Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, kabla sijaanza kuchangia naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunistahilisha, kunirudisha kwenye Bunge hili kwa awamu ya tatu na bado ninaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu wa mwaka 2025/2050 tunahitaji mawazo tulivu ili uweze kutekelezeka. Mipango mingi duniani huandaliwa, hutekelezwa kwa sababu viongozi wenyewe wanakubali mpango huo utekelezeke. Tunaweza tukaandika sana kama huko mbele na viongozi wengine hawajaamua itakuwa ni historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na kilimo, miaka 10 tumeimba kilimo ni hatua ndogo sana iliyoguswa kwenye umwagiliaji, hivi tuna tatizo gani mabonde ambayo yamefanyiwa usanifu yakiweko na ya Magu. Tukikopa fedha tukawekeza tukaanza kutoza wakulima kile walichokipata kwenye uzalishaji tukalipa hayo madeni tuna tatizo gani Watanzania. Nchi zote zilizofanikiwa hazijasubiri cash bajeti kwamba tukusanye ndipo tutekeleze nchi zote duniani zilizofanikiwa zilikopa zikatekeleza mpango zikaanza kulipa. Lazima maendeleo utangulie kwanza halafu uanze kuchukua fedha kutokana na kile ambacho umekiwekeza kulipa hilo deni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niombe, hebu nchi iamue kama deni ni himilivu kama deni lina nafasi, tukope tuwekeze kwenye umwagiliaji ili uchumi jumuishi uweze kupatikana. Mfano tu tunayo mabonde mazuri, lakini kila wananchi wanapolima hali ya hewa ikibadilika hawaivishi, anatupa gharama ya mbegu, anatupa gharama ya vibarua, lakini anaambulia hewa. Atafika kwenye kipato cha dola milioni saba, lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bunge lazima tuamue na tuweke maazimio kwenye mpango huu ili tuupime vizuri mpango huu kwa sababu tukikusanya mapato yetu ya ndani, hatutaweza kufikia malengo. Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia waandike historia ya Mpango huu kwa kukubali kukopa ili tuwekeze kwenye umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu mbegu; nchi zote duniani zina mbegu zake mbegu hizi tulizonazo lazima tuzitazame zinatupeleka. Je, zinavumilia magonjwa mfano tu mbegu ya pamba leo imelimwa miaka 12, mwananchi anapulizia zaidi ya mara 15 na mapato hayapati utamshawishije kwenda kulima pamba ambayo kwa eka anapata kilo 200, hazalishi kwa tija? Tutafikiaje lengo la kuzalisha kilo milioni moja bila kuwekeza kwenye mbegu, turudi maabara, sayansi ifanye kazi ili tuweze kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kwenye suala hilo la mbegu na namna ya kuwekeza viwanda vya nguo, niombe, Mheshimiwa Babalevo amezungumza hapa sisi Tanzania kama hatutazuia kuingiza mali iliyokamilika kutoka nje, hatuwezi kuwaondoa Watanzania kwenye umaskini. Mazao ya kimkakati yale matano ambayo mojawapo amegusa la mchikichi ukiwa unatoka Congo kupita Rwanda kuja Burundi, Burundi imepiga hatua kwa zao la mchikichi, Burundi inakwenda kutuacha sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaagiza mafuta yote kutoka nje, unafikiri mkulima wa alizeti ambapo Mheshimiwa Naibu spika anatoka kule Babati atauza alizeti kwa bei ya juu? Unafikiri mkulima wa pamba atauza pamba yake kwa bei ya juu? Kwa sababu mbegu zake hizo zina mafuta ya kutosha. Sasa hebu tuweke miaka mitano tumwambie MO ndani ya miaka mitano hutaagiza mafuta, tumwambie Bakeresa ndani ya miaka mitano hutaagiza ngano. Ngano yote ilimwe hapa ili iweze kupunguza fedha za kigeni kwenda nje…
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, Taarifa.
