MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na neema ya mvua ambayo Wilaya yangu ya Nkasi imepata katika msimu huu imepelekea barabara zote za pale Mjini Namanyere kuharibika sana. Sasa mvua imeisha; je, ni lini Serikali itatuwezesha kujenga hizo barabara zilizoharibika vibaya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa ufuatiliaji wake wa mara kwa mara alishakuja Ofisi za Waziri Mkuu, TAMISEMI mara kadhaa na tumemhakikisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua kufuatia mvua hizi nyingi barabara zetu zimaharibika za Jimbo la Nkasi Kaskazini, Wilaya ya Nkasi kwa ujumla lakini pia katika eneo la Namanyere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie kwamba tayari Serikali tumeshatoa maelekezo kwa Mameneja wote wa TARURA kote nchini, TARURA Mkoa na TARURA Wilaya wanaendelea na utangazaji wa zabuni wa 60% ya bajeti kwa ajili ya matengenezo ya haraka na ya dharura kwa barabara zote zilizoathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumsisitiza Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Rukwa na Wilaya ya Nkasi kuongeza speed na kufika pia Namanyere na kuona barabara zilizoharibika ili ziweze kupata kipaumbele kwenye bajeti ambayo tayari tumetangaza kwa ajili ya kupata wakandarasi.