Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kija Limbu Ntemi (3 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ndiye aliyetufanya na kutupa uhai mpaka kufika siku ya leo tuko hapa tumesimama tunazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nataka nisome kidogo maandiko Matakatifu. Warumi 13:1 ili kuonesha kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa nini yupo amekaa pale kwenye kile kiti, Biblia yangu inasema kwamba, “Kila mtu na atii mamlaka iliyo kuu, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, na ile iliyopo imeamriwa na Mungu.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni chaguo la Mwenyezi Mungu, ndiyo maana amemuweka pale. Hata sisi ambao tumefika humu siku ya leo, nasi pia tumepitishwa na Mwenyezi Mungu kupitia vyama vyetu, ndiyo maana tumefika humu na tunazungumza katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi kwa kuchaguliwa kupitia Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgombea naye kuwa Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Spika wa Bunge, ninakupongeza na wewe Naibu Spika Daniel Sillo kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika katika Bunge hili kwa kura nyingi 100% nadhani zote zilipatikana. Ninampongeza pia Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa pia kuwapongeza wananchi wa Katoro walionichagua kuwa Mbunge au mwakilishi wao walionipigia kura nyingi za kutosha ili niwe Mbunge wao katika Jimbo la Katoro. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Katoro ninayeongoza wananchi wote, wawe wa upinzani wawe wa chama gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndiye Mbunge wao na mimi niko tayari kufanya nao kazi kwa namna yoyote ambayo tutaongozwa na kwa sababu tuna Rais jemedari kabisa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tutawatumikia wananchi wote wa Katoro wa vyama vyote na wa itikadi zote ambazo zipo katika Jimbo la Katoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye mambo machache. Jambo la kwanza nizungumzie suala la madini. Ninaomba kupendekeza jambo moja kwa Wizara ya Madini, kama itawapendeza, tufike hatua basi turuhusu wachimbaji wetu ambao wapo wa kati na wadogo, kama inawezekana kutunza mali zao katika Benki ya BoT au benki ny,ingine watunze na kuweza kupata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa ungekuwa umetunza mali kuanzia mwezi wa Kwanza au mwezi wa 12, leo mchimbaji mdogo angeuza kwa fedha nyingi sana kwa soko ambalo lipo kwa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza benki zetu zitoe nafasi au fursa ya kutunza mali katika benki zetu. Kama mtu anao mtaji wa kutosha na hahitaji kuuza mali yake kwa siku hiyo, aweze kuitunza iwe akiba na akihitaji kuchukua fedha benki, apatiwe nafasi ya kuchukua fedha benki kwa dhamana ya mali aliyoiweka benki katika benki zetu ili imsaidie kufanya maendeleo na kupiga hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Wizara ya Nishati ambao hata mimi ni mnufaika wa umeme ambao sasa nitakwenda kupata kaya 4,151 zinakwenda kuwashiwa umeme. Ninawapongeza Waziri wa Nishati pamoja na Naibu wake ambao wamekubali hata kwenye nyumba za matope wanakwenda kuwasha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu kule Katoro kuna nyumba nyingi. Nimemwambia Naibu Waziri Salome Makamba aje atuwashie umeme kwenye zile nyumba ambazo ni za matope kwa sababu ni haki ya wananchi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwashiwa umeme katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametujengea shule nzuri nyingi na mahiri Katoro. Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Profesa Shemdoe alifika akashuhudia shule nyingi za kisasa ambazo zimejengwa Katoro kwa fedha za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wale ambao hawajaona shule nzuri, njooni mshuhudie Katoro, kuna shule nzuri ambazo amejenga Rais ambazo ni bora na imara zinazotoa mafunzo kwa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu jambo moja, tunapoelekea katika mipango hii na kusaidia vijana wetu, kuna vijana ambao wako mtaani, wengine wamemaliza shule, lakini baadhi ya vijana hao hawajapata vyeti vyao, vipo chuoni mpaka leo, lakini wapo wanazurura mtaani. Wengine wameanza kujiajiri. Mmoja nimemkuta anafanya kazi ya car wash, lakini amemaliza chuo ni kijana mzuri na ni mwalimu, anakwambia sina cheti cha form four na cha chuo viko wapi? Viko chuo vimeshikiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui Wizara imejipangaje kusaidia hawa vijana ili wapatiwe vyeti vyao. Wanapoomba ajira wanaambiwa mpaka uende na cheti original, anakitoa wapi cheti original? Cheti original kiko chuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoenda na mipango hii tukumbuke kuna vijana ambao vyeti vyao hawana, lakini wanataka ajira. Ndiyo hawa ambao tunawaona kila siku huenda wanatangatanga kutafuta ajira, lakini ajira hawapatiwi kwa sababu hawana vyeti katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tu kupongeza na kusema kwamba, tunapoendelea kujipanga na huu mpango wetu niwakumbushe Wizara ya Fedha pamoja na Waziri wa Mipango, sisi Katoro tuna uvuvi mkubwa sana, tunahitaji tungepata viwanda vya kuchakata Samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile viwanda vinavyochakata samaki ili kuwasaidia wananchi wetu wanapovua samaki, maana tuna samaki wengi sana. Katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imeeleza, kupata kiwanda kimoja cha samaki, mtusaidie ili wananchi wetu waweze kufanya biashara nzuri wanapokwenda kuuza bidhaa zao katika maeneo hayo ya viwanda ili waweze kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ninapenda kulizungumzia ni hili jambo ambalo ni kama tu la kupongeza sasa. Tunamshukuru Rais mambo ambayo ameyafanya; ukisikia mtu anayesema Mheshimiwa Dkt. Samia hajafanya; Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipatiwa hii nchi na mtangulizi wake Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli akiwa ameacha Daraja la Busisi kwa asilimia ndogo sana kukamilika, lakini leo sisi tunaotoka Katoro, tunaotoka Geita, tunapita pale kwa dakika tatu tu, na huyu ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyekamilisha daraja hili. Leo tunavuka kwa kishindo kikubwa tukitokea Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunakaa masaa matatu, mpaka manne, mama huyu aliachiwa daraja hili likiwa lina asilimia kama 20, leo limekamilika. Tumpongeze, tumtie moyo, tumtie shime, tumuunge mkono, tushirikiane naye ili aweze kutuongezea, aweze kutusaidia kutuvusha mpaka kufika 2030, tuweze kupata maendeleo makubwa katika sehemu zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru sana kwa nafasi hii kwa ajili ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Madini. Kwanza nimpongeze Waziri wa Madini, kaka yangu Anthony Mavunde kwa kazi anayofanya, anafanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Mavunde sifa zake zimevuma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu moja nimpongeze kwa kutoa leseni katika eneo la Kigosi, alifanya kazi kubwa sana, alikuwa na malengo ya kutoa leseni 6,000 ila akapitiliza akatoa leseni 9,000. Ni 146% zaidi ya kiwango ambacho alikuwa amejipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mavunde amekuwa mtu mwema sana wa kutoa maeneo kwa wachimbaji wadogo. Tumeona alitoa eneo lile la Sengerema – Igalula juzi juzi hapa leseni zimeshatoka, watu wamepata ili wakafanye kazi, kwa sababu Waziri anajitahidi kuwasaidia watu ili waweze kufanikiwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze katika eneo ambalo ninataka nizungumzie kidogo kiujumla Wizara ya Madini wanafanya vizuri. Asubuhi ma-RMO wa Mikoa yote hapa nchini walikuwepo, tulitamani kuwapongeza kwa kazi wanayoifanya kumsaidia Waziri wa Madini kutekeleza majukumu katika kila eneo wale ma-RMO wakiongozwa na RMO wangu wa Geita kaka yangu Samwel Shoo, wanafanya kazi kubwa sana kutekeleza majukumu yao na kusimamia sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie tu mambo machache. Kwanza niipongeze STAMICO kwa kazi inayofanya nzuri kwa sababu uhalisia Mheshimiwa Waziri wa Madini STAMICO ilikuwa inaelekea kufa, lakini baada ya kuingia wameisimamia wakiwa na Balozi Kamanda Sirro, sasa inasimama inafanya kazi vizuri sana. Mimi niwaombe waende wakaongeze nguvu kwa STAMICO ili iweze kuwasaidia wachimbaji wadogo waweze kufanikiwa zaidi katika utafiti na katika mambo yote ili waweze kufanikiwa kupata mali nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie jambo moja ambalo linaonekana kama lina changamoto kidogo. Mheshimiwa Waziri kuna kitu kinaitwa VAT leaching plant. Jambo hili ambalo leo linatuletea changamoto kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri baada ya bajeti yake akatusaidie basi. Mfano watu wanaotokea Chato wanalipa ushuru na Service Levy, watu wale wenye VAT Leaching, lakini kuna sehemu nyingine hawalipi, kuna sehemu nyingine wanalipa fedha nyingi. Tunaomba basi, kama alivyoweka kwenye madini na akatuwekea wazi kabisa, kwa mfano, kama sisi Geita ametuwekea mpaka na TV, ukienda kupima asilimia zako unaziona, hamna wizi; ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri anafanya vizuri. Maana, kama ameweza kutuwekea uwazi huo, tulikuwa tunapoteza, wakati mwingine unapimiwa tu hovyo hovyo, sasa hivi ukifika unapimiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa VAT Leaching tunaomba basi tuwe na kodi moja. Kama tunalipa shilingi laki tano, yaani nchi nzima tulipe shilingi laki tano, kama vile tunavyolipa royalty 8.7% au 9%. Hii double standard inawaumiza wachimbaji na kuongeza malalamiko makubwa. Ninaamini kwa sababu, Mheshimiwa Waziri ni msikivu, mtendaji na mtu anayeshughulika na mambo mengi, tunaamini atatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazungumza jambo lingine la mwisho. Sisi wachimbaji wadogo ni wavumbuzi, lakini pia, kuna msemo unasema kwamba, ni wavamizi. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, wale waliochukua leseni, kwa ajili ya uchimbaji wao, sisi Watanzania wote hatuwezi kupata leseni kwa pamoja, lakini wengine tuna mitaji kununua mawe tu; baada ya bajeti yake kupita, ninaamini tutampitishia maana tunamwamini, ataenda kufanya na tutaenda vizuri, akatusaidie wachimbaji wetu wadogo wadogo ambao leo wanaondolewa kila maeneo kwa sababu ya wenye leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba, hawa wachimbaji wadogo, wanapokwenda kuvumbua madini, kama mwenye leseni hataki wachimbaji wadogo wafanye kwenye eneo lake, kwenye leseni yake, basi muda mchache waondolewe, ili wasije wakachimba kwa muda mrefu halafu mwisho wa siku wanakuja kuambiwa ondokeni kwenye eneo hili nyie siyo wenye leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli usiopingika ma-RMO wanasimamia sheria na wanafanya vizuri. Wakisema kwamba, jamani hili eneo siyo la kwenu ni la mtu amekata leseni, inatuletea changamoto kwa wachimbaji. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, maana anajua na anafuatilia, basi alibebe hili akalifuatilie. Hawa wachimbaji wadogo wanapoanza kuchimba kwenye leseni zao, watu wanaokuja kuchimba kwenye leseni zao, wale wavumbuzi siyo wavamizi. Mtu mwenye leseni awahi kutuambia kwamba, jamani ondokeni hamtakiwi, lakini akichelewa akatuacha wiki mbili, mwezi mzima, tumeingia na gharama, anakuja kutuambia, inatupa changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, yapo mambo mengi ya kuzungumzia, ninaomba, Mheshimwa Rais juzi amezungumza, hatuwezi kupeleka hela kwenye Mfuko wa Vijana wote. Sisi, Mheshimiwa Waziri wa Madini, kuna vijana ambao hawawezi kufanya kazi ya kilimo, hawezi kufanya kazi nyingine, kazi yao ni madini. Tumemshuhudia juzi akiwasaidia wachimbaji kupata fedha kutoka Benki ya CRDB. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri amefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu na watu wengine wana leseni ikiwezekana atuletee mpango mkakati atakaosimamia wachimbaji wote waweze kupata fedha katika benki ili wachimbaji wetu waweze kuchimba vizuri. Tunaamini kwa sababu ameanza na kwa sababu atapitishiwa bajeti hii, ninaomba tumwombe aendelee kuzungumza na benki zote, siyo CRDB tu, zipo benki nyingine zinazoweza kutusaidia sisi wachimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Kuna jambo ambalo linatupa shida sana, la CSR. Waziri amesimamia vizuri sana, pamoja na kwamba, zipo changamoto kwenye CSR, lakini kazi yake inaonekana, anaifanya, CSR zinatoka japo changamoto zipo. Ninamwomba basi, ikiwezekana Mheshimiwa Waziri ... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge. Muda wako umekwisha.

