Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. John John Nchimbi (2 total)

MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata yangu ya Mpepo katika Wilaya ya Nyasa ndiyo kata ya pili kwa ukubwa katika Wilaya yangu. Kwa bahati nzuri inapakana na nchi ya jirani ambapo mwaka jana ilisababisha maambukizi ya ugonjwa wa M-Pox kutoka katika nchi ya jirani, lakini kata hiyo mpaka sasa pamoja na unyeti wake haina kituo cha afya. Nini kauli ya Serikali ili kulinda maisha ya wananchi wa Nyasa kutokana na njia hiyo ambayo imeonekana inapitisha magonjwa mengi na bado hakuna sehemu ya afya ya kuwalinda wananchi wangu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inaendelea kupambana na haya magonjwa ya mlipuko, kupitia vile vituo vya kimkakati Mheshimiwa Mbunge ataweza kutuambia kama kituo hicho kiende kikajengwe katika kata hii, yeye mwenyewe atatupa uelekeo huo na tutaona namna gani ya kwenda kuboresha katika kituo chetu cha afya hicho na tunaweza tukajenga kituo cha kimkakati katika Jimbo hilo.
MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza baada ya kupata majibu haya mazuri. Swali la kwanza; Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais anapokuwa ametoa ahadi na pia ahadi hiyo inapokuwa imewekwa katika Ilani ya chama ni ahadi ambayo inatakiwa itekelezwe na Serikali na siyo kuwasubiri Private Sectors ambao wanaweza wakaja muda wanaopenda wao na ikapita hata miaka mitano inayotarajiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je Serikali haioni umuhimu wa kukusanya wataalam wake waende kuwasaidia wananchi wa wilaya yangu kuwezeshwa kusaidiwa kupata mikopo ambayo ni ya riba nafuu kutoka maeneo ya Serikali kama Agricultural Bank, TIB na Benki ya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa John John Nchimbi kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Ni kweli ninaungana naye Mheshimiwa Rais anapotoa ahadi jukumu letu sisi kama Serikali ni utekelezaji wa ahadi hiyo. Kimsingi Serikali imeshaanza utekelezaji wa ahadi hiyo na ndiyo maana Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imeshatoa miche 2,000,000 kwa wakulima wa kahawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo wameshanunua eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda, uzalishaji wa kahawa Nyasa umeongezeka na ndiyo maana kuna umuhimu wa ujenzi wa kiwanda. Ukisoma Dira ya 2050 inazungumzia ushirikishwaji kwa maana tunazungumzia Uchumi Jumuishi na Sekta Binafsi ina mchango wa 70%. Ndiyo maana Serikali kupitia taasisi za fedha, kupitia wadau kama Vyama vya Ushirika tunaendelea kuhamasisha kuwekeza katika viwanda vya kati ili kushiriki kikamilifu katika dhana ya Uchumi Jumuishi kama nguzo ya Dira ya 2050 inavyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la uwezeshaji wa Serikali ninaungana na Mheshimiwa Mbunge. Ndiyo maana sisi kama Serikali tumeshatoa mwongozo kwa halmashauri kuona kwamba mazao ambayo yanatokana na maeneo husika tunaenda kuyajengea uwezo Vyama vya Ushirika. Pia kuomba fedha maalum kupitia bajeti ya Serikali kuona uwezeshaji wa ujenzi wa viwanda hivyo ili kuongeza mnyororo wa thamani, kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama ya uzalishaji na kuchochea uzalishaji katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.