MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Hoja yangu ya msingi ilikuwa ni kwamba hii Barabara ya kutoka Mtama kwenda Newala Vijijini hadi Newala Mjini kama nilivyosema ni barabara kubwa ya uchumi mkubwa na inaunganisha mikoa miwili, Mtwara na Lindi na wilaya zetu. Barabara hii imekuwa ikijengwa kidogo kidogo sana, yaani fedha inatoka kidogo kidogo sana. Ni wakati sasa Serikali iamue kutoa fedha kuimaliza badala ya kuwa inajenga hivi kidogo kidogo na uchumi wetu unaendelea kudorora kwenye eneo hili husika.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, tunatambua umuhimu wa barabara hii. Kama nilivyotangulia kusema, barabara hizi tutazitengea fedha kwenye mipango yetu. Kwenye eneo hili si barabara hiyo tu yenye umuhimu, ipo Barabara ya kutoka Maputi kwenda Ndanda, pia iko Barabara ya kutoka Chiwonga, Pacha Nne hadi Nanganga njia panda ya kwenda Ruangwa. Zote hizi ni barabara tunazozitazama kwa jicho la ukaribu na tutakwenda kuhakikisha kwamba barabara hizi zinafunguka. Ni dhamira ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba uchumi unafunguliwa, barabara zinafunguliwa.