Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia siku hii ya leo katika bajeti hii ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha sisi sote tuna afya na tumeweza kuwemo ndani ya hili Bunge. Pia, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo anatusimamia na kutuongoza kama Kiongozi wetu Mkuu katika nchi yetu hii ya Tanzania. Pamoja na yeye niwapongeze sana na kuwashukuru wasaidizi wake wa karibu Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali hasa Wizara yetu hii ya Nishati. Kiukweli bila kificho na kila mmoja na kila Mtanzania anaona jinsi gani ambavyo Wizara ya Nishati inafanya kazi nzuri hapa Tanzania. Wizara hii imekuwa ni mojawapo ya Wizara ya mfano katika kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata umeme. Siyo kupata umeme tu hata katika service pale ambapo kunakuwa kuna changamoto Wizara hii watu wake wamekuwa waki-respond kwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana watendaji wote wa TANESCO Tanzania kwa jinsi ambavyo wana-respond kwenye matatizo ya umeme yanavyokuwa yametokea kwa uharaka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee sana ni ushahidi uliotosha kabisa kuona jinsi ambavyo Wizara imeshughulika na suala la mafuta. Nchi zingine jirani tunaona kwamba kuna changamoto kubwa na wengine wamefika sehemu hata vituo havina mafuta lakini kwa Tanzania tunajivunia Wizara yetu, tunajivunia Mheshimiwa Rais wetu kwa jinsi ambavyo amehakikisha masuala ya mafuta kwetu Tanzania hatujapata upungufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi tunavyozungumza, kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba, mafuta tunayo na siyo tu kwa taarifa, ukienda kwenye vituo Tanzania nzima utakuta vituo vyote vimefunguliwa na mafuta yanapatikana. Kwa jambo hili ninapenda kuwapongeza sana Wizara ya Nishati ambayo inaongozwa na Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na mambo mazuri hayo, ninapenda kusema jambo moja. Katika maisha changamoto inapotokea inatengeneza fursa. Sasa katika suala zima la changamoto ya mafuta ilivyotokea tumeona kwamba, kuna fursa zingine zimejitokeza ambazo, kama Serikali na kama Wizara na kama Taifa, tunahitaji kuharakisha na kuongeza nguvu kuhakikisha tunaendelea kwenye hivyo vipaumbele vingine, ili pale ambapo mafuta yanaleta changamoto tuweze kupata njia mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hapa tunayo gesi, lakini pia, tunao umeme ambao tunaona kabisa kwamba, tuna mpaka excess. Tunajua kwamba, nchi zingine duniani zinabadilika, zinatoka kwenye kutegemea sana mafuta zinaenda kwenye kutegemea gesi pamoja na umeme. Sisi hapa Tanzania, wale ambao tumefanikiwa kwenda kwenye maonesho ya TANESCO pale, kwenye Wizara ya Nishati tumeona gari ambalo linatumia umeme. Kama leo tungekuwa tunayo magari mengi Tanzania yanayotumia umeme tusingekuwa tunawaza sana mafuta kwa sababu tungekuwa tume-switch na tunatumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kuangalia pia, Tanzania hapa tunayo gesi na kuna magari tayari yameanza kutumia gesi. Ombi langu na ushauri wangu sasa kwa Serikali ni kwamba, tuongeze kasi kwa Tanzania nzima kuongeza hizi filling station za gesi, tuongeze hizi sehemu za kuchaji magari, ili tuhamasishe Watanzania wengi zaidi waweze kuagiza haya magari na inapotokea crisis kama hii, basi tuweze kupata alternative ambayo watu wanaweza wakatumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia magari ya Dangote yanaweza yakatoka kule Mtwara mpaka Dar es Salaam kwa kutumia gesi, lakini hayo hayo magari ya Dangote hayawezi kuondoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza, kuelekea Kanda ya Ziwa kwa kutumia gesi. Wakifika Dar es Salaam inakuwa ni kituo na huku hivi inakuwa hakuna. Kwa hiyo, tukifanikiwa kuongeza filling stations za gesi na umeme watu hawatanunua magari na tutapunguza tatizo la mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ninaomba pia, niweze kuzungumzia jambo moja lingine ambalo ninatamani niishauri Wizara yetu ya Nishati. Tunajua kabisa miundombinu yote ya umeme inamilikiwa na TANESCO, muundombinu wowote unapokuwa mahali popote huo muundombinu unaanza kumilikiwa na TANESCO. Sasa Wizara imesema kuna Sheria ipo inaruhusu mwekezaji kujiunganishia umeme