Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kija Limbu Ntemi (1 total)

MHE. ENG. KIJA L. NTEMI aliuliza:-

Je, ni nani anayesimamia mikataba ya wenye leseni na wachimbaji wadogo wa madini wanaovumbua madini na mikataba hiyo ni ya muda gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kuwa msaidizi wake kama Naibu Waziri wa Madini, pia wananchi wa Jimbo la Longido kwa mara ya tatu sasa wameendelea kuniamini kuwa mwakilishi wao katika Bunge lako Tukufu, ninaahidi kwamba sitawaangusha wote, siyo Rais wangu wala walionipa ridhaa ya kuwa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Kija Limbu Ntemi, Mbunge wa Katoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kufuatia marekebisho ya Kanuni za Haki Madini za Mwaka 2018 na marekebisho ya mwaka 2025, Kanuni ya 5(a)(1) imeweka sharti la mwenye leseni ndogo ya uchimbaji ijulikanayo kama PML, kuingia mkataba na mchimbaji mdogo atakayefanya shughuli za uchimbaji ndani ya eneo la leseni yake na kuhakikisha mkataba huo unaidhinishwa na kusajiliwa Tume ya Madini.

Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara ya Madini imeandaa rasimu ya mkataba kati ya wamiliki wa leseni na wachimbaji wadogo na kuuwasilisha kwa Maafisa Madini Wakazi wote na watausimamia pindi unaposainiwa na kusajiliwa. Mikataba hiyo itadumu kipindi cha miaka mitatu na huruhusiwa kuhuishwa kwa kipindi kingine kulingana na makubaliano ya wahusika. Ahsante sana.