MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kijiji cha Tundu ni kijiji chenye wakazi zaidi ya 3000 na kijiji hicho kipo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, namna pekee ya kufikia pale kijijini ni njia ya maji. Tokea ziwa limechafuka wakazi wa pale hawafikiki. Je, ni lini serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufungua Barabara kutoka Kala kwenda Tundu na kujenga madaraja mawili ili wananchi hawa waweze kupata huduma za msingi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninaomba nikiri kuwa Mheshimiwa Mbunge alikwishakuja ofisini kwenye ofisi zetu za TAMISEMI. Tumekwishakaa na watalam, tumeangalia umuhimu wa barabara hii ambayo ipo pembezoni kabisa, lakini inaenda kwenye kata yenye wakazi zaidi ya 3000. Kupitia mradi wetu wa Mheshimiwa RISE tunaangalia uwezekano wa kuweka madaraja; ambapo yanahitajika madaraja takribani matatu; ili tuweze kufungua uchumi kwa eneo lile na kusaidia wananchi wetu wa eneo lile.