Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZULFA MMAKA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia leo hii katika Wizara hii. Kwanza, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha uhai na uzima ili kuweza kuungana na wananchi katika majukumu yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mambo mazuri, makubwa na yenye mwonekano kwa kipindi kifupi tu ambacho kaingia madarakani. Katika mambo hayo ambayo leo hii tunayoiona, Mheshimiwa Rais wetu wa Tanzania wakati analihutubia Bunge hili alitoa ahadi nyingi ikiwemo uanzishwaji wa Wizara hii. Wizara hii imeanzishwa, inafanya kazi na pia ameruzuku fedha nyingi kwa ajili ya kuwasaidia vijana katika kujikwamua na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika sera na mipango ya Wizara hii. Lazima tubadilike kutoka kuwa ya kiutawala na kwenda kuwa ya matokeo yanayoonekana. Ninaomba nichangie kuhusu mitaji. Tatizo la vijana siyo ukosefu wa ubunifu, bali ni ukosefu wa upatikanaji wa sera, mitaji nafuu na upatikanaji wa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko ya uwezeshaji ambayo tukonayo sasa hivi vijana, ni mifuko ambayo ina masharti magumu, na utaratibu mrefu wa kuipata. Suala hilo linachangia vijana kutokupata mikopo hii kwa ajili ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara basi ije na mfumo wa mikopo midogo (micro finance) ili tuweze kupata mikopo hiyo yenye riba nafuu, dhamana mbadala na ufuatiliaji wa karibu. Aidha, kuwe kuna blended finance model ambayo Serikali itachukua sehemu hatarishi ili kuvutia taasisi binafsi kuweza kuwavutia vijana kuliko kuachia vijana kujiingiza katika mikopo chechefu kama vile kausha damu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujuzi na vitendo ni muhimu kwa vijana wetu. Ni lazima tubadili mtazamo, siyo kila kijana anaweza kuajiriwa Serikalini. Basi, tunahitaji mapinduzi ya kweli katika mafunzo ya ufundi, ujenzi, kilimo cha kisasa, uchakataji wa mazao, TEHAMA na huduma za kidijiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapendekeza kuanzishwa kwa vituo vya ubunifu katika kila mkoa vitakavyoweza kuunganisha mafunzo ya teknolojia na masoko ya bidhaa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwajibikaji wa Wizara bila viashiria mahsusi vya kupima mafanikio tutabakia tu na kauli nzuri bila mafanikio ambayo yanaonekana. Ninaiomba Wizara, basi iweke wazi takwimu za kila mwaka kuhusu idadi ya ajira mpya za vijana zilizotolewa, biashara mpya zilizoanzishwa, ongezeko la kipato kwa walengwa hizi, ziwe ni KPI rasmi zinazokaguliwa na Bunge letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusisitiza kwamba mapambano dhidi ya umaskini wa vijana siyo suala la sera pekee, ni suala la dharura la Kitaifa. Kushindwa kuwawezesha vijana leo hii tunajenga mzigo wa kesho. Hivyo basi, ninaiomba Wizara hii ije na mkakati mahsusi utakaotekelezeka na unaopimika kimikakati utakaowatoa vijana kutoka kwenye umaskini na kujiingiza kwenye uzalishaji wenye tija na unaonekana katika jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tutambue kwamba vijana siyo viongozi wa kesho peke yake, bali ni nguvu kazi ya sasa. Unapomkosesha kijana ajira, siyo kwamba unamkosesha kipato peke yake, bali unamkosesha matumaini ya maisha yake ya baadaye na ya sasa, hadhi yake katika jamii, na imani yake katika mfumo mzima wa maisha. Jambo hili ni hatari sana katika jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa ajira unaweza kusababisha na kuchochea ongezeko la vitendo vibaya vya rushwa, uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu. Pia, ninaiomba sana Serikali hii inapokuja katika suala la mikopo, tuangalie mikopo hii wanaonufaika ni kweli wale wahusika? Au wanaonufaika ni wale ambao wana ukarimu wa karibu na wale watoaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wana imani sana na Serikali yetu hii ya Mama Samia. Tunafahamu kwamba Mama Samia ana imani kubwa sana juu ya sisi vijana na tunaona kwamba hata katika Bunge hili, kuna mifano ya kutosha. Wabunge wengi ambao walipitishwa na Chama chetu cha Mapinduzi ni vijana na pia katika uteuzi wa nafasi zake tunaona nafasi nyingi vijana wameteuliwa na wameaminiwa katika nafasi kubwa kubwa ili sasa kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumwombe sana Mama Samia, sisi vijana tunampenda, tunamjali na tunamwomba Mwenyezi Mungu azidi kumzidishia nguvu, hekima na busara katika kuiongoza nchi hii. Sisi Vijana wa Tanzania tuko bega kwa bega na Mheshimiwa Rais, kuna msemo unasema, “Hakuna kama Mama.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunadhihirisha moja kwa moja kwa matendo anayoyafanya Mheshimiwa Mama Samia. Anayafanya kama Rais, lakini ni kama mama kwa watoto wake, katika nchi yake. Rais wetu wa Tanzania ameamua kuja na mageuzi makubwa kwa vijana, na sisi tunayaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana vijana wenzangu walioko mitaani, wamwamini Mheshimiwa Rais kwamba anaweza na ana imani kubwa juu yetu, tusishawishike, na tusiingikie katika makundi mabaya ya kuaminishwa kwamba nchi yetu haitutambui ama haitupendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upotoshaji unaofanyika huko katika mitandao; niwaombe sana vijana wenzangu tujikite katika kufanya kazi, tujikite katika masuala mazima ya kiupendo na imani na nchi yetu kumuunga mkono Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye anatuonesha imani kubwa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)