Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MARIRTA G. KIVUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ikiwa ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuchangia katika Bunge lako Tukufu, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kunipa kibali cha kuwa mahali hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kukishukuru chama changu, Chama Cha Mapinduzi, chini ya Mwenyekiti Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniona ninafaa na kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Arusha. Vile vile, ninawashukuru wanawake wa Mkoa wa Arusha kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao, ninawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo katika sekta ya nishati. Kwa pamoja ninapenda kuipongeza Wizara ya Nishati, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Deogratius Ndejembi; ninapenda kumpongeza Naibu Waziri, Salome Makamba na ninapenda kuwapongeza watendaji wote kwa juhudi kubwa ya kuboresha upatikanaji wa umeme na nishati safi nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Arusha tumeshuhudia maendeleo makubwa. Kati ya vitongoji 1,505, vitongoji 945 vimeshapata nishati ya umeme. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hii inafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Arusha, hususan wanawake. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Mtera. Miradi hii ya kimkakati imepunguza changamoto ya kukatika kwa umeme. Sisi wote ni mashahidi, umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara, ukipita unakutana na majenereta yanawaka, lakini sasa hivi changamoto hiyo imepungua. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo, Mkoa wa Arusha bado una changamoto. Takriban vitongoji 400 havijafikiwa na huduma ya umeme na tukizingatia Mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii, mjini na vijijini. Ninaishauri Serikali kuharakisha kupeleka umeme katika vitongoji vilivyobakia kusudi maendeleo ya kiuchumi yaweze kuendelea kwa wananchi wa Arusha hususan wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)