Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Lazaro Killiani Komba (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi. Nami kwa kuwa ni mara ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenifikisha katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea nafasi ya Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi na hatimaye wananchi wa Jimbo la Peramiho kunichagua na kuwa mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo, wakiwemo wananchi wa Jimbo la Peramiho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kazi kubwa anayoifanya, kazi ya kuwatembelea Watanzania kule kwenye mikoa, kuwasilikiliza na kutatua changamoto zao pale inapobidi afanye hivyo. Kazi hii kwa hakika siyo nyepesi, ni kazi ngumu na inayohitaji kujitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivi, Mheshimiwa Waziri Mkuu anaendelea kuimarisha imani ya Watanzania dhidi ya Serikali yao, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais mbeba maono, Rais mpenda maendeleo, Rais mpenda haki, na zaidi Rais mpenda Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza pia Mkuu wetu wa Mkoa, Mheshimiwa Kanali Ahmed Abbas Ahmed kwa kazi nzuri anayoifanya akiwa anashirikiana na viongozi wenzake, wasaidizi wake, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Wilman Kapenjama Ndile, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea Vijijini dada yangu Elizabeth Gumbo, pia na Mwenyekiti wake wa Halmashauri, Mheshimiwa Ponera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze katika kuchangia Hotoba ya Waziri Mkuu ya Bajeti, na kama muda utaniruhusu nitakwenda katika maeneo matano. Eneo la kwanza nitazungumza kuhusu barabara, eneo la pili nitazungumza kuhusu afya, na eneo la tatu nitazungumza kuhusu elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la barabara. Sisi wananchi wa Jimbo la Peramiho, sehemu kubwa ya maisha yetu yanategemea kilimo. Niseme tu, ili kilimo kiweze kuimarika ni lazima tuwe na barabara ambazo zinapitika wakati wote wa mwaka. Ikifika nyakati za Novemba, Disemba na Januari sisi tunatumia barabara kwa ajili ya kupeleka pembejeo, zikiwemo mbolea, katika mashamba yetu. Ukifika wakati wa mavuno pia tunatumia barabara kwa ajili ya kurudisha mazao kutoka mashambani kupeleka sokoni na baadaye kupeleka katika maeneo mengine ya kuhifadhia mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya barabara katika Jimbo la Peramiho kwa hakika siyo njema sana. Ubovu wa barabara umezungumzwa na Wabunge takribani zaidi ya 90%. Takribani kila Mbunge aliyesimama amezungumza, na jambo hili pia liko katika Jimbo letu la Peramiho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara ya kutoka Njiapanda ya Likuyufusi – Mpitimbi – Mkenda ambako ni mpaka kati ya Taifa letu hili la Tanzania na majirani zetu wale wa Msumbiji. barabara hii ina kilometa 120. Barabara hii imezungumzwa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa miaka mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pamoja na kuzungumzwa kwa miaka mingi, utekelezaji wake kwa hakika umekuwa wa kusuasua kwa muda mrefu. Hii barabara ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya Taifa hili na pia maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Peramiho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa barabara hii ina mchango wa kusafirisha bidhaa zinazoshuka katika Bandari ya Mtwara na kuelekea kaskazini ya Msumbiji. Gari zinapita katika barabara hii ya Likuyufusi – Mpitimbi – Mkenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, barabara hii tarehe 10 Juni, 2025 mkandarasi alipata nafasi ya kusaini mkataba ili kuweza kuanza ujenzi wa barabara hii, lakini hivi ninavyozungumza, ni takribani mwaka mmoja, mkandarasi hayuko site kwa sababu hajapata fedha za kuanza ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali itusaidie sisi wananchi wa Jimbo la Peramiho, barabara ile ijengwe kwa kiwango cha lami ili nia ya Serikali ya kuhakikisha eneo lile linaendelea kuimarisha uchumi wake liweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi ni nyingi, ningeweza kuzitaja zote, lakini niseme tu, iko barabara ya Njia Panda ya Ndongosi kwenda Ndongosi hadi Nambendo; Barabara ya kutoka Ndongosi kwenda Mpingi hadi Kikunja; Barabara ya kutoka Magagura kwenda Mipeta; Barabara ya Magagura kwenda Ngahokora; Barabara ya Kutoka Peramiho kupita Maposeni kwenda Kilagano ile ya kutoka Kilagano kwenda Mwepai. Barabara hizi ni nyingi na hali yake siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu pia kuitaja barabara ile ya kutoka Songea kwenda Mpingi, barabara hii hazipitiki. Ninaomba sana, pamoja na ongezeko hili la bajeti ya TARURA ya shilingi trilioni 1.2, bado kwa mahitaji ninayoyasikia katika Bunge hili, hatutafanikiwa kuweza kuzijenga barabara hizi kwa kiwango kinachotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kupata matokeo ambayo hatujawahi kuyapata katika ujenzi wa barabara, tunapaswa kuja na mawazo ambayo hatukuwahi kuwa nayo huko nyuma kuhusu namna ya kupata fedha za ujenzi wa barabara zetu katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa ni jambo jema na la busara sana Serikali ikatumia mbinu ile ile iliyotumika katika kuweka umeme vijijini kwa maana ya REA, njia ile ile iweze kutumika kupata fedha za kwenda kujenga miradi ya barabara ili mwisho wa siku barabara zetu ziweze kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya hivi, katika kipindi hiki cha miaka mitano, ni imani yangu hata zile ambazo zinapitika leo, ikifika miaka mitano ijayo hazitakuwa na nafasi ya kupitika sawa sawa, na hivyo tutapeleka mzigo mkubwa kwa Serikali jambo ambalo tungeweza kupunguza mzigo huo kwa kutafuta fedha kwa wakati mmoja ili ziweze kuimarisha barabara katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika eneo la afya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa bahati mbaya muda wako umeisha…

MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana… (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi, lakini nitumie pia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia zawadi hii ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuimarisha sekta hii ya kilimo. Kazi hii si ndogo na pongezi hizi ninazozitoa nitazitoa kwa takwimu ili tujue kabisa kwamba kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais inaonekana pia katika maisha ya kawaida na vilevile iko vizuri katika takwimu tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu ambaye sisi tunaomfahamu tunamfahamu kwa ufanisi wake mkubwa katika kazi anazozifanya na hajawahi kushindwa mahali popote alipopata kufanya kazi. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri, wananchi wa jimbo la Peramiho huwa wanaamini sasa shamba limepata mkulima, kwa hiyo mazao lazima yaongezeke kupitia Mheshimiwa Waziri na timu yake yote akisaidiana na Naibu Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Silinde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa pongezi hizi nikiwa nina takwimu zinazopelekea tutoe pongezi hizi. Tutakumbuka Mwaka wa Fedha 2021/2022 uzalishaji wa mahindi katika nchi hii ulikuwa ni tani 6,950,000, wakati mahitaji ya chakula ndani ya nchi ilikuwa ni tani milioni 5,900,000, na hivyo tukawa na ziada ya tani 950,000, ziko pembeni. Miaka michache baadaye, ni miaka miwili tu baadaye uzalishaji uliongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka tani milioni sita mpaka kufika tani milioni 10,925,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo matumizi yetu pia yalikuwa yameongezeka kwa sababu ya ongezeko pia la idadi ya watu. Tukawa tunahitaji kutumia ndani ya nchi tani 7,300,000. Hivyo kupelekea kuwa na ziada ya chakula kwa takribani tani 3,600,000. Hizi zipo zinahitaji kutoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu hizi hazijaja kwa bahati mbaya. Takwimu hizi zimekuja kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Kilimo kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amepanga kuimarisha na kukuza sekta ya kilimo ambayo kimsingi inaajiri kwa kiwango kikubwa katika nchi hii ukilinganisha na sekta nyingine tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja; ongezeko hili limesababishwa na ongezeko la pembejeo zile za ruzuku; kwa maana ya mbolea, mbegu, pamoja na madawa. Mwaka wa Fedha 2021/2022 tulikuwa tuna uwezo wa kununua mbolea tani 7,241, lakini miaka miwili, mitatu baadaye ongezeko limekuwa kubwa sana. Tunapata sasa mbolea ya ruzuku kwa tani 21,457 kwa mwaka mmoja. Ongezeko hili ukilitazama ni mara tatu ndani ya kipindi cha miaka miwili. Si jambo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, maendeleo yoyote yana tabia ya kuzalisha matatizo. Tumeongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa lakini uzalishaji huu umezalisha tatizo la upatikanaji wa masoko. Sisi wakulima wa mahindi wa Jimbo la Peramiho soko letu kubwa lenye uhakika ni NFRA; na NFRA ukiitazama imekuwa inaongeza kiwango cha kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 