Supplementary Questions from Hon. Eng. Amosy William Maganga (7 total)
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Sikonge kwa hivi sasa wanakabiliwa sana na ufinyu wa maeneo, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wilaya ya Sikonge ina jumla ya mapori tisa na kati ya haya, yaliyo mengi ni mapori ya akiba. Je, Serikali, ni wakati gani sasa haya mapori ya akiba yataanza kutumika, kwa ajili ya hao wananchi, ukizingatia kwamba, kwa kweli wananchi wanahitaji kuendesha shughuli zao za kiuchumi na hasa kilimo, ufugaji, pamoja na urinaji wa asali na kwa hivi sasa, hata viashiria vya uvunjifu wa amani vinaanza kuonekana?
SPIKA: Mheshimiwa swali lako limeshaeleweka. Ahsante.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sikonge, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Utakumbuka Bunge lako hili kipindi cha Mwaka 2021 mpaka 2025 iliundwa Kamati ya Mawaziri Nane, ambayo ilizunguka nchini kote kuainisha maeneo haya na kufanya tathmini. Hivyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tathmini ikikamilika kwa wakati watatengewa maeneo ili wapate kufanya shughuli za uzalishaji mali, kilimo na ufugaji.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja tu la nyongeza. Kwa vile Barabara ya kutoka Ipole – Rungwa imekuwa kwenye ahadi ya Serikali kwa kipindi kirefu sasa na barabara hii imekuwa ni sehemu ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Je, Serikali haioni umuhimu kwamba sasa fedha zipatikane na barabara hiyo ianze kutengenezwa na impendeze Mwenyezi Mungu hii barabara ikamilike hata kabla ya mwaka 2030?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara imeshafanyiwa usanifu na kwa sisi kama Serikali imekuwa ni moja ya barabara kubwa na Barabara Kuu (Trunk Road) ndefu ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami. Tunavyoongea sasa hivi, Serikali inatafuta chanzo sahihi kwa maana ya kuijenga hiyo barabara kuanzia Ipole – Rungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, atakubaliana nami, lakini kutoka Rungwa – Singida ambako tumeshaanza na kutoka Rungwa – Makongorosi ili kuiunga Tabora, Singida na Mkoa wa Mbeya kwa kiwango cha lami. Mpango upo mkubwa wa kutafuta chanzo cha uhakika ili kuikamilisha barabara hiyo. Ahsante.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini kituo chetu cha afya kilichopo Kata ya Kipili, Jimbo la Sikonge, kitajengewa jengo la wagonjwa wa nje (OPD)?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Serikali tumejielekeza katika mwaka huu wa fedha angalau kukamilisha majengo ya OPD katika vituo hivi vya afya na yaanze kutoa huduma. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka huu wa fedha tutakamilisha jengo hilo la OPD na lianze kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tunaishukuru Serikali kwamba tunayo Hospitali ya Wilaya ya Sikonge, lakini haina uzio na kumekuwa na changamoto nyingi sana zinazosababishwa na kukosekana kwa uzio. Je, ni lini Serikali itatujengea uzio katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Sikonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kusisitiza halmashauri, kwanza kufanya tathmini na kutenga fedha za kujenga uzio. Pia tutawasilisha maombi haya TAMISEMI, na kujiridhisha, kisha kuanza ujenzi wa uzio katika hospitali zote za halmashauri.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Mji Mdogo wa Kituo ulio Kata ya Kituo, Wilaya ya Sikonge, baadhi ya barabara zake ziko katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kufungiwa taa. Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ujenzi wa hizo barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Engineer Maganga, Mbunge wa Sikonge, kwamba tunafahamu kuna uhitaji wa barabara za changarawe na za lami katika miji na vijiji katika Jimbo la Sikonge na ndiyo maana kwanza tumeshapokea orodha ya mapendekezo ya barabara za kufungua, kujenga na kukarabati, lakini pia tunaendelea kuandaa bajeti na utaratibu wa kuanza kujenga barabara hizo kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Sikonge kwamba Serikali hii sikivu itakwenda kufanya kazi hiyo kwa awamu kuhakikisha kwamba miundombinu inapitika vizuri.