Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amina Mussa Mkumba (2 total)

MHE. AMINA M. MKUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuna Mradi wa maji Mchungu katika Jimbo la Kibiti, Kata ya Mwambao na Mradi huu unatoa maji yenye chumvi nyingi sana, Serikali ina mpango gani wa kufunga mtambo desalination plant ili watu waweze kupata majisafi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kubaini changamoto ambayo wananchi wanapitia katika kutumia maji ambayo yana chumvi. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba kwa mujibu wa Sera yetu ya Maji ya Mwaka 2002 Toleo la Mwaka 2025, tunatakiwa kuhakikisha watu wanapata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, ninatumia fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Maji, kuelekeza wataalamu wetu waende wakafanye tathmini, kwanza, kama inawezekana kuyatibu yale maji na ili yanyweke bila ya kuwa na changamoto ya chumvi, ama kama maji hayo chumvi yake ina concentration kubwa ambapo haiwezekani, basi tutafute chanzo kingine tukachimbe kisima ili kuhakikisha kwamba tunawafikishia wananchi huduma ya maji yaliyo safi na salama, ninakushukuru sana.
MHE. AMINA M. MKUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itatenga bajeti ili kuanzisha miradi katika Jimbo la Kibiti katika maeneo ya Visiwani ambapo kuna kata nne: Kata ya Kiongoroni, Mbuchi, Maparoni na Msala? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijue ni jimbo au wilaya gani, kwani ni kata tu amezitaja.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Amina, ninaomba uulize swali lako tena, lakini tunaomba Waheshimiwa Wabunge tupunguze sauti ili tuweze kusikilizana.

MHE. AMINA M. MKUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali langu linauliza, ni lini Serikali itaanzisha miradi katika Jimbo la Kibiti, maeneo ya Visiwani ambapo kuna Kata nne za Msala, Maparoni, Kiongoroni na Mbuchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kutekeleza miradi yote na kuikamilisha ili iweze kutoa matokeo kwa wananchi. Pia, ni dhamira ya Serikali ya CCM ambapo falsafa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani. Hapo ni Sera yetu ya Maji ya Mwaka 2002 ambapo toleo la mwaka 2025 linatutaka kuhakikisha kwamba maji yawe siyo zaidi ya meta 400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, dhamira hiyo hiyo inatusukuma kuhakikisha kwamba tunaweka msukumo kwenye kupeleka fedha ili miradi mbalimbali iendelee kutekelezwa ikiwemo na miradi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiongelea, Tutakwenda kuipatia msukumo mkubwa ili iweze kutekelezwa na kukamilika na kutoa matokeo na wananchi ambao wamemtuma kuwasemea ili sauti yako iweze kutambulika kwa matokeo zaidi ambayo yatakuwa yametokea katika jimbo lake. Ahsante sana.