TAARIFA
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpa taarifa mzungumzaji, anayemzungumzia anaitwa Bakhresa siyo Bakeresa. (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga, unaipokea hiyo Taarifa?
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majina yanaweza kuwa hayo hayo mengine ya Kigiriki, mengine ya Kisukuma ni hayo hayo, ninapokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambayo imejitawala miaka 60 lazima tuweke muda. Bakhresa huyo huyo tumempa shamba la kulima miwa kule Bagamoyo anafanya vizuri tunaamini ndani ya miaka mitano hatutakuwa tena na vibali vya kuagiza sukari. Bakhresa huyo huyo tukimpa kulima ngano kule Njombe au Arusha hataagiza ngano atakuwa mkulima mkubwa na atajenga viwanda na tutapunguza fedha za kigeni kwenda nje, tutauza nje ili kuleta fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo gani waandika Mpango kuamua jambo hili? Nchi iliyojitawala miaka 60; kama tunakuja humu kufurahisha tu kwamba nimeongea kama kilabu hatuna maana ya kuwa Wabunge wa namna hiyo. Tumestahilishwa na Watanzania kuja hapa ili tuweze kuwasaidia na Watanzania wapige hatua. Kwa hiyo, niombe Bunge hili pamoja na Mpango ndani ya miaka mitano vitu ambavyo vinaweza kulimwa hapa na vikapatikana viwe marufuku vilimwe hapa ili tuweze kuzalisha hapahapa, niombe sana hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi kuna vikwazo vingi vya uwekezaji. Nilikuwa ninawasikiliza Wabunge, Mbunge wa Mbeya alizungumza sana jana kuhusu viwanda vya nguo. Pamba tunayolima hapa Tanzania inahitaji fedha dola milioni 300 ili kujenga viwanda angalau vitatu vya kuchakata pamba yetu hapa. Tumezungumza miaka mingi lakini incentive zetu tulizonazo zinaweza kusaidia mipango mikubwa hii. Mfano tunapozungumza dola milioni 300, VAT 18% ni zaidi ya dola milioni 54. Je, kuna Benki kwanza hapa Tanzania ambayo inaweza kukopesha dola milioni 300, ni ndoto ya Alinacha. Kwa hiyo, lazima utashi wa Serikali yenyewe iweze kuamua ili viwanda hivi vijengwe na kwenye incentive VAT iondolewe kwenye uwekezaji mkubwa kama huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tatizo letu tulilonalo tunaangalia tu kodi ya msingi halafu unasema hii itakuwa refund. Sasa wewe unakopa dola milioni 54 za kulipa VAT unaanza kuchajiwa riba halafu refund yake hata ikija unapewa ileile ni sawasawa? Kwa sababu hizo dola ninazozungumzia za VAT ni uwekezaji mwingine wa kiwanda kingine mbona hawatuelewi tuko kwenye industry hii sisi. Mimi ni mwekezaji wa ndani ambaye hata nikipata faida siwezi kwenda kujenga Canada. Tuangalie miradi ya wawekezaji wazawa, tuipe kipaumbele, VAT ni nini? Huyu mwekezaji akianza production anaanza kulipa VAT. Kwa nini tunang'ang'ania kodi? Kwa nini tunang'ang’ania Sera za Kijerumani, sera za ki-Europe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwamba sisi ambao tuko kwenye industry hii tunakutana na mambo mengi ambayo ni vikwazo kwa kuendeleza hii Dira ya Mwaka 2025 -Mwaka 2050. Kama hatutaondoa vikwazo tukaweka vitu chochezi vya uwekezaji tutaimba, watakuja na wengine, nchi hii ni yetu tungepata historia tulioko hapa kwamba tumebadilisha sera na sheria zikaendana na Dira hii …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunafanya nini? Ninaunga mkono hoja, lakini tusikilizwe hatuna sababu ya kuwa Waheshimiwa Wabunge kama hatusikilizwi. Ahsante sana.