ilikuwa imenunua tani takribani 58,000, lakini hivi tunavyozungumza kwa msimu uliopita NFRA wameongeza na wakanunua tani 457,000. Ongezeko ni kubwa, lakini ongezeko hili haliendani na ongezeko la uzalishaji wa mahindi na hivyo kutengeneza uhaba wa soko kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuishauri Serikali katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, niishauri Serikali, juhudi kubwa inayofanya katika kuhakikisha sekta ya kilimo inaimarika na kuongeza uzalishaji, juhudi ile ile itumike katika kutafuta masoko ya nje kwa sababu ndani tayari pamekwishajaa na hatuwezi kuuziana wenyewe kwa wenyewe wakati wote tunazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili kwa Serikali; ukitazama katika takwimu nilizozitoa tuna akiba ya tani 3,600,000. Ukitoa ile inayonunuliwa na NFRA ambayo ni tani 445,000 na ile inayouzwa nje ya nchi, kwa maana ya mahindi kutoka nje ya tani 665,000, bado tunabaki ndani ya nchi na akiba ambayo haijakwenda kokote ya tani 2,500,000, ambazo kimsingi hizi ziko katika maeneo mawili. Either ziko kwa wananchi na zimeshindwa kufika sokoni au zimeharibika kwa sababu wamekosa maghala ya kuhifadhia mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu wa tatu kwa Serikali, tuiombe sana Serikali. Sisi wananchi wa Jimbo la Peramiho tunazalisha kwa kiwango kikubwa mahindi; na kwa sababu tunashindwa kuyauza yote kwa wakati, yale yanayobaki tunaomba sana tujengewe maghala katika maeneo manne nitakayoyataja. Tunaomba kujengewa ghala katika Kata za Ndongosi, Kata ya Mbinga Mhalule, Kata ya Magagula na Kata ya Kilagano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi tutakuwa tumesaidia sana maeneo mawili. Jambo la kwanza tutaimarisha uzalishaji na jambo la pili tutashawishi vijana ambao wanapaswa kuingia katika sekta hii kama sehemu ya maisha yao kuwa na fursa na kuona kilimo ni sehemu ya biashara na kwamba biashara hii inakwenda kuimarisha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaona nitumie nafasi hii kutoa ushauri katika maeneo haya. Nikushukuru sana kwa nafasi. Niendelee pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya na sisi wananchi wa Jimbo la Peramiho tuna imani sana na Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Maji. Ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uhai na afya njema aliyonipatia iliyoniwezesha kupata kibali cha kusimama hapa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Peraminho, ambao kimsingi wamenituma nije nizungumze habari ya maji katika vijiji vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi cha Watanzania, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Jimbo la Peramiho. Miaka mitano iliyopita sisi wananchi wa Jimbo la Peraminho tulikuwa tunapata maji kwa 67.7%, lakini leo tunavyozungumza mpaka sasa tumefika 79.3%. Haya ni mafanikio makubwa na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Peramiho wana utamaduni wa kushukuru, lakini huwa wanaamini kushukuru ni kuomba tena. Sisi tunaomba tena katika maeneo matatu; eneo la kwanza, tunaomba miradi ile ambayo tayari ilikuwa imepatiwa fedha zaidi ya shilingi 4,451,000,000 ilianza utekelezaji na iko katika vijiji sita, lakini imesimama kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali na kwa bahati nzuri ndugu yangu Mheshimiwa Waziri yuko hapa ananisikia. Miradi iliyoko katika Kijiji cha Mpandangindo, Kijiji cha Makwaya, Kijiji cha Maleta, Kijiji cha Liweta na Kijiji cha Mdunduwaro, maeneo haya yamekuwa na changamoto kwa muda mrefu, lakini ipo miradi ambayo utekelezaji wake ulikuwa umesogeasogea kwa kiwango kikubwa, ukiwemo wa Kijiji cha Kitulo. Ninaomba sana, Mheshimiwa Waziri, Serikali iweze kutupatia katika bajeti hii fedha iliyobaki, ili kukamilisha, maji yaliyo safi na salama yaweze kupatikana kwa wananchi takribani 17,565 katika vijiji hivi sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vijiji viwili vilivyokuwa na miradi ya maji. Miradi ile chakavu kwa sababu, vijiji hivi vipo tangu mwaka 1960 na miradi hii ilikuwepo tangu wakati huo, kabla hatujapata uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiko Kijiji cha Mpitimbi A na kiko Kijiji cha Magazini. Vijiji hivi idadi ya watu imeongezeka, imekuwa kubwa sana. Ninaomba sana sasa Wizara yetu ya Maji itusaidie kufanya ukarabati katika maeneo haya ili wananchi hawa waweze kupata maji yaliyo safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu ninakushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)