MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Kwedikwazu - Sindeni inayopitia Daraja la Komdudu ambayo ipo kwenye Mradi wa World Bank kwa kiwango cha Lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Jacob Sungura, Mbunge wa Jimbo la Handeni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Handeni ni miongoni mwa wilaya zilizo kwenye mpango wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kupitia Programu ya Mradi wa Uibuaji na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi (RISE) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.
MheshimiwaNaibu Spika, Kupitia program hii, barabara ya Sindeni – Kwedikwazu yenye urefu wa kilometa 38 itajengwa kwa kiwango cha lami ikijumuisha ujenzi wa Daraja la Komdudu. Zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi mjenzi imeshakamilika na mkataba wa ujenzi umesainiwa tarehe 24 Aprili, 2026.