Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kakulu Burchard Kakulu (2 total)

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyotangulia wenzangu, nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku ya leo tukiwa salama, tukikutana tena kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; moja, kwa ajili ya kuyachakata na kuyachambua maoni ya Mheshimiwa Rais ili tukayatafsiri kwa usahihi mbele ya Watanzania waliotuchagua na kuwaaminisha kwamba bado kuna nafasi kubwa ya kuijenga nchi yetu nzuri iitwayo Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nikupongeze wewe na Mheshimiwa Spika pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuaminiwa katika nafasi mlizoaminiwa kuhudumia nchi yetu. Sambamba, pongezi hizi ziende kwa Mawaziri wetu walioteuliwa kuhudumia katika Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza pia Wabunge wenzangu waliochaguliwa kuhudumu katika Bunge hili. Nitoe shukrani zangu za dhati kwa wananchi wenzangu wa Jimbo la Mbagala walionichagua kwa kura nyingi kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Ahadi yangu kwao ni kuwahudumia kwa uaminifu kwa uzalendo na kwa utii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajielekeza kwa uchache katika maeneo machache. Kwanza katika kutafsiri maoni ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa kupitia hotuba yake kwa Bunge lako Tukufu. Mheshimiwa Rais alichora mchoro wa uhakika katika maono yake kuhusu sekta ya viwanda na sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajielekeza kwenye maeneo hayo, kuonesha kwamba viwanda vyetu ambavyo tunakusudia kuvijenga kupitia kongani zitakazofunguliwa katika kila wilaya na katika kila halmashauri zetu, na namna zitavyoenda kufungamanishwa na sekta yetu ya viwanda ambaye ndiye mlishaji mkubwa sana wa viwanda vyetu na sekta yetu ya usindikaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kilimo chetu bado kinategemea sana kilimo cha mkono na kilimo cha kujikimu. Maono ya Mheshimiwa Rais ni kwenda kukitafsiri na kukipa nyongeza na kukiongezea uwezo kilimo chetu ili kiweze kuhudumia viwanda vyetu kwa uhakika, kituhakikishie usalama wa chakula pamoja na kutupatia mapato kupitia fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza, sekta yetu ya kilimo kwa sasa inachangia pato letu kwa Taifa angalau kwa 26.3%. Lengo ni kuifanya ichangie zaidi kwa sababu ndiyo sekta inayoajiri watu wengi. Mabadiliko kidogo katika sekta hii angalau ikiwa katika asilimia nane mpaka 10% ina uwezo wa kupunguza umaskini kwa zaidi ya nusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukiunganisha sekta yetu ya viwanda na sekta yetu ya kilimo kwa kuzingatia maono ya Mheshimiwa Rais aliyotupa kupitia hotuba yake, tuna uwezo wa kutoa ajira za kutosha kwa vijana wetu ambao ndio tunakusudia kuwahudumia kwa kweli, kwa sababu ndio wanaounda sehemu kubwa ya nchi yetu kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda nichukue nafasi hii kuwaonesha vijana wa nchi hii kwamba bado kuna nafasi ya kuihudumia nchi hii kwa kuitunza na kwa kuitumikia kwa uzalendo. Kilimo chetu pekee tukikifanya vizuri, zile kongani zetu za viwanda katika wilaya zetu 139 na halmashauri zetu 184 tuna uwezo wa kuzalisha ajira za kutosha ambazo zitapunguza presha kubwa iliyopo katika soko la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais, tunaenda kufungua Kongani ya Viwanda ya Kwala. Kongani ya Viwanda ya Kwala peke yake itazalisha ajira zaidi ya 600,000. Kongani ya Buzwagi pekee inaenda kuzalisha zaidi ya ajira 300,000. Kongani ya Bagamoyo inakuja, hebu jaribu kufikiria tutakapofungua kongani katika wilaya zote 139, hali ya ajira na mfumuko wa ajira kwa ajili ya vijana itakuwa ya namna gani? Yote haya, kwa vyovyote vile wanufaika wakubwa ni vijana wenzetu ambao ndio tunakusudia wapate ajira za kutosha katika kongani hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwa speed ya Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka mitano ijayo, matarajio yetu tunakusudia kuyaona mabadiliko makubwa kupitia kongani hizi ambazo zitafunganishwa na sekta yetu ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa wasaidizi wa karibu wa Mheshimiwa Rais kupitia Baraza aliloliteua likiongozwa na Waziri Mkuu, ni kumsaidia Mheshimiwa Rais kuitafsiri barabara ndoto yake hii na maono yake haya ili vijana waweze kupata furaha kwa sababu wanaye Rais ambaye anawaamini, anawategemea na tunawaamini vijana wote kama walinzi na watetezi muhimu wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye jambo lingine muhimu sana hasa katika kipindi cha miaka minne iliyopita ambacho Mheshimiwa Rais wetu ametuhudumia kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa wengi ambao tuna shukrani, kwa kweli Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa, kubwa sana. Kwa mfano, kwenye jimbo langu pekee ninalotoka, katika halmashauri ya Temeke ninayotoka peke yake, zaidi ya shilingi 323,000,000,000 zililetwa katika kipindi cha miaka minne na zimetekeleza na kusababisha mapinduzi makubwa sana katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo ninalotoka peke yake Jimbo la Mbagala vituo vitatu vya afya katika kipindi cha miaka minne peke yake, Hospitali ya Zakhem tunakamilisha kuijenga. Tunaenda kujenga hospitali nyingine kwa ngazi ya wilaya katika kata moja pale Toangoma ya ghorofa sita. Tunaenda kusababisha mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu kama ambavyo tumefanya katika kipindi kilichopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jimbo langu peke yake zaidi ya shilingi 123,000,000,000 zililetwa katika kipindi cha miaka minne. Jimbo moja tu lenye kata sita peke yake, pamoja na kwamba lina wakazi zaidi ya 500,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wenye shukrani kama tulivyo Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, tunao wajibu wa kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpa moyo, aendelee kuhudumia nchi yetu, kwa sababu tunaamaini katika kipindi cha miaka mitano inayokuja, matarajio makubwa ni kuona mapinduzi makubwa kwenye sekta zote kuanzia nishati, miundombinu, kilimo, na ajira kwa vijana. Yote haya lengo ni moja tu, kuhakikisha uchumi wetu unastawi na uweze kuwahudumia wananchi wetu ambao wanaongezeka kwa kasi kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu kwa vijana kama kijana mwenzao, ni kuwaomba wawe wazalendo kwa nchi yetu. Sisi sote tumetembea safari ndefu kufika tulikofika. Mimi miaka 32 iliyopita nilihamia Dar es Salaam nikiwa na miaka karibu 18. Leo hii tunapozungumza nimeaminiwa na Watanzania wenzangu katika eneo la Mbagala na kuwa mwakilishi wao baada ya kukaa hapo kwa miaka 32.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nchi yetu ni nzuri, kila mahali ulipo unayo nafasi ya kuhudumia watu. Nchi yetu hii ni kiasi tu kama kijana kupanga maono yako vizuri, kuwa mtii kwa nchi yako, kupenda nchi yako, kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuwa mtii kwa mamlaka ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache niliyochangia, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi na ninawapongeza Mawaziri wote wawili waliotuwasilishia taarifa zao. Waziri Profesa Kitila Alexander Mkumbo na Waziri wetu wa Fedha wamefanya mawasilisho muhimu na mazuri sana kwa nchi yetu. Sisi kazi yetu ni kuwashauri namna gani ya kuyaboresha na kuhakikisha kwamba, maoni yaliyopo katika mpango wetu yanatekelezwa, kama tunavyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwenye maeneo machache sana, la kwanza ambalo ninataka kuchangia ni hasa katika kugharimia mpango kwa sababu, unaweza ukapanga vizuri, lakini utekelezaji wa mipango hiyo ni kitu kingine. Katikati ya kupanga na kutekeleza ni fedha, bila fedha na rasilimaliwatu, mipango utakuwanayo, lakini matokeo yako kwa sehemu kubwa yatategemea injini inayoitwa pesa. Tunapataje pesa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwenye jambo