halafu akawa anarudishiwa kwa asilimia kidogo kidogo, hela kiasi inaenda kwenye Wizara na kiasi anajirudishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tunalifahamu watu wachache sana. Ninaiomba Wizara iende kutangaza jambo hili, iwafahamishe wawekezaji, ili kila mwekezaji anapotaka kuweka umeme, anapokuwa na mradi wake, asisubiri TANESCO mpaka ipate bajeti, asisubiri Wizara mpaka ipate bajeti, aweze kujivutia umeme akiwa na assurance kwamba, ile pesa itarudishwa. Maana kama akiwa na assurance hiyo atapeleka hakika umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, kuna jambo kubwa ambalo ninalichukua kuwapongeza sana REA. REA wamefanya kazi kubwa hapa Tanzania, wamesambaza umeme, umefika sehemu nyingi sana, lakini kuna jambo moja dogo ambalo wakati mwingine linachafua ule uzuri wa jambo lile ambalo limefanyika; kuna sehemu moja unakuta mwananchi mmoja anafanyiwa connection na REA na mwananchi mwingine anafanyiwa connection na TANESCO. Gharama za ku-connet watu hawa ambao wako sehemu moja ni tofauti. Ninaiomba Serikali iende ikafanye tathmini upya kwa jambo hili. Ione jinsi gani inaweza ikasimamia na kuondoa hizi dosari ndogo ambazo mwisho mwisho wa siku zinaweza kuharibu jambo kubwa zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na Mungu awabariki sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Madini. Awali ya yote, ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa jinsi ambavyo ameendelea kutupa afya na tumeendelea kufanya kazi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii pia, kumshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jinsi ambavyo ameendelea kuisimamia Serikali na hasa katika Wizara yetu hii ya Madini ambapo tunaona kwamba kila kunapokucha pato lake limeendelea kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu, nitajielekeza katika masuala kama manne hivi. Suala la kwanza ambalo nilitamani kuchangia ni katika eneo la utafiti. Wizara inayo mkakati mzuri ambao inauita Vision 2030, ambapo mpango huu unamaanisha kwamba tunapofika mwaka 2030 tuwe tumeweza kufanya utafiti kufikia 50% na sasa hivi tumeshafanya utafiti kwa 16% tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ombi langu kwa Wizara na Serikali kwamba jambo hili tumaanishe na ili tumaanishe ni lazima tutenge fedha kwa ajili ya jambo hili. Ukiangalia katika taarifa ambayo imesomwa mwaka jana katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026, ni shilingi bilioni 10 tu ya maendeleo ndiyo ambayo imeshatoka ambayo hiyo ndiyo inaenda kufanya suala zima la utafiti, lakini ukiangalia hata hiyo shilingi 10,000,000,000 ambayo ni asilimia nane imeenda kwenye majukumu ambayo siyo direct kwenye utafiti, yameenda kujenga ofisi na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwendo huu ni kweli kabisa kwamba tunavyofika 2030 bado lengo hili hatutakuwa tumelifikia. Ninaiomba Wizara, lakini ninaiomba Serikali iweze kuona kwamba kuna haja kuanzia sasa hivi kutenga fedha za ndani kwa ajili ya utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulikuwa tunategemea fedha za nje na hazikuja na hakuna kilichofanyika. Kwa hiyo, ninaomba sana tunapofika hitimisho la bajeti hii, Mheshimiwa Waziri basi ahakikishe kwamba wanaangalia utaratibu mwingine wa kupata fedha kwa ajili ya utafiti. Tunaamini kama tutafanya utafiti tukafika 50% na kama sasa hivi pato la Taifa kwenye Sekta ya Madini linachangia 11.9%, basi litaenda ku-double na tuki-double Serikali yetu itaenda kupata fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo ninataka kuchangia ni sehemu ambayo tumekuwa na wageni wengi sana Tanzania wakichukua leseni za wachimbaji kwa kigezo cha technical support. Sasa hivi ukiangalia Tanzania nzima kuna wageni wengi wapo lakini kigezo kikubwa wanachokitumia ni kwamba wamekuja kutoa technical support na ukiangalia kazi wanazozifanya ni zile zile ambazo Watanzania wanazifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mikataba hii inayoingiwa na Watanzania kwenye leseni na hao wageni imekuwa ni kiini macho kiasi kwamba kile kinachoandikwa kwenye makaratasi sicho kinachotekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Wizara, ninajua kwamba ina namna nyingi za kufanya auditing, tufanye auditing kwenye hii mikataba yote ya technical support iliyopo, tuone kwanza ni aina gani ya technical support inayotolewa na hao wageni kwa Watanzania. Pia, tuone huu mkataba ulioandikwa kwamba huyu Mtanzania, huyu mwenye leseni atapata asilimia kadhaa, je wanaipata kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba sana Wizara tunapomaliza Bunge hili la Bajeti basi twende tukahakikishe tunaangalia, tuna-review, tunaangalia hii technical support. Kweli Watanzania hatuna uwezo hapa? Wizara kama wizara, hizo technical support zinazotolewa na hao wageni hatuwezi kuzitoa hapa ndani tukaacha kuuza maeneo na leseni zote kuzitoa kwa wageni kwa kigezo cha technical support? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuzungumzia eneo lingine la CSR. CSR kweli ninaipongeza migodi imekuwa ikitoa CSR ambayo imesaidia maendeleo katika maeneo ambayo yanazunguka migodi. Hata hivyo, CSR hii imekuwa na changamoto kubwa sana. Ninachukulia mfano pale Geita Mjini katika Mgodi wetu wa GGM pale. Toka mwaka 2018 na kule nyuma CSR ilikuwa inatolewa na Mgodi wa GGM kwa jinsi watakavyoona inafaa, lakini mwaka 2018 baada ya kukaa vikao na majadiliano wakakubali kutoa kwa mwaka shilingi bilioni 5.02. Mpaka leo tunavyozungumza 2026 mgodi wa GGM unatoa CSR shilingi bilioni 5.2. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuangalia 2018 dhahabu ilikuwa inauzwa shilingi 100,000 kwa gramu lakini sasa hivi dhahabu inauzwa shilingi 390,000 kwa gramu. Mgodi wa GGM umeongeza uzalishaji. Mwaka ule ulikuwa unatoa CSR, tukiangalia kwenye CSR, ulikuwa unatoa service levy kama shilingi 800,000,000 lakini sasa hivi inatoa shilingi bilioni 7.5 kiasi kwamba uzalishaji umeongezeka, mapato yameongezeka almost mara 10, lakini CSR imebaki kutolewa ile ile ambayo ilikuwa inatolewa 2018 mpaka leo 2026 tunapata CSR ile ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara na ofisi yako, tunapomaliza Bunge hili tubadilishe hizi taratibu twende tuka-discuss tukubaliane. Hoja yangu sasa ni kwamba tuangalie kiasi hiki kinachotolewa. Kweli kama kipindi kile tulikuwa tunazalisha almost sasa hivi tume-triple karibu mara 10 ya uzalishaji wa kipindi kile. Mapato yameongezeka karibia mara 10 lakini CSR imeendelea kutolewa ile ile ambayo ilitolewa miaka 10 iliyopita kuna haja ya kubadilisha na kutafuta mfumo mpya wa kutoa hii CSR. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, CSR hii inayotolewa hata hiyo ndogo inayotolewa, hata hiyo ndogo inayopatikana, utaratibu wake wa manunuzi wa kutekeleza miradi umekuwa mgumu sana. Sasa hivi unakuta kwamba kuanzia zabuni inatangazwa, inasimamiwa na mradi unasimamiwa na Mgodi wa GGM lakini halmashauri au manispaa inaenda tu kukagua au kukabidhiwa mradi. Ninaomba tubadilishe utaratibu, manunuzi yafanyike Halmashauri, Mgodi wa GGM ubaki na fedha kwa ajili ya kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itapunguza gharama kubwa ambayo tunaingia ya kutekeleza miradi kwa kiwango kile kile ambacho Serikali inaweza kutekeleza kwa gharama ndogo, lakini tunapotekeleza kwa kutumia mgodi tunatekeleza kwa kutumia gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ila siyo kwa umuhimu, ninaomba kanuni zibadilishwe kwa sababu mwisho wa siku baada ya uchimbaji huu kuendelea kuna siku moja madini yataisha na yakiisha hii migodi itaondoka. Tuwe na utaratibu kulingana na hizi pesa tunazozipata tuzibadilishie kanuni na sheria ili basi iweze kutengeneza miradi ya uchumi ambayo itaendelea kudumu kwa miaka mingi na itaendelea kutoa ajira na kutengeneza mzunguko wa fedha ili hata pale itakapoondoka tusiendelee kutekeleza tu miradi ambayo Serikali inaweza kutekeleza kwa fedha zake za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ninaomba nizungumzie double taxation ambayo inafanyika katika Wizara hii ya Madini. Kule kule kwenye uchimbaji tunao wachimbaji ambao kiukweli ninaipongeza Wizara imewapa leseni za kutosha na kwa kweli wana leseni nyingi ambazo wanachimba sasa hivi lakini tumekuwa na double taxation. Tumekuwa tukichaji mrabaha mpaka mara tatu kwa wachimbaji hawa wa wadogo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge, muda wako umekwisha. Tunashukuru sana kwa mchango wako.
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)