MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mfumo madhubuti wa kupima matokeo ya mikopo 10% ya Halmashauri ili kubaini changamoto na mafanikio?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Neema Peter Majule, Mbunge wa Mkoa mzima wa Dodoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kanuni za 31, 32 na 36 za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2024 zinaelekeza na kuweka utaratibu wa kufanyika kwa tathmini ya utoaji na usimamizi wa mikopo kila mwaka katika ngazi ya Halmashauri Mkoa na Taifa. Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI imekwishafanya tathmini mara moja tangu kuanza kwa mfumo mpya wa utoaji mikopo. Pia tathmini imekuwa ikifanyika kulingana na changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa utekelezaji. Tathmini hizi ndizo zinazowezesha kufanya maboresho mbalimbali mifumo inayotumika.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Januari, 2026, jumla ya vikundi 24,064 vimepata mikopo, ambapo vikundi vya wanawake ni 13,639, vijana ni 8,140 na watu wenye ulemavu ni 2,285. Serikali pia imejenga uwezo kwa wasimamizi 736 wa Halmashauri na 78 wa Mikoa kuhusu usimamizi wa Mfumo wa WEZESHA na inaendelea kuufanyia maboresho Mfumo wa Wezesha ili kuongeza ufanisi na tija ya mikopo kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza: -
Je, Serikali imeweka vivutio gani vya uwekezaji kwa Wazawa ili kuwahamasisha kuwekeza zaidi nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Neema Peter Majule, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Namba Sita ya Mwaka 2025, Serikali imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji wazawa na wageni wenye leseni ya vivutio (Certificate of Incentives). Wawekezaji hao wamegawanywa katika makundi mawili: wa kawaida na mahiri, kulingana na aina na kiwango cha mtaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wawekezaji wa kawaida, kiwango cha chini cha mtaji kwa wazawa ni dola 50,000 na kwa wageni dola 500,000. Kwa wawekezaji mahiri, kiwango cha chini ni dola milioni 20 kwa wazawa na dola milioni 50 kwa wageni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipunguza pia kiwango cha chini cha mtaji kwa wazawa kutoka dola 100,000 hadi 50,000, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wazawa na kupunguza vikwazo vya kuingia kwenye sekta rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji hunufaika na urahisishaji wa huduma kupitia kituo cha pamoja, upatikanaji wa ardhi, na miundombinu kama umeme, maji na barabara. Pia hupata vivutio vya kikodi kama punguzo au msamaha wa kodi kwa mitambo na vifaa vya uzalishaji, pamoja na ulinzi wa uwekezaji kwa mujibu wa sheria na mikataba ya Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mikubwa hupata vivutio maalum kupitia Kamati ya Kitaifa ya Uwekezaji (National Investment Steering Committee - NISC) ambayo ipo chini ya Waziri Mkuu, ikiwemo makubaliano ya kikodi na huduma za haraka za vibali.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatoa vivutio vya ziada kwa wazawa, ikiwemo kipaumbele cha ardhi nafuu, fursa za mikopo na programu za kuwezesha biashara ndogo na za kati. Wazawa pia huhamasishwa kuingia ubia na wawekezaji wa kigeni na kunufaika na sera za local content.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mshauri Gatsby Africa, Serikali inaandaa mwongozo wa Kitaifa wa vivutio vya uwekezaji ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushindani wa wawekezaji wazawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.