Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Jafar Rajab Seif (23 total)
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa majibu haya mazuri. Uhalisia wa site ni tofauti na fedha ambazo zimeelezwa kwenye jibu la msingi kwamba, zinatengwa. Nini Kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba, mafuta haya yanapatikana kwenye halmashauri na Manispaa zetu, sambamba/sawasawa na fedha zinazotengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya shilingi milioni 182 zimetengwa kwa wanufaika 14,695 waliopatiwa mafuta ya lotion na pia, utambuzi unaendelea kufanyika katika maeneo yote. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Stella, kwenye maeneo ambayo bado utambuzi haujafanyika, tuendelee kuwatambua. Ni maelekezo ya Serikali kwa Wakurugenzi wetu kuendelea kuwatambua wahitaji wa mafuta haya.
MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuwepo mahali hapa, Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa Mbunge, Viti Maalum, kundi la Wenye Ulemavu. Bila kuwasahau wapigakura wangu wote nchi nzima, ninawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni kwamba, Wizara ina mpango gani wa kuajiri Madaktari wa Afya ya Ngozi, maalum kwa ajili ya watu wenye ualbino kwenye hospitali zote za halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa hawa watu kwenye halmashauri utasaidia kupanga bajeti ambayo wao watakuwa na idadi kamili ya mafuta na hata kufanyiwa check-up, siyo tu lotion; check-up kwa ajili ya watu wenye ualbino kwenye halmashauri zote, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha kwanza na kipindi cha pili, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kundi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli tayari tumewaelekeza madaktari wote wa halmashauri ambako kuna uhitaji mkubwa wa wenye changamoto ya ngozi. Hivyo, pamoja na wataalamu wale 5,000 ambao tumewaajiri mwezi Januari, wamo ambao wanahusika na kufanya utambuzi wa changamoto hizi za ngozi, pamoja na kutoa ushauri katika matibabu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Nderiananga.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba niongeze jambo kwenye eneo la mafuta kwa watu wenye ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uhitaji wa mafuta ya ualbino kwa watu wenye ualbino nchi nzima, lakini ninamhakikishia dada yangu, Mheshimiwa Stella kwamba, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Waziri wetu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi, tunao Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu Tanzania ambao kwa sasa tayari tumetenga fedha. Kupitia kwenye mfuko, tuta-push fedha hiyo ndani ya wiki mbili, tangu sasa, ili iende KCMC ika-produce mafuta mengi zaidi yaweze kusambazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili kupitia wenzetu Wizara ya Elimu, tunasambaza mafuta haya kwa wanafunzi. Tunanunua, kama eneo la vifaasaidizi, moja kwa moja yanawafikia shuleni. Kwa hiyo, nawatoa wasiwasi wenzangu wenye ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema na hili la pili kidogo. Tuna hospitali ambazo ni teule, kama hospitali za kanda. Kwa mfano, kule Mwanza Bugando yanafanyika matibabu hayo ya kufanya screening tangu mwanzo, watoto wanapokuwa wadogo, kwa ajili ya kutambua level yao ya aina ya ngozi, mafuta na kila kitu ambacho wanatakiwa wapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna KCMC, tuna Ocean Road na tunaendelea kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kusambaa hadi chini. Kwa hiyo, nawahakikishia watu wenye ualbino wasiwe na mashaka, tuko vizuri. Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia ya Kazi na Utu Tunasonga Mbele, tutaendelea kupeleka huduma kwao, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Buchambi, Wilaya ya Maswa ina wakazi wengi, lakini haina kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya kwa Kata ya Buchambi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katika Bunge lako Tukufu tayari tulishapeleka fedha za kujenga vituo vya kimkakati katika Majimbo 120. Majimbo mengine 94 tumeshayaombea fedha Hazina, nayo yatapata kwa awamu ili kuweza kukamilisha ujenzi wa vituo hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge Esther kwamba Wilaya ya Maswa ni wanufaika katika ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Afya cha Kazulamimba, Kituo cha Afya cha Kata ya Mwakinzega na ni lini pia Serikali…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge swali la nyongeza ni moja tu.
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge akiulizia kuhusu Kituo cha Afya cha Kazulamimba. Kituo cha Afya cha Kazulamimba ni pamoja na vituo vya afya 341 ambavyo tumeviainisha. Tutaendelea kutenga fedha za ndani za halmashauri na zile za Serikali Kuu ili kuhakikisha kituo hiki cha afya kinaanza kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Afya inataka kila Kata kuwa na kituo cha afya, lakini katika Jimbo la Kigoma Kaskazini mpaka sasa Kata za Mkongoro, Mkigo, Nyarubanda, Nkungwe, Mungonya, Kidahwe na Matendo hawana vituo vya afya na wakinamama wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya. Ni lini Serikali itakamilisha sera hii kwa kuleta vituo vya afya katika Kata hizi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Kiza Mayeye, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, kwa kazi kubwa anayoifanya hapa Bungeni ya kufuatilia maendeleo ya Jimbo la Kigoma Kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kujenga vituo vya afya katika Kata zote. Awali tulianza na zile Kata za kimkakati kulingana na mahitaji na vipaumbele. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Kiza Mayeye, ndani ya awamu hii tunakwenda kujenga vituo vya afya kulingana na vipaumbele katika Jimbo la Kigoma Kaskazini. (Makofi)
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali la nyongeza. Katika Zahanati ya Imalakaseko iliyopo Kata ya Goweko, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora, Serikali ilitoa shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto lakini wodi hiyo bado haijakamilika. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa wodi hiyo ya mama na mtoto katika zahanati ya Imalakaseko, Kata ya Goweko, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amegusia hasa katika zahanati ya Imalakaseko, Halmashauri ya Uyui. Kwanza Serikali imeshatenga shilingi milioni 80 kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Pia, ninamwelekeza Mkurugenzi kuendelea kutenga fedha za ndani Halmashauri ya Uyui ili kuweza kukamilisha ujenzi wa zahanati hii. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Lukozi ni kati ya vituo vya kimkakati ambavyo vimetengewa fedha na Serikali. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunaipongeza Serikali kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kilipelekewa fedha shilingi milioni 250 za awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaombea wale Waheshimiwa Wabunge ambao hawajapata, yale Majimbo 94, lakini tumeshawaelekeza Wakurugenzi wote katika Halmashauri kuendelea kutenga fedha za ndani ili kuhakikisha huduma zinatoka katika vituo vyetu vya afya, na maeneo yote yenye upungufu tutayaombea fedha Hazina. (Makofi)
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba nimuulize swali moja la nyongeza. Mwezi Novemba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye hospitali moja hapa Mjini Dodoma na wananchi, hususan wazazi, waliipongeza Serikali kwa huduma nzuri za matibabu na dawa, lakini walilalamikia ukosefu wa mabeseni na ndoo, kwa ajili ya wajawazito; Mheshimiwa Waziri Mkuu akaagiza jambo hili litatuliwe. Ninaomba kujua limefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hija Hassan Hija. Tunakumbuka ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye kituo chetu, kile cha afya na akatoa maelekezo yale.
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo maelekezo ya Serikali. Nami kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninawaelekeza Waganga Wakuu wote wa Mikoa, Waganga wote, ma-DMO wa Halmashauri na ma-MOI wetu waendelee kutekeleza majukumu hayo, waendelee kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maana kwamba, sasa mambo ya kuwatoza hivyo vifaa kama mabeseni na ndoo visiwe vikwazo kwa mama zetu wanapokwenda kujifungua katika hospitali zetu
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri na amesema, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo, lakini maelekezo haya mpaka tunavyozungumza huko kwenye vijiji wajawazito bado wanapeleka mabeseni wembe na mipira. Ninataka majibu ya Mheshimiwa Waziri kuanzia sasa, ni lini hii hali itakoma kwa wajawazito kwa sababu, Kigoma Kaskazini na maeneo mengine bado akinamama wanapeleka mabeseni na vifaa vingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni maelekezo ya Serikali. Ninarudia kwa kwamba, halmashauri zote nchini tunatoa wito kwa Wakurugenzi, Waganga Wakuu na ma-DMO watekeleze maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa maana maagizo hayo ndiyo maagizo ya Serikali.
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara. Kwanza kabisa ninapenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya, lakini ninampongeza Mheshimiwa Rais, wananchi wa Jimbo la Igalula wanamshukuru kwenye chanjo ya ruzuku, kuondoa na utambuzi wa mifugo.
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza; je, Serikali ina utaratibu gani wa kisheria na kiutendaji, ili kuhakikisha sasa maeneo haya yaliyotengwa hayavamiwi na hayabadilishiwi matumizi ili kuweza kuepuka migogoro kati ya wakulima na wafugaji ndani ya Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Igalula, Halmashauri ya Uyui, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na Sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikitu-guide na zimepitishwa na Bunge lako Tukufu. Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, hii ilikuwa inatoa hati ya Hatimiliki ya Kimila, lakini kuna Sheria ya Ardhi Namba Sita ya Mwaka 2007, ambayo imeainisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, lakini kuna maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo, yote yameainishwa katika Sheria hii. Sambamba na sheria hizi pia, kuna Sheria Namba 287, ambayo imewezesha halmashauri kutunga Sheria Ndogo. Kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaziagiza Halmashauri zote nchini zifuatishe Sheria hizi na kuona zinatatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Sikonge kwa hivi sasa wanakabiliwa sana na ufinyu wa maeneo, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wilaya ya Sikonge ina jumla ya mapori tisa na kati ya haya, yaliyo mengi ni mapori ya akiba. Je, Serikali, ni wakati gani sasa haya mapori ya akiba yataanza kutumika, kwa ajili ya hao wananchi, ukizingatia kwamba, kwa kweli wananchi wanahitaji kuendesha shughuli zao za kiuchumi na hasa kilimo, ufugaji, pamoja na urinaji wa asali na kwa hivi sasa, hata viashiria vya uvunjifu wa amani vinaanza kuonekana?
SPIKA: Mheshimiwa swali lako limeshaeleweka. Ahsante.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sikonge, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Utakumbuka Bunge lako hili kipindi cha Mwaka 2021 mpaka 2025 iliundwa Kamati ya Mawaziri Nane, ambayo ilizunguka nchini kote kuainisha maeneo haya na kufanya tathmini. Hivyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tathmini ikikamilika kwa wakati watatengewa maeneo ili wapate kufanya shughuli za uzalishaji mali, kilimo na ufugaji.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwatengea maeneo wananchi wa Wilaya ya Bunda, Nyatwali, kwa ajili ya ufugaji ambapo maeneo hayo yalitwaliwa na Serikali kurudishwa hifadhini. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuwatengea wananchi, hasa wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ujumla, maeneo ya kulishia wanyama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu hapo awali, swali hilo linaenda sambamba na swali la Mbunge kutoka Sikonge kwa maana ya kwamba ile Kamati ya Mawaziri Nane bado wanafanya kazi na tathmini ili tuweze kuwatengea maeneo wananchi wetu waweze kuendelea na shughuli za uzalishaji.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nini maswali mawili ya nyongeza: swali la kwanza; wakati tukisubiri Serikali ilete fedha, kwa ajili ya ukarabati, je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuanzisha huduma ya upasuaji kwenye kituo hiki, ambayo ni huduma muhimu sana kwa watu wa Masama?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Hospitali ya Wilaya ya Hai iko katikati na inapokea wagonjwa wengi sana wanaotokana na ajali kwenye maeneo mbalimbali kwenye Barabara yetu ya Arusha kwenda Moshi, lakini mpaka sasa hivi hatuna theatre, kwa ajili upasuaji. Je, Serikali ni lini italeta fedha ya kujenga theatre, kwa ajili ya upasuaji katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Hai? [MANENO HAYA SIYO SEHEMU YA TAARIFA RASMI ZA BUNGE]
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kituo chetu cha Afya cha Masama, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali ya msingi. Pili, ninamwelekeza Mkurugenzi kuendelea kutenga fedha za ndani na kuanza ujenzi wa jengo la upasuaji katika Kituo chetu cha Afya cha Masama.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tayari halmashauri ilijenga jengo la upasuaji katika Hospitali ya Hai na tayari kazi za upasuaji zinafanyika pale, wataalam wangu wameni-brief. Ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge, kama taarifa hazijafika kwa wakati, ninamwomba DMO aweze kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge, lakini pia, Mkurugenzi anifikishie taarifa sahihi kwa Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba, Hospitali ya Hai imeshaanza matibabu hayo ya upasuaji hadi upasuaji wa mifupa. (Makofi) [MANENO HAYA SIYO SEHEMU YA TAARIFA RASMI ZA BUNGE]
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Serikali iliahidi kujenga vituo vya afya vya kimkakati, ili wananchi wasiendelee kufuata huduma katika umbali mrefu sana. Katika Wilaya yetu ya Kilolo kuna Kata za Kimara, Idete, Ukwega, Kwiugumu na Image, wananchi wanapata mateso sana kufuata huduma za afya na barabara hazipitiki. Mpaka sasa hivi madaraja hayapo…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, je ni lini sasa hivi vituo vya kimkakati vitajengwa, ili wananchi wasiendelee kupata mateso makubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilimetenga bajeti ya zaidi ya vituo 120 katika majimbo 120 vya kimkakati, zaidi ya shilingi bilioni 30. Tayari tumeomba fedha zingine, kwa ajili ya majimbo 94 pamoja na yale majimbo ambayo ni mapya, yote yataingia katika mpango huo na tutakwenda kujenga hivi vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Hunyari kimejengwa ni miaka mitatu sasa hakina jengo la upasuaji. Wananchi wenyewe wakaamua kujenga jengo na Serikali ikasema itakwenda kuwasaidia kulimalizia. Sasa ni lini jengo hili litakwenda kumaliziwa kwenye Kituo cha Afya cha Hunyari? Ninakushukuru
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere. Kwanza tunawapongeza wananchi kwa hatua waliyochukua na kuanza kujenga majengo hayo katika hospitali aliyoiainisha. Ninamwelekeza Mkurugenzi aweze kutenga fedha na kuanza ujenzi wa majengo yanayopelea katika hospitali hiyo.
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza naanza kwa kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuletea pesa wiki iliyopita shilingi bilioni 1.4, kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali yetu ya Magunga. Hospitali ya Magunga imezeeka sana, imechakaa na ina umri karibu miaka 73 sasa. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari twende pamoja katika hospitali ile, kwa ajili ya kufanya tathmini, ili ikiwezekana tufikirie kujenga majengo mapya badala ya kuendelea kuweka viraka katika hospitali ile, ambayo inakuwa ni gharama kubwa zaidi kwa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pamoja na timu ya wataalam tutaongozana pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwenda kwenye hospitali hiyo kufanya tathmini na kuendelea kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema, Kituo cha Afya cha Kasekese na Kituo cha Afya cha Mwese kuna tatizo kubwa la ukosefu wa Jengo la Mama na Mtoto, Maabara na nyumba za watumishi. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha,ili iweze kukamilisha hivyo vituo vya afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kwamba, zaidi ya vituo 532 vimeishatengewa bajeti ya shilingi bilioni 102.08. Kwa hiyo, pamoja na vituo ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha vimo katika ukarabati huu mkubwa na kuweza kujenga majengo mengine ambayo yanahitaji, kama maabara, ili kuendelea kupata huduma kwa wananchi wetu.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusu kuboresha huduma katika hospitali yetu ya Manispaa ya Kahama, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali inatenga bajeti kwa ajiili ya kuboresha huduma kwa kujenga jengo la dharura na kuweka vifaa vya uchunguzi kwa maana ya CT- Scan. Sasa ni lini Serikali ina mpango wa kupeleka CT- Scan kwenye hospitali hii ambayo inapokea wagonjwa wengi sana kutoka hospitali zingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini sasa Serikali ina mpango wa kuboresha na kukamilisha majengo ya zahanati ambayo yamefikia hatua za lenta kama vile Chalya, Nyandekwa na sehemu zingine za Wilaya yetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngayiwa. Kwanza, ninampongeza Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI anatoa michango mizuri kwa ajili ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kweli kwa idadi kubwa ya wagonjwa ambao tunawapokea katika hospitali hii ya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na uhitaji wa CT- Scan kwa ajili ya upimaji, uchunguzi wa mifupa kwa wagonjwa wetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba ndani ya muda mfupi Serikali imekwishafanya tathmini na uhitaji huo tumeshauona, tunaipeleka CT-Scan pale ili iende kutoa matibabu kuwahudumia wahitaji wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu zahanati nilikwishaeleza hapa kwamba zaidi ya zahanati 1,841 zinakwenda kufanyiwa ukarabati na kumaliziwa maboma, Serikali inajielekeza zaidi katika miradi hii ambayo tayari imekwishaanzishwa ili tuweze kuikamilisha kabla ya kuanza miradi mingine ya zahati na vituo vya afya. (Makofi)
MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata yangu ya Mpepo katika Wilaya ya Nyasa ndiyo kata ya pili kwa ukubwa katika Wilaya yangu. Kwa bahati nzuri inapakana na nchi ya jirani ambapo mwaka jana ilisababisha maambukizi ya ugonjwa wa M-Pox kutoka katika nchi ya jirani, lakini kata hiyo mpaka sasa pamoja na unyeti wake haina kituo cha afya. Nini kauli ya Serikali ili kulinda maisha ya wananchi wa Nyasa kutokana na njia hiyo ambayo imeonekana inapitisha magonjwa mengi na bado hakuna sehemu ya afya ya kuwalinda wananchi wangu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inaendelea kupambana na haya magonjwa ya mlipuko, kupitia vile vituo vya kimkakati Mheshimiwa Mbunge ataweza kutuambia kama kituo hicho kiende kikajengwe katika kata hii, yeye mwenyewe atatupa uelekeo huo na tutaona namna gani ya kwenda kuboresha katika kituo chetu cha afya hicho na tunaweza tukajenga kituo cha kimkakati katika Jimbo hilo.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mitaa hii mitano na siyo Kata, Mitaa hii mitano ilipimwa kama vijiji mwaka 1973. Je, ni hatua gani Serikali inachukua kuwanusuru wakazi wa Kata hii ya Mbalawala wapatao takriban 12,000 ambao wanategemea ardhi hii kwa maisha yao ya kila siku? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati Serikali inajiandaa kutwaa Bonde la Mzakwe iliwafidia wakazi wa vilivyokuwa vijiji vya Mzakwe na Mchemwa, baadhi kuwahamishia katika Kata ya Chahwa ambayo sasa hivi iko kwenye Jimbo la Mtumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wakazi wa mitaa hii ya Kata ya Mbalawala ili wapishe Bonde la Mto Ruvu kama ilivyowafidia waliokuwa wakazi wa Vijiji vya Mzakwe na Chahwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Inyasi, Mbunge wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la pili, kwa maana kwamba sisi TAMISEMI ndiyo wamiliki wa ardhi, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona namna gani ya kuendelea kuwafidia wale ambao hawajapata kwa sababu Serikali imeendelea kutoa fidia katika maeneo mengi sana nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Ardhi kuona namna gani tunaweza tukafikisha maendeleo haya kwa wananchi wetu kwa maana ya kwamba vijiji vimeshapimwa toka mwaka 1973, tuone namna gani sahihi ya kuendeleza eneo hili. (Makofi)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Spika, ninaomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kutokea katika swali langu la msingi.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; mpaka hivi sasa ninavyozungumza hapa bado kuna mifugo katika mashamba ya wakulima huko katika Jimbo la Morogoro Kusini. Nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa hivi ili iweze kutekelezwa na mifugo hiyo iondolewe katika mashamba ya wakulima?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara ina mpango gani sasa katika Jimbo la Morogoro Kusini kuongeza ujenzi wa majosho, malambo pamoja na kasi ya kuelimisha wafugaji juu ya ufugaji bora wa kisasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa maswali yanayogusa changamoto hizi za wakulima na wafugaji. Sisi Ofisi ya TAMISEMI tunashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo na wameendelea kutoa elimu wenzetu Wizara ya Mifugo na pia wanatoa mbegu za ruzuku kwa ajili ya malisho ili kuondoa migogoro hii kabisa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha mifugo inaondolewa katika maeneo ya wakulima wetu na baadae nitakaa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo ili tuweze kuyaangazia maeneo haya na kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kujenga majosho mengi nchini. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuweze kuainisha eneo ambalo hasa amelizungumzia ambalo halijapata majosho mpaka sasa ili tuweze kujenga majosho hayo.
MHE. LUCY D. S. KOMBANI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hii migogoro imekuwa ya muda mrefu sana na inaleta madhara makubwa sana kwenye hizi jamii zetu na kwa upande mwingine tukiangalia tuna wataalam ambao wamesomea utatuzi wa migogoro; je, Serikali haioni haja sasa ya kuwatumia wataalam hawa katika kumaliza haya matatizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025 hakujaripotiwa migogoro yenye kuleta mapigano katika maeneo mengi nchini. Serikali inamuahidi Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuwatumia wataalam hawa ili kuweka hali hii ya usalama wa wakulima na wafugaji. Tunaendelea kuhamasisha zile kampeni (kwa mfano, Kampeni ya Tutunzane) ili kuona kabisa wakulima na wafugaji wanavyohitajiana na waweze kuishi katika maeneo kwa usalama na uzalishaji mali uendelee.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu hivi ninavyozungumza kuna mgogoro mkubwa wa wafugaji na wakulima na kusababisha mashamba ya wakulima kuliwa na mifugo ya wafugaji. Je, Serikali ina kauli gani kuwalazimisha hao wafugaji ambao wamesababisha hasara kubwa kwa wakulima waweze kulipa gharama zote za uzalishaji na badala yake kuwaachia Polisi kushughulikia suala hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia migogoro ya wakulima na wafugaji ni eneo sensitive sana na Serikali huwa haijiweki katika eneo la kupendelea, hivyo niwaelekeze wahusika wote wa halmashauri za vijiji na halmashauri zetu waweze kufuatilia mgogoro huo na waripoti kwa wakati ili tuweze kwenda kutatua tatizo hilo. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunaweza kuonana baadaye ili tuweze kuona namna gani ya kuli-handle hili bila kuleta pressure katika pande zote. (Makofi)