Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amina Mussa Mkumba (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. AMINA M. MKUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika Hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Maji 2026/2027. Awali ya yote, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, karimu kwa kuniwezesha kusimama hapa kuchangia katika hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na chama changu, Chama Cha Mapinduzi kwa kuniwezesha kuwa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaomba pia kuwashukuru sana wananchi wa Kibiti kwa imani kubwa waliyonipa, ninawaahidi imani hiyo nitailinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa michakato mbalimbali, kwa hatua nyingi ambazo amezifanya katika kuhakikisha kwamba anamtua mama ndoo kichwani; na sisi Kibiti tumeshuhudia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, kaka yangu Jumaa Aweso, Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Meneja wa Maji Kibiti, Mabula, Meneja wa Maji Mkoa, kiukweli wanatupa ushirikiano sana, ninawapongeza sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake. Tumeona juhudi mbalimbali za kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji; na mwenyewe ametumia neno hapa la kutangatanga na ninawatia moyo katika juhudi zao na Mwenyezi Mungu atawajalia na Tanzania itapata maji. Nipongeze pia hali ya upatikanaji wa maji Tanzania. Upatikanaji wa maji vijijini umefikia 85.2% mwishoni mwa mwaka 2025; hiyo ni hatua kubwa, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote hizo, sisi katika Wilaya yetu ya Kibiti bado tuna changamoto nyingi katika maji. Katika eneo la Kibiti kuna eneo la visiwani ambapo kwa sasa hatuna miradi yoyote ya maji; na katika eneo hilo kuna Kata tano za Mbuchi, Kiongoloni, Msala na Makaloni. Niiombe sana Wizara, kwa sababu katika kata hizo kuna wananchi wengi na wanahitaji huduma ya maji, wahakikishe kwamba wanatenga bajeti kwa ajili ya kwenda kuweka miradi ya maji katika kata hizo. I(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi ambayo imeshakamilika, lakini inatoa maji ya chumvi. Tuna Mradi Mchungu ambao unatoa maji, lakini unatoa maji ya chumvi. Niiombe Wizara ihakikishe kwamba inafanya process za kusafisha maji ili watu waweze kunywa maji mazuri, masafi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna madeni ya wakandarasi. Kuna Mradi wa Nyanjati, mkandarasi anadai shilingi milioni 200; Mradi wa Jaribu Mpakani, mkandarasi anadai shilingi milioni 100; Mtunda shilingi milioni 150. Sasa labda niulize Wizara, ni lini wakandarasi hawa watalipwa madeni yao ili watu waanze kupata maji safi na salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nipongeze sana wizara kwa mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba Taifa letu linapata maji kwa miradi mikubwa kwa ajili ya Gridi ya Taifa ambayo inaunganisha Ziwa Victoria na maeneo mengine ambayo yana uhaba wa maji. vilevile Bwawa la Kidunda ambalo litahakikisha kwamba maeneo ya Dar es Salaam na Mikoa ya Pwani tunapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, niendelee kuwapongeza Wizara na pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapambania wanawake wa Tanzania na kuhakikisha kwamba mama anapata unafuu katika utafutaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja Wizara hii kwa asilimia mia moja. Ninashukuru sana. (Makofi)