MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nipate majibu kwa Naibu Waziri kwamba, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo cha kukusanyia maziwa kilichopo katika Kijiji cha Msomela, Kata ya Misima?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti ninakushukuru sana. Kadri ya upatikanaji wa fedha ndivyo ambavyo Serikali itaendelea na ujenzi wa kituo hiki cha ukusanyaji wa maziwa kilichopo Msomela. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri. Kwa kuwa barabara ya Michungwani - Kwadoya yenye urefu wa kilometa 19 nayo ni sehemu ya utekelezaji wa barabara za awamu ya pili (second road generation) na zabuni barabara hii ishatangazwa, je, ni lini sasa Serikali itatoa barua ya tuzo (letter of award) ili ujenzi wa barabara hii nao uanze kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la pili. Kwa kuwa barabara ya Mkata kwa Sunga yenye kilometa 21 nayo ni miongoni mwa utekelezaji wa barabara za third generation road wa RISE, sasa ni lini Serikali itatangaza zabuni ili ujenzi wa barabara hii nao uanze kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Sungura, Mbunge wa Handeni, kwamba Serikali inatambua muhimu wa barabara hizo na ndiyo maana tayari tumeanza na hii barabara, na tayari zabuni imeshasainiwa, mkataba ushasainiwa tayari kwa kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu na hizo barabara nyingine mbili, moja ambayo Mheshimiwa Mbunge angependa ifanyiwe matangazo na mzabuni apatikane. Nimhakikishie tu kwamba suala hilo tumelichukua, tutalifanyia kazi kwa barabara zote mbili ili tuweze kutangaza zabuni kwa kadri fedha zitakavyopatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizo.