MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii kwa ajili ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Nianze kwa kuipongeza Wizara ya Madini, ndugu yangu Mavunde kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, lakini pamoja na hayo ninaomba kuuliza swali moja.
Mheshimiwa Spika, tunajua kabisa kwamba suala zima la double taxation limekuwa halikubaliki lakini kwenye Wizara hii ya Madini suala zima la mrabaha tumeona double taxation mara kadhaa ikifanyika. Kuna baadhi ya mikoa ambapo tuna-charge mara mbili. Mara moja tuna-charge wakati mchimbaji anavyokuwa anagawa mawe pia wakati mwingine mchimbaji huyu aki-process akipata dhahabu akifika kule sokoni tena anatozwa mrabaha. Je, Wizara imejipanga vipi au ina mpango gani kuhakikisha kwamba suala zima hili la double taxation tunaliondoa na huyu mchimbaji aende kulipa kodi moja kwa mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba kodi zilizoidhinishwa rasmi na Wizara ni kodi ya mrabaha, kodi ya ukaguzi wa leseni na ile ya service levy inayokwenda kwenye halmashauri. Hizi tozo anazoongelea Mheshimiwa ni tozo ambazo watu wanapotoa madini mgodini na wakati huo ni mawe tu, anayetoa mawe mgodini, anapoyapandisha pale siyo yeye anayepeleka sehemu ya kuchakata yale madini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hakuna namna sisi tunaweza tukasubiri yaende mpaka kule mwisho wa eneo itakapotumika kuweza kuchaji. Kwa hiyo, anatozwa kwa asilimia ya mawe aliyogawa pale baada ya kutoa na yule anayekwenda kuchakata anawekewa kiwango ambacho kinalingana na zile tozo za Serikali.
Mheshimiwa Spika, tuko katika mpango wa kuhakikisha kwamba katika migodi yote uchenjuaji ufanyike palepale ili mawe yotozwe kodi ya Serikali baada ya kuwa yameshachakatwa.
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini kwa majibu yake mazuri, lakini niseme tu kwamba wote humu ndani tunajua kwamba tunazalisha dhahabu nyingi Tanzania na hususani katika Mkoa wetu wa Geita, lakini dhahabu yote hii tunai-export, tunaisafirisha kwenda nje bila kuitengenezea vifaa vinavyotokana na dhahabu. Tukiweza kutengeneza vifaa hivi kama pete, mikufu na vinginevyo ambavyo vinatokana na dhahabu tutaenda kuongeza ajira, mapato, lakini pia tutakuwa sasa tunatengeneza Tanzania tuna-export, tutategemea tutopata wageni, lakini tutapata watalii.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha kwamba tunaanzisha kituo maalum cha utengenezaji hivi vitu ambavyo vinatokana na dhahabu ili basi tuweze kuhakikisha kwamba vijana na wajasiriamali wa Geita wanaweza kuhusika moja kwa moja kwenye mnyororo huo wa utengenezaji wa vitu hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; endapo itatokea Serikali haina mpango wa moja kwa moja wa kuanzisha kituo hiki, je Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi au Halmashauri ya Manispaa ya Geita kuwawezesha kuanzisha vituo hivi, maana ninaamini kabisa kwamba kwenye Geita na Taifa hili litaenda kuwa na faida kubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Chacha kwa maswali yake mazuri na pia nimkaribishe katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa sababu nina taarifa kwamba hivi karibuni amepata kuelekezwa awe Mjumbe wa Kamati hiyo. Ninajua kwamba ni Engineer mwenye uzoefu na tunahitaji kuvuna hazina ya elimu aliyonayo katika Wizara ya Madini.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nijibu sasa maswali yake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, viwanda vya kuchakata madini na kutengeneza bidhaa za mlaji wa mwisho (end user products). Tayari zipo katika sehemu mbalimbali nchini kama nilivyoelezea kwenye majibu ya swali la msingi, lakini kwa upande wa huko Geita sasa na kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anataka kujua hasa bidhaa zinazotokana na dhahabu ni kweli kwamba sasa hivi dhahabu nyingi inachakatwa, wanachoma, wanatengeneza zile ground bars na zinauzwa hivyo hivyo ila ni kwa Geita tu na baadhi ya maeneo mengine nchini, lakini tayari tuna viwanda vinavyochakata dhahabu na kutengeneza bidhaa za dhahabu.
Mheshimiwa Spika, moja ya mfano hai ambao upo na hata Wanageita wanaweza kwenda kujifunza ni Kiwanda cha Banjul Limited kilichoko Dar es Salaam ambacho kinafanya biashara ya kuchakata madini ya dhahabu na kuuza dhahabu nje kama wanavyouza wengine, lakini pia wanatengeneza vidani, mikufu, pete, bangili, lakini siyo ya dhahabu tu na madini mengine mbalimbali ikiweko madini ya metali pamoja na madini ya vito.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia katika kujibu swali lake la pili kumwelekeza Mheshimiwa Mbunge, ashauriane na Halmashauri yake maana na yeye ni Mjumbe Halmashauri ya Geita siyo maskini, wakitaka kuanzisha kiwanda cha kuongeza thamani ya madini ya dhahabu na kutengeneza bidhaa za mlaji wa mwisho, sisi kama Wizara tuko tayari kutoa ujuzi na elimu kwa kuwaletea wataalam waweze kuanzisha kiwanda ambacho kitahakikisha kwamba dhahabu ile inatengenezewa bidhaa mbalimbali zinazoweza kutumika nchini na Watanzania wote, siyo lazima kuuza bidhaa ambazo zimechakatwa tu kwa asilimia Fulani.
Mheshimiwa Spika, tunaweza kutengeneza bidhaa za mlaji wa mwisho na wako wengi ambao ninapenda kuwapongeza wanaotengeneza bidhaa za madini ya vito hasa kule Arusha ambako kuna kile chuo chetu cha TGC, lakini pia kuna wadau mbalimbali katika mikoa mbalimbali nchini, Mererani pia wanafanya hivyo katika madini ya Tanzanite na Dar es Salaam kuna watu binafsi ambao wanajishughulisha na biashara hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tuko tayari kama Wizara kuiwezesha Halmashauri ya Geita kwa kuwapa utaalam ili waweze kuanzisha kiwanda cha kuchakata madini au kituo kikubwa kama kile cha Tanzanite City Center.