Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Moses Ludovico Kaegele (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Kilimo. Ninatumia fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kuwepo mahali hapa, lakini pia, ninatumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake yote kwa namna ambavyo amewekeza kwenye kilimo. Ukiangalia bajeti hii, zaidi ya shilingi trilioni 1.2 inaenda kutekeleza ajenda ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. Ninajua amejikita sana pia, kwenye umwagiliaji na ninajua umwagiliaji unaenda kuwaokoa sana wakulima wadogowadogo pale ambapo miradi hiyo itaenda kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana kwenye kushauri na pia, kuomba. Ninaanza na suala la bei ya mahindi. Mwaka huu wa Fedha NFRA walinunua kilo moja kwa shilingi 700 na ukiangalia dunia ilivyo kwa sasa na mambo yanayoendelea duniani, unaona kwamba, ni lazima tu kama si mbolea basi ni mbegu, gharama zitaongezeka. Ukiangalia wakulima wetu, hasa wa Jimbo la Nkasi Kusini, wao wanategemea sana wauze mahindi, ili wakanunue mbolea ili wakanunue mbegu. Hali hii inaonesha nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kwamba, wanapokwenda kujiandaa na msimu unaofuata ni lazima Serikali, kupitia NFRA, waone namna ya kuongeza hata shilingi 150 kilo ifike shilingi 850, ili wakulima hawa waweze kumudu gharama za kilimo na pia, kumudu gharama za maisha. Watu wa Mkoa wa Rukwa na Jimbo la Nkasi Kusini ili ununue nguo au ununue ng'ombe au ukatibiwe ni lazima uuze mahindi. Ndiyo maana ninaiomba sana Serikali, suala la bei ya mahindi waone namna ya kuongeza hata shilingi 150 kuwasaidia hawa wakulima kuweza kumudu gharama za uzalishaji, lakini pia, gharama za maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni upatikanaji wa mbolea ya ruzuku. Ni kweli sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa na Jimbo la Nkasi Kusini tunatamani kuona kwamba mbolea inapatikana kuanzia mwezi Agosti, Septamba hadi wa Oktoba. Ukiangalia kuna muda mwingine mbolea zimekuwa zikichelewa na hii inakwamisha wananchi wengi kutokuingia kwenye kilimo na kuvuna mavuno mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nimesoma mwongozo wa usambazaji wa pembejeo za ruzuku, nimeona pale kuna jambo ambalo kama Wizara wanatakiwa walitazame. Kwanza hawa mawakala wanapofuata mzigo kwa maana ya mbolea kwa makampuni wanaenda kuwauzia wananchi kwa bei nzuri sana, lakini pale ambapo makampuni wanasafirisha zile mbolea kupeleka Mikoani wanawauzia wale mawakala kwa bei ambayo inawalazimisha wao wakauze ile mbolea nje na bei elekezi ya TFRA. Ninaishauri Serikali kwanza kuna umuhimu wa Serikali kuangalia namna ya kutoa mwongozo wa bei elekezi kwa makampuni ambayo wanaenda kusambaza mbolea kwa mawakala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo bei elekezi inawasaidia sana mawakala nao wanunue kwa bei nzuri na wao wakawauzie wakulima kwa bei ambayo ni elekezi kutoka TFRA. Niombe sana Serikali, wananchi kimsingi wanaponunua kwa bei ambayo siyo elekezi kwanza wanaona mbona tumesikia taarifa ni hii, lakini imekuja taarifa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la ombi, Mheshimiwa Waziri ninajua kwamba yeye ni mpambanaji, mpiganaji, watu wa Jimbo la Nkasi Kusini wanaomba mambo mawili tu. Kwanza, wanaomba maghala katika Jimbo la Nkasi Kusini, hadi sasa tuna ghala na wanasafirisha mazao yao mbali sana kutafuta soko, lakini la pili, wanaomba visima vinne kwa ajili ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo pekee la Nkasi Kusini ndiyo halina miradi ya umwagiliaji, ukiangalia Bonde la Kati, Bonde la Kipande, Bonde la Kizumbi na kadhalika wanahitaji visima virefu ili siku ya siku waweze kuendesha kilimo cha umwagiliaji. Ninawapongeza kwamba sasa wana magari zaidi ya 19 ambayo yanachimba hadi mita 1,800 kwenda chini kwa maana ya visima virefu vya umwagiliaji. Hizi nyenzo ni muhimu sana, zitatusaidia sana sisi wananchi wa Jimbo la Nkasi Kusini kama tutapata hivyo visima tuweze kuzalisha kwa muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi na niseme kwamba, ninaunga mkono hoja. (Makofi)