la kwanza kuhusu maboresho au reforms muhimu katika mashirika yetu ya umma. Katika mpango, Mheshimiwa Waziri ametueleza kwamba, matarajio ya Serikali ni kuona sekta ya umma, kupitia mashirika ya umma, inachangia angalau asilimia nane ya matarajio ya rasilimali ili kugharimia mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu kwa sekta, mashirika ya umma peke yake nchi hii yana assets zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 86.3. Mashirika yenye uwezo mkubwa na mali kubwa kiasi hicho kuchangia kiasi hicho bado ni kidogo. Kwa hiyo, tunahitaji na ninaungana na maono ya Mheshimiwa Waziri ya kufanya maboresho makubwa na more aggressively katika mashirika yetu ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapa mfano, hebu tuangalie uwezekano wa mashirika yetu yote yanayojiendesha kibiashara tualike ushiriki kwa sekta binafsi kwenye mashirika hayo badala ya kuendelea kuyashikilia; ufanisi bado upo chini, tija bado iko chini na faida bado iko chini. Tualike ufanisi wa sekta binafsi kupitia masoko yetu ya mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, moja, tutapata faida ya kuwaalika Watanzania kushiriki moja kwa moja katika kuyaendesha mashirika yao. Pili, tutaialika sekta yetu ya ndani binafsi kushiriki moja kwa moja katika kumiliki mashirika yetu na kuyaendesha, ili kwanza tupate tija. Pili, tuongeze ufanisi, tuongeze faida na tuongeze ajira. Tatu, kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumesaidia kuchangia utekelezaji wa mpango wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninasisitiza Mheshimiwa Waziri atusaidie ku-drive radical and fundamental change katika mashirika yetu ya umma. Ninaamini sana katika ufanisi ulioko katika sekta binafsi. Mashirika yetu ya umma yako yanayofanya kazi vizuri sana kibiashara, lakini naamini yanaweza kufanya mara 10 zaidi, kama tukialika sekta binafsi kushiriki na tukiwaalika wananchi katika kumiliki mashirika yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano mizuri, angalau, ya mashirika makubwa mawili. Kwa mfano, NMB na CRDB miaka 30 iliyopita wakati tunabinafsisha CRDB ilikuwa na hali hoi kabisa taabani, leo quarter ya nne kwa matokeo yao waliyoyatoa juzi CRDB peke yake imepata faida kabla ya kodi shilingi trilioni moja na NMB faida yake kabla kodi ni shilingi trilioni 1.13. Hebu tuangalie miaka 30 tu, kizazi kimoja hapo katikati, lakini kampuni mbili tulizoamua kuzibinafsisha leo zinachangia, moja ni kwa sababu, tuna hisa kidogo kwenye hayo mashirika tunapata gawio na pili tunakusanya kodi pale, 30% inaingia TRA huku tunapata gawio kwa hiyo, tunapata mara mbili. Kwa hiyo, ninasisitiza kabisa tufanye mabadilko makubwa kwenye mashirika yetu, tusiogope. Tuwaalike sekta binafsi washiriki moja kwa moja, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni Serikali inapata stress kubwa sana kutafuta fedha, kukopa na kukusanya kodi, lakini ipo miradi ambayo ina uwezo wa kualika sekta binafsi ikashiriki moja kwa moja kuiendesha. Matumizi ya PPP katika kutafuta fedha za kugharamia mpango ni muhimu, tupunguze uwoga, tuamini watu watapata na sisi tutapata. Watatusaidia sisi kupunguza stress yetu ya kibajeti na watatusaidia kutekeleza hiyo miradi kwa haraka katika muda tunaotarajia. Sisi tutajielekeza kwenye miradi ambayo tunafikiri ni muhimu, lakini haiwezi kuvutia uwekezaji kutoka sekta binafsi kwa hiyo, ni muhimu sana haya mambo kuyazingatia, kama ambavyo ninasisitiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, kuhusu carbon credit, carbon finance au tunaita biashara ya kaboni. Kama Wilaya moja tu ya Tanganyika inaweza kupata shilingi bilioni 20 kwa mwaka, hebu fikiria, tuna misitu ambayo ni karibu 55% ya uso wa ardhi yetu ya nchi nzima. Tukiamua hiyo misitu kuirasimisha, tukaiweka kwenye biashara ya kaboni tuta-generate shilingi ngapi, kwa ajili ya kusaidia kutekeleza mpango wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji mambo matatu tu muhimu; la kwanza