Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Jafar Rajab Seif (8 total)
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -
Je, Serikali inachukua hatua zipi kwa Halmashauri ambazo hazitengi fedha za kununua mafuta ya Watu Wenye Ualbino?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa mafuta kwa watu wenye ualbino kupitia halmashari zote nchini. Katika mwaka 2024/2025 Serikali ilitenga shilingi bilioni 8.74, kwa ajili ya huduma za ustawi wa jamii na shilingi bilioni 1.4 zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta maalum ya ngozi kwa watu wenye ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuzielekeza halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya watu wenye ualbino. Katika mwaka 2025/2026 jumla ya shilingi bilioni 1.9 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya watu wenye ualbino kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo ya utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Zahanati Kata ya Nsalala Wilayani Shinyanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, TAMISEMI kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetoa shilingi milioni 44.45 kwa ajili ya ukamilishaji wa boma la zahanati katika Kata ya Nsalala. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2025/2026 imetenga shilingi milioni 22, kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kwa ajili ya ukamilishaji. Ujenzi wa zahanati ya Nsalala utakamilika na kuanza kutoa huduma kabla ya mwezi Juni, 2026.
MHE. HIJA HASSAN HIJA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha, hususan vifaa vya kujifungulia, katika hospitali zote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri ninayeshughulikia masuala ya afya, TAMISEMI. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Hija Hassan Hija, Mbunge wa Kiwani.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi vinavyoendelea kujengwa kote nchini. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano, 2021/2022 hadi 2024/2025, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 285.6, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vikiwemo vifaa vya kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 shilingi bilioni 32 imetolewa, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ngazi ya msingi. Shilingi bilioni 9.6 imetolewa, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali za halmashauri kote nchini.
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga maeneo ya malisho katika Jimbo la Igalula ili kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Jimbo la Igalula, Halmashauri ya Uyui, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI:-
Mheshimiwa Spika, eneo la Igalula limekuwa na migogoro midogo ya wakulima na wafugaji, hususan katika maeneo ya kulishia mifugo. Aidha, migogoro hii imekuwa ikitatuliwa kupitia maridhiano ya mtu na mtu na hata kuwahusisha viongozi wa Serikali, kwa ajili ya kusimamia taratibu za fidia kwa hasara inayojitokeza. Aidha, Serikali imetenga jumla ya hekta 6,226.92 katika vijiji 16 vilivyopo Igalula.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Matumizi Bora ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuainisha na kutenga maeneo maalum ya wakulima na wafugaji, kwa ajili ya ustawi wa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Pia, Serikali inatoa wito kwa viongozi ngazi ya mkoa na halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa wakati na kuweka utaratibu mzuri wa matumizi bora ya ardhi.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-
Je, lini Serikali itakarabati Kituo cha Afya Masama pamoja na nyumba za watumishi wa Kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Saashisha kutoka Jimbo la Hai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Masama kilijengwa Mwaka 1979, hali inayosababisha kuwa na miundombinu michache na chakavu. Kituo hicho kinahitaji miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD), maabara, jengo la huduma za uzazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia, kichomea taka, vyoo vya nje na nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini na kuainisha vituo vya afya kongwe 532 kote nchini, ambavyo vinahitaji kuongezewa na kukarabatiwa miundombinu yake. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 102.08 zinahitajika, kwa ajili ya uboreshaji wa vituo hivyo. Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya kongwe kote nchini, kikiwemo Kituo cha Afya Masama. (Makofi)
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama kuwa Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utolewaji wa huduma za kibingwa. Huduma za kibingwa zinazotolewa ni pamoja na huduma za magonjwa ya ndani (internal medicine), matibabu ya mifupa, magonjwa ya uzazi, magonjwa ya macho, pamoja na huduma za uchunguzi wa mionzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Kahama Manispaa ina upungufu wa miundombinu muhimu ikiwemo jengo la huduma za dharura, jengo la huduma za wagonjwa mahututi na baadhi ya vifaa vya huduma za uchunguzi. Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika hospitali hiyo kisha kufuata Miongozo ya Wizara ya Afya kupandisha hadhi kuwa hospitali ya hadhi ya mkoa.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE aliuliza:-
Je, kwa nini wananchi wa Kata ya Mbalawala wamezuiwa kuendeleza ardhi wanayomiliki kwa maelezo kuwa ni sehemu ya Bonde la Kati Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Inyasi Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini. Bonde la Mzakwe linasimamiwa na Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu Water Basin na Mamlaka ya DUWASA na siyo Bonde la Kati la Singida kama swali lilivyoelekezwa. Bonde hili lilipimwa kisheria na kusajiliwa Aprili, 2000 kwa ramani yenye Namba 45977.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo lina ukubwa wa hekta zaidi ya 34,000 na lipo katika Kata za Chihikwi, Kawawa, Matangizi, Makulu na Mtaa wa Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu zilizopelekea kuzuiwa kufanya maendelezo katika bonde hilo ni kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuwa kuna zaidi ya visima 20 vinavyotoa huduma ya maji yanayotumika na wananchi wa Dodoma Mjini na maeneo jirani, eneo ilo kitaalam lina kimo cha maji kilichopo juu. Serikali imechukua hatua za kusitisha upimaji na umilikishaji pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari ya kuendeleza eneo hilo.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza:-
Je, lini Serikali itadhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mvuha, Selembala, Dutumi, Kisaki, Bwakila Juu, na Kolelo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Yahya Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini:-
Mheshimiwa Spika, kipindi cha kiangazi hutokea adha ya upungufu wa malisho maeneo mengi, ambapo hupelekea wafugaji kuanza kuhama kwa ajili ya kutafuta maji na malisho. Hali hii inasababisha wimbi la wafugaji vamizi kutoka nje ya Wilaya ya Morogoro kuleta mifugo mingi ambayo husababisha mwingiliano na uharibifu wa mazao.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na migogoro, ikiwa ni pamoja na kutenga na kutambua maeneo ya malisho kwa wafugaji kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, ambapo jumla ya vijiji 68 vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi kwa kutenga hekta 54,577. Watendaji wote wa vijiji na kata kutoruhusu wafugaji wageni kuingia kwenye maeneo yao bila kufuata taratibu, kuhamasisha uzalishaji wa malisho ili kuongeza upatikanaji wa malisho kwa wafugaji.
Mheshimiwa Spika, wizara za kisekta zimeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa elimu ya ufugaji wenye tija wa kuwa na mifugo michache.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama kufanya operesheni maalum ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Morogoro. Pia, Serikali inapopata tetesi ya mgogoro kwa wafugaji na wakulima, Viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya hufika kwa wakati na kuhakikisha migogoro inatatuliwa.