaalia mimi na Wabunge wote jioni hii tumekutana hapa Bungeni. Pili, shukrani zangu za kipekee ninazipeleka kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazoendelea kufanya kupitia Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango, kwenye Wizara hii ya Kilimo. Kama jinsi tunavyoona Wizara hii ya Kilimo imeajiri zaidi ya watu 65% Watanzania wa nchi hii. Hata hivyo, inachangia kwenye pato la Taifa zaidi ya 27%, inachangia kwenye Mfuko Mkuu wa pato la Taifa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na faida hizi bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa zichukuliwe hatua za haraka kwenye Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tukiangalia kwenye Ripoti ya Wizara ya Mwaka 2026 inaonesha ongezeko la mazao yanakuwa kwa asilimia 4.5, hii inatuambia nini? Mazao yanaongezeka lakini bado ongezeko la watu haliendani na mahitaji ya chakula nchini. Hapa tunaona kwamba, bado Wizara haijawekeza kwa wakulima wadogo wadogo kwa sababu ndio uti wa mgongo wa sekta hii ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaishauri Wizara ijielekeze kwenda kuwekeza tija zaidi kwa wakulima wadogo wadogo hapa nchini, hasa hasa kuweza kuangalia kwenye masuala ya pembejeo, mbegu zenye ruzuku na kuwatafutia masoko wakulima wadogo wadogo, ndiyo watakuwa wameweka tija kubwa kwenye sekta ya kilimo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio haya ya Wizara, lakini ndani ya Jimbo langu la Igalula bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wakulima wangu. Ucheleweshaji wa pembejeo kufika kwa wakati kwa wakulima hasa vijijini bado inaonekana ni changamoto kubwa sana, licha ya wakulima kulima kwa bidi, lakini bado pembejeo zinachelewa kufika. Zinafika katikati ya msimu wa kilimo na wakati mwingine zinafika zinakuta wakulima kabisa wamemaliza kulima kilimo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri nini hapa? Serikali ihakikishe tunapata pembejeo kwa wakati ili wakulima waweze kulima vizuri na tuweze kupata tija kwenye sekta hii ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, tunaona ni jinsi gani sisi kwenye Mkoa wetu wa Tabora ilani imetuelekeza vizuri. Katika miaka hii mitano, ilani imetuelekeza kwamba inatakiwa tukaongeze uzalishaji wa mbegu kutoka tani 80,000 mpaka tani 19,000; inatakiwa tukaongeze uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 200,000 mpaka tani 300,000 lakini na mazao ya chakula kutoka tani 200,000 mpaka tani 500,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote hatuwezi kuyapata bila kuirejea ilani ambayo imetuahidi kwamba Mkoa wa Tabora inatakiwa tupate kiwanda cha mbolea ndani ya miaka hii mitano ili tuweze kuyashuhudia haya. Watu walioandaa ilani wameyaona malengo haya ya miaka mitano kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Wizara iharakishe mchakato wa kupata Kiwanda cha Mbolea katika Mkoa wa Tabora. Kama watakuwa wanakutana na changamoto zozote za kuhusu maeneo, sisi Wabunge tupo, tutakaa na Viongozi wetu wa Mkoa, kuweza kutafuta maeneo ambayo tutaweza kujenga Kiwanda chetu cha Mbolea Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miundombinu ya skimu ya umwagiliziaji. Takwimu zinaonesha kwamba ni chini ya 10% tu, ardhi ambayo inafaa kuwekezwa kwenye umwagiliziaji ndiyo ambayo imetumika nchini. Ninaiomba sana Wizara iendelee kutafuta fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, tuhakikishe skimu za umwagiliziaji tunakwenda kuzikwamua nchi nzima na hii ndiyo italeta maendeleo ya kweli kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spia, kwa sababu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, sisi Mkoa wa Tabora inatuelekeza kwamba ndani ya miaka hii mitano inatakiwa tukazalishe kutoka ekari 37 za sasa mpaka ekari 150,000. Bila ya kwenda kuzirejea hizi skimu za umwagiliziaji sisi hatutaweza kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara ya Kilimo ihakikishe kwamba Skimu ya Umwagiliziaji ya Bwawa la Goweko inakwenda kujengwa ndani ya miaka hii mitano, lakini Skimu ya Umwagiliaji ya Kata ya Miswaki inakwenda kujengwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JUMA M. KAWAMBA: …Skimu ya Umwagiliaji pia ya Kata ya Loya na yenyewe inakwenda kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazao...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda umekwisha, malizia sentensi ya mwisho.
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Ninapenda kuishauri Wizara kama tunataka maendeleo ya kweli na mageuzi ya kweli kwenye sekta ya kilimo, sera zetu ziende zikawalenge wakulima wadogo wadogo kwa ajili ya kwenda kuleta mapinduzi makubwa na halisi ya kiuchumi nchini.
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)