ni kuihifadhi misitu yetu, la pili ni ku-certify, tuitafutia thirdy party verification, ikawa certified, tukaanza kukusanya fedha na tatu ni kuhakikisha tunaandaa watu wetu wawe na uwezo wa kuifahamu hii sekta vizuri kwa ku-train watu wetu katika vyuo mahiri kabisa katika eneo hili. Mambo matatu tu, hela zina-flow zenyewe baada ya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ninakusudia kuchangia ni kuhusu namna ya kufanya mapinduzi ya uchumi wa vijijini. A more radical rural economy yetu inahitaji tufanye maamuzi muhimu kuhusu namna tunavyosimamia sekta yetu ya ushirika. Ushirika ninaamini ndiyo nyenzo muhimu sana ya kufanya mapinduzi makubwa sana vijijini sana. Hebu fikiria kwamba, kwa kiwango na idadi ya vyama vya ushirika tulivyonavyo vijijini kila chama cha ushirika kikawa na mashine, angalau kiwanda kidogo cha kuongeza thamani kidogo kwenye mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tutakuwa tumeongeza mazao yetu thamani; pili tutazalisha ajira; na tatu tutachechemua uchumi kwenye eneo lile kwa sababu, vile viwanda vitazalisha shughuli nyingine pale; kama kuna mama ntilie atauza chakula, kama kuna mwingine ana-supply vipuri ataleta pale, amepata pesa. Kwa hiyo, tutaongeza tija kwenye mazao yetu, tutatengeneza ajira vijijini, tutazuia kwa sehemu fulani ile rural urban drift ya vijana wetu wanaotoka vijijini kuja mijini na kwa hiyo, kupunguza pressure ya vijana walioko mjini kutafuta ajira kumbe ajira zinaweza kupatikana vijijini kama tukiamua kufanya maamuzi muhimu ya kubadili sekta yetu vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu sana katika hili ni kuhakikisha ushirika wetu unasimamiwa kwa uadilifu kwa sababu, ubabaishaji ni mwingi sana kwenye vyama vya ushirika wakati mwingine. Kwa hiyo, lazima kusimamia vyama vya ushirika more aggressively hasa kwa kuwekeza katika teknolojia ya namna ya kusimamia vyama vyetu vishiriki vizuri zaidi. Kujenga uwezo wa watu wetu ikibidi kutenganisha ushirika wa mazao na ushirika wa fedha, ili ushirika wa fedha usimamiwe tofauti na ushirika mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nizungumze hayo, lakini kwa kuhitimisha, kama nyongeza kwa wenzangu waliotangulia kuhusu mbegu, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri. Shirika letu la ASA, wakati fulani tuliwahi kupendekeza JKT itusaidie kuzalisha mbegu. Tukitumia nidhamu tuka-exploit nidhamu ya jeshi letu, hasa Shirika letu lile la SUMA-JKT, tunaweza kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu hii tani laki mbili na kitu ni kitu kidogo sana, ni uamuzi tu. Ardhi tunayo, watu tunao, watu wenye bidii wapo, ni uamuzi tu. Tufanye maamuzi ya kulifanya Shirika letu la SUMA JKT tuwape uwezo wa kuzalisha hizo mbegu, ili twende kuchochea kilimo chetu, mbegu ni jambo muhimu, mbegu ni usalama wa nchi. Mtu anaweza akaamua kukusababishia njaa kwa kukuletea mbegu mbovu tu, halafu ukatumia pesa nyingi sana kutafuta chakula, watu wako huko wanakufa, watu hawazalishi wana njaa. Kwa hiyo, ni muhimu hili jambo tulipe kipaumbele, ni jambo muhimu sana kama unataka kusababisha mapinduzi makubwa sana kwenye viwanda na kwenye kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeona niyasema hayo kwa kuhitimisha kwa sababu, ni masuala muhimu. Kama wenzangu walivyosema mwanzoni, kilimo ndiyo nguzo muhimu sana ya mapinduzi ya uchumi wetu. Tukatae, tusikatae, ndiyo eneo ambalo linaajiri watu wetu wengi sana vijijini. Kama tukifanya mabadiliko kidogo kwa kuweka na kufanya mapinduzi ya viwanda vijijini, kwa kuongeza tija kwenye mazao yetu, kilimo chetu kitasaidia kuchangia pato letu la Taifa na kuzalisha ajira nyingi sana kwa vijana wetu na kwa hiyo, tatizo tunalolia nalo la ajira, tutafika mahali itakuwa ni historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Ninamalizia kwa kuwashukuru wananchi wangu wapendwa kabisa wa Jimbo la Mbagala, ninawatakia heri na upendo mwingi sana. Mwenyezi Mungu awabariki sana. Ahsante sana. (Makofi)