MHE. JOHN J. NCHIMBI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha kukoboa Kahawa Nyasa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, ninaomba nijibu swali namba 79 la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nyasa inazalisha kahawa aina ya Arabica kwa wastani wa tani 2193 kwa mwaka. Kutokana na uzalishaji huu, Mheshimiwa Rais aliona umuhimu wa kuwa na kiwanda katika eneo hili. Hivyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Nyasa imetenga eneo lililopo Kitongoji cha Ndanda, Kijiji cha Kingirikiti Kata ya Kingirikiti kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kukoboa kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili lina ukubwa wa hekta nne na lina miundombinu wezeshi kama vile barabara, maji na umeme. Aidha, eneo hili linamilikiwa na Serikali na lipo tayari kwa ajili ya uwekezaji kwa kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa. Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. JOHN J. NCHIMBI aliuliza: -
Je, lini Serikali itatoa mikopo nafuu ya Boti za Uvuvi za Fiber kwa Wavuvi wa Wilaya ya Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ninaomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa shilingi bilioni 200 kwa vijana ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani kwa ajili ya kufanya biashara ndogo, za kati na kampuni changa. Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ilitoa tangazo tarehe 4 Machi, 2026 ili kuujulisha umma juu ya fursa ya mikopo nafuu kwa vijana ili kupata mitaji na kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mikopo hiyo inalenga kutoa vifaa na pembejeo muhimu za ufugaji samaki kwa vizimba, zana za uvuvi, ufugaji wa kuku, ufugaji wa nguruwe, ufugaji wa mbuzi na kondoo, miundombinu ya ubaridi, uchakataji wa dagaa pamoja na mwani katika maeno yote ya wavuvi hapa nchini; wakiwemo wavuvi wa Wilaya ya nyasa. Ninatoa rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kuwahamasisha vijana kujiunga kwenye vikundi na vyama vya ushirika ili waweze kunufaika na mikopo hii isiyokuwa na riba na yenye masharti nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha