Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Lazaro Killiani Komba (2 total)

MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza katika eneo hili la maji. Kwanza niishukuru Serikali, inafanya kazi kubwa katika sekta hii hasa katika Jimbo la Peramiho, lakini tuna vijiji sita mpaka sasa hakuna huduma ya maji. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hii ya maji katika vijiji hivi sita ambavyo vimebaki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba tunavyo vijiji takribani 1,575 ambavyo havijapata miundombinu rasmi ya utoaji wa huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, tunao mpango mkakati ndani ya kipindi cha miaka mitano tutahakikisha kwamba na Serikali imejipanga, awamu kwa awamu tutaenda kuhakikisha kwamba vijiji vyote 1,575 vinapata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia bajeti hii katika vijiji hivyo sita, baadhi ya vijiji, ninaomba tukitoka hapa Mheshimiwa Mbunge tukutane ili angalau baadhi ya vijiji tuviingize kwenye bajeti tuanze hatua moja wapo ya kutatua changamoto ya maji katika vijiji hivyo sita vya Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze sana kwa kuchaguliwa, ahsante sana.
MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nipate kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Peramiho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Songea Mjini kupitia Liwena, Kijiji cha Lipaya hadi kufika Mpitimbi ambapo inaunganika na barabara ile ya Likuyufusi - Mkenda ni barabara ya miaka mingi sana, na barabara hii haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu na sasa tunavyozungumza daraja linalounganisha vijiji hivi limekwishaanza kukatika.

Je, ni lini sasa Serikali itaijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Komba, Mbunge wa Jimbo la Peramiho kwa ufuatiliaji wake wa mara kwa mara na nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Peramiho kwamba kipaumbele cha Serikali kwenye miradi ya barabara ni kuhakikisha maeneo yote korofi yanajengwa ili wananchi waweze kusafiri na kusafirisha bidhaa zao bila kikwazo vyovyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nitumie nafasi hii nimwelekeze Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea wafike kwenye barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja kutoka Songea kwenda maeneo mengine ili waifanyie tathmini. Kwanza, wajiridhishe na hali ya daraja hilo kama linaweza likafanyiwa matengenezo kabla halijaharibika, tuweze kufanya matengenezo ya dharura ili daraja hilo lisikatike, lakini tuone gharama zinazohitajika kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo ambayo haijatengenezwa muda mrefu ili Serikali iweze kutenga bajeti kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo.