Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kakulu Burchard Kakulu (2 total)

MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbagala kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza kwa kutusaidia kujenga ile barabara. Kwa kweli ilikuwa ni changamoto kubwa, ilisababisha msongamano mkubwa na ajali nyingi katika Kilima kile cha Mto Kizinga. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu hayo mazuri, swali moja tu la nyongeza. Ninafahamu na wote tunajua umuhimu wa barabara inayounganisha pale Kongowe kutoka Kongowe kuelekea Kivukoni katika Jimbo la jirani la Kigamboni, na umuhimu wake hasa katika kulisha viwanda vilivyopo Kigamboni katika eneo la Kisarawe II na viwanda vilivyopo katika eneo la Mwandege pamoja na eneo la Mkuranga.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali inaona umuhimu pia wa kupanua hii barabara kutoka Kongowe kwenda Kigamboni ili kusaidia kuhudumia hivi viwanda na shughuli nyingine za wananchi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongezi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, kwa kutambua kazi kubwa ambayo anaifanya na hasa kuondoa changamoto ya msongamano wa barabara kwenye eneo hilo ikiwa ni pamoja na kulijenga hilo daraja la Mzinga ambalo muda siyo mrefu tunaanza kulijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, hii barabara ya Kongowe kwenda Kivukoni ipo kwenye mpango wa kuondoa misongamano (decongestion) ya miji ikiwepo Mji wa Dar es Salaam ikiwepo pamoja na hiyo barabara ya Kongowe – Kivukoni.
MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu linahusiana na Jimbo langu la Mbagala. Ziko kata kadhaa ambazo zilikuwa na miradi ambayo wananchi walianzisha wenyewe na wakati ikiwa mikononi mwa wananchi, imefanya kazi nzuri sana. Baada ya kuchukuliwa na DAWASA kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya Kata ya Kijichi, Kata ya Mbagala na Kata ya Mbagala Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Naibu Waziri atupe hakikisho, je, Serikali iko tayari kuirejesha hiyo miradi kwa wananchi ili tui-manage wenyewe na tuendelee kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nisiwe mwongo, kwa usimamizi wa miradi ya maji na huduma ya maji tunaenda sambamba na maelekezo ya sera yetu. Sera yetu inaturuhusu, kwanza Serikali kusimamia miundombinu na pia, kuhakikisha maji yanatoka na ni salama (secure of water), lakini pia, yawe toshelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, tunapoongelea maji, ni usalama wa Taifa, tunaangalia namna ambavyo tunaweza kushirikisha wananchi kwenye ownership ya kujua mradi ni wa kwao, lakini usimamizi wa mradi bado utabaki katika mamlaka ambayo imetamkwa kwenye sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamtoa hofu, kama kuna jambo na changamoto za usimamizi wa miradi hiyo, sisi tutatuma timu yetu, itaenda kufanya tathmini na kuangalia wapi kuna tatizo ili tuweze kutatua, lakini siyo kurudi kule ambako hatuwezi kufika tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii ina sensitivity yake, kwa hiyo, tukisema kwamba, kwa mujibu wa Sheria yetu Na. 5 ya Mwaka 2019, ambayo ndiyo ilianzisha Wakala wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira, ndiyo yenye jukumu la kisheria la kusimamia na kuendeleza huduma za maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye hili naomba nisiseme uongo kwamba tutawarejeshea wananchi, hilo tutakuwa tunavunja sheria. Kikubwa ni kwamba tutawashirikisha wananchi kwenye kuelewa na kuwa na upana wa kujua nini maana ya miradi ya maji na nani anatakiwa kusimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika naomba kuwasilisha.