Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juma Ramadhani Mustafa (3 total)

MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga maeneo ya malisho katika Jimbo la Igalula ili kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Jimbo la Igalula, Halmashauri ya Uyui, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI:-

Mheshimiwa Spika, eneo la Igalula limekuwa na migogoro midogo ya wakulima na wafugaji, hususan katika maeneo ya kulishia mifugo. Aidha, migogoro hii imekuwa ikitatuliwa kupitia maridhiano ya mtu na mtu na hata kuwahusisha viongozi wa Serikali, kwa ajili ya kusimamia taratibu za fidia kwa hasara inayojitokeza. Aidha, Serikali imetenga jumla ya hekta 6,226.92 katika vijiji 16 vilivyopo Igalula.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Matumizi Bora ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuainisha na kutenga maeneo maalum ya wakulima na wafugaji, kwa ajili ya ustawi wa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Pia, Serikali inatoa wito kwa viongozi ngazi ya mkoa na halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa wakati na kuweka utaratibu mzuri wa matumizi bora ya ardhi.
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Daraja la Loya ili liweze kupitika muda wote na kuruhusu shughuli za kijamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Ramadhani Mustafa, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa shilingi milioni 318.9 kwa ajili ya kumlipa Mhandisi Mshauri aliyefanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Daraja hilo la Loya pamoja na madaraja mengine manne katika barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya usanifu imekamilika ambapo shilingi bilioni 26.68 zinahitajika kuweza kujenga daraja hilo lenye urefu wa meta 80 pamoja na madaraja mengine madogo manne. Taarifa zote za usanifu pamoja Kibali cha Mazingira kutoka NEMC tayari kimeshapatikana kwa ajili ya kuruhusu ujenzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi bilioni 10 kupitia Mradi wa Urejeshaji wa Miundombinu katika maeneo yaliyoathirika na maafa ya mvua za mwaka 2024, chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ujenzi wa madaraja mengine manne utafanyika kadiri fedha zitakapopatikana. Kwa sasa TARURA ipo katika hatua ya mwisho ya kumpata Mhandisi Msimamizi wa kazi hiyo na kazi ya ujenzi wa daraja hilo inatarajiwa kuanza kabla ya mwezi Mei, 2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. JUMA M. KAWAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Shule za Msingi na Sekondari, pamoja na miundombinu katika Shule zilizopo Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Mustapha Kawamba, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya vipaumbele vya Serikali katika sekta ya elimu msingi na sekondari ni pamoja na ujenzi wa madarasa, shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali yenye vigezo stahiki kote nchini. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 – 2025/2026 Serikali imetoa shilingi bilioni 4.23 katika jimbo la Igalula, kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za msingi za Mnadani na Izumba Migusa, shule nne za sekondari za Venant Daud, Mmale, Magulyati na Uyui Modern na madarasa 33 katika shule 17 za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2026/2027 Serikali imetenga shilingi bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Mzumba na madarasa 54, ya msingi 40 na ya sekondari 14, pamoja na matundu ya vyoo 10 katika shule mbili za sekondari. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari na kuongeza miundombinu katika shule zilizopo kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.