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mji wa Sikonge ni miongoni mwa miji mikongwe sana katika Taifa letu, lakini umekuwa hauna soko kwa muda wote huu, na kwa vile katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi wameahidi kujengewa soko hilo, je, Serikali ni lini sasa itaanza ujenzi wa soko hilo katika Mji wa Sikonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ninatumia nafasi hii kuwakumbusha Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwamba, katika mipango yao ya kila mwaka ni muhimu kuainisha vipaumbele ambavyo ni mahitaji ya juu ya jamii katika maeneo yao, yakiwemo masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, Halmashauri ya Sikonge ni halmashauri kongwe na inahitaji kuwa na soko zuri ambalo litakidhi mahitaji ya wananchi wa Sikonge. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Maganga, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, namwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sikonge kwanza wafanye tathmini ya gharama zinazohitajika katika ujenzi wa soko hilo, waainishe eneo, na pia, waanze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikihitajika Serikali Kuu kuunga mkono, tutaunga mkono wakileta andiko hilo. Lengo ni kuhakikisha kwamba, soko hilo linajengwa.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi na vilevile nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pamoja na majibu hayo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa vile tanki la maji katika Kijiji cha Tumbili, Kata ya Igigwa tayari limeshajengwa na kwa vile tanki hili tayari limeshajazwa maji takribani miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kusambaza maji kwenye kata hizo za Igigwa, Pangale, Ipole, Tutuo pamoja na Mole.
Je, Mheshimiwa Waziri sasa haoni kwamba wakati umefika kwamba hayo maji ambayo tayari yameshajazwa yaanze kusambazwa kwa wananchi hawa ili kuwaondolea adha kubwa ya ukosefu wa maji waliyonayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Kata ya Kilumbi pamoja na Kata ya Kipili wana adha kubwa, wana changamoto kubwa sana ya maji, na suluhu ya kata hizo ni ujenzi wa Bwawa la Kilumbi.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka wataalamu wake ili waweze kufanya tathmini na hatimaye kuanza ujenzi wa bwawa hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Amosy William Maganga, Mbunge wa Sikonge kwa namna ambavyo ameingia na kuhakikisha kwamba anasukuma sana huduma ya maji katika Mji wa Sikonge na kwa namna ambavyo anaendelea kutushirikisha Wizara ya Maji na katika package hii ya Urambo, Kaliua pamoja na Sikonge ni Sikonge pekee ndiyo imekuwa ya kwanza kuhakikisha kwamba maji yanaanza kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi. Hii ni kwa sababu ya msukumo wake ambao anaendelea kutupa ushirikiano sisi Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tanki la Tumbili ni kweli kabisa kwamba tulilijaza maji na Mheshimiwa Waziri alifika Sikonge kwa ajili ya kufanya testing ya yale maji katika lile tanki. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwamba baada ya kufanya test na kukamilika tutaanza sasa kusambaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi ni kwamba tuhakikishe ile miundobinu hakuna maji yatakuwa yanavuja ambayo yatasababisha kupoteza maji. Kwa hiyo, ndiyo maana bado tuko katika hatua za mwisho na baada ya hapo tutaanza mara moja kuhakikisha kwamba watu wako wa Sikonge wanasambaziwa maji ikiwemo kilometa 12 katika maeneo ya pembezoni ambayo Mheshimiwa Rais ameelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili Kata ya Kilumbi; hii ni kata ambayo iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2025/2030 na hivyo bwawa ndiyo suluhisho. Nimtoe hofu, Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu sana na kwa sababu amesema na sisi tutatuma timu yetu kwenda kufanya need assessment. Baada ya hapo tufanye feasibility study na baada ya hapo tufanye usanifu wa kina. Baada ya hapo tupate fedha kwa ajili ya kujenga bwawa kwa ajili ya wananchi wake wa Kata ya Kilumbi pamoja na Kata ya Kipili. Ninakushukuru sana.