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi ninamwombea baraka Mheshimiwa Waziri wa Madini. Mungu amsaidie akayatekeleze haya yote. Tunamwamini akayatende kwa uhakika, maana sisi wachimbaji na mimi ni mchimbaji, tunamwamini sana kwamba atatekeleza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kupata nafasi hii kuchangia katika Wizara ya Maji. Mheshimiwa Waziri Aweso, awali ya yote niipongeze sana ofisi kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja anasema, anaweza ukawa simba ukawa peke yako, lakini pia anaweza akawa simba akawa na wenzake wakafanya kazi vizuri. Mheshimiwa Aweso ni simba na ana simba wenzake wanaofanya kazi vizuri, niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, sitasoma sana mafungu na mimi ni msomaji wa mafungu, ataenda asome mwenyewe pamoja na Naibu wake. Watasoma Isaya 44:2, wakiusoma utawasaidia kwa ajili ya manufaa yao. Mheshimiwa Waziri, sisi kule kwetu Katoro, nadhani O-Kundo agomanile, okobhise Katoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametuletea maji yenye gharama kubwa sana, kupitia Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitupatia maji nadhani hata yeye kwenye kampeni alikuja na wale watu wa Katoro tuliwaeleza kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameleta maji ya zaidi ya shilingi bilioni 6.3 pale Mji wa Katoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiwekeza lazima pia ujipange kuvuna ulichokiwekeza, umewekeza mradi mkubwa sana wa maji tunaomba, hoja yetu ni ndogo sana tunatamani watuletee mabomba ili tuweze kusambaza maji katika Mji wa Katoro maana maji yapo. Hadi sasa maji yanapampia kutoka Chankorongo nadhani ukipata muda utatembelea Katoro twende Chankorongo maji yapo yako mengi sana yanayosukumwa kwenye matenki ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, changamoto ukishayapampu unayapeleka wapi? Yanabaki kwenye matenki kwa sababu mabomba ya kusambaza maji ili wananchi wapate maji katika Mji wa Katoro na kata zake bado ni mdogo sana. Kwa hiyo, nimwombe, watu wanasema kushikilia shilingi, mimi sitaki nishikilie shilingi yake ila ninaomba anisaidie kupata mabomba ya kutosha ili watu wa Katoro waweze kusambaziwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ukishayasambaza haya maji wale idara ya maji wana uwezo wa kujiendesha kwa sababu watalipa madawa, watalipa watumishi watafanya, kwa sababu maji yamepata nafasi na maji yamesambazwa na wananchi wetu wamepata maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waziri anapofanya hivyo anatuletea mabomba tukumbuke kwamba ili watu wetu waweze kupata huduma sasa maana siyo watu wote wanalingana kiuchumi, basi watupunguzie gharama za kuwasambazia watu hawa maji kwa sababu wanapokwenda kuwasambazia ikiwa gharama kubwa, watu watakaosambaziwa maji watakuwa ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Waziri baada ya bajeti yake ajitahidi kutuhudumia, awasaidie wananchi wetu waweze kupata huduma ya kutosha ambayo itawasababisha wao kuamini kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipopita katika Mji wa Katoro alitoa ahadi pamoja na kwamba kuna maji yanayokuja yenye mradi mkubwa kutoka Geita, alisema yatakuwepo maji ya kutosha katika Mkoa wa Geita kiujumla.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kabla ya huo Mkoa wa Geita kwa ujumla kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishawekeza katika Jimbo la Katoro, basi ahakikishe anakwenda kusambaza hayo maji ili wananchi hawa waweze kupata huduma nzuri na Waziri tunamwamini na ndiyo maana tunatafuta nafasi sana ya kuzungumza, tumpongeze kwa kazi nzuri uliyoifanya. Miaka tisa yuko ndani ya hii Wizara na ameonekana kuwa simba jasiri anayeweza kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wetu na katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya haya machache, kubwa sana kwangu ninaweza nikazungumza mambo mengi sana, lakini hoja yetu sisi ni moja tu akatusambazie maji ya kutosha maana maji yalishayafika katika Mji wa Katoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, ninaunga mkono hoja, ninamwombea heri Mungu ambariki, achape kazi, asonge mbele pamoja na Mheshimiwa Naibu wake Mheshimiwa Injinia Kundo, wachape kazi, Mama amewaamini kwa moyo wa hali ya juu sana, waende wakapige kazi walete maendeleo kwa wananchi. (Makofi)