Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Neema Peter Majule (7 total)

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri kijana kabisa. Nina maswali ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kutambua umuhimu wa sekta ya fedha, Serikali imeandaa au kusimamia miongozo ipi ya kuhakikisha wananchi hususan wanawake na vijana wanapata elimu ya fedha ili kuchochea jitihada za ukuaji wa kiuchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imechukua gani sasa kwa hao watu ambao wamejinufaisha sana kwa mikopo hii yenye riba kubwa? Waingereza wanasema Predatory Loans, lakini sisi tumeitafsiri kama ‘Mikopo ya Kausha Damu’. Kwa maana kwa namna walivyofanya wameweza kabisa wenyewe kujinufaisha na kupunguza kabisa jitihada ya Serikali ya kuwakwamua wananchi kiuchumi hususan wanawake na vijana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Neema Peter. Kwanza ninakushukuru kwa maswali mawili ya nyongeza, maswali mazuri, lakini hii inamaanisha kwamba wanawake wa Dodoma hawakukosea kukuchagua. Kweli Ph.D kichwani ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo sasa, niseme tu kwamba, Serikali imeendelea kuandaa na kusimamia miongozo na utekelezaji wa sekta ya fedha ili kuchochea uchumi wa wananchi, hasa vijana pamoja na wanawake. Serikali imekuja na mkakati maalum ambao unaitwa Programu ya Elimu ya fedha ya mwaka 2020/2021 – 2025/2026, ikiwa ni mpango maalum wa kutoa elimu kwa wananchi (wanawake wanaume na makundi mengine) ambayo inalenga zaidi kuwawezesha Watanzania kupata uelewa, maarifa na kuwajengea kujiamini katika kusimamia mapato na matumizi na kufanya maamuzi sahihi katika kutumia huduma rasmi za kifedha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, ninyi mnaweza mkawa ni mashahidi ya kwamba kama Wizara ya Fedha tumekuwa kila mwaka tukiadhimisha maadhimisho ya Huduma ya Wiki ya Kifedha; ambapo tumeanza mwaka 2021 – 2026 (ambapo yamefanyika rasmi tarehe 21 mwezi huu, 2026). Mimi binafsi nikimwakilisha Waziri wa Fedha nimeenda kufungua rasmi maadhimisho hayo ambayo yamefanyikia nchini (Tanga) ili wananchi waweze kupata elimu ya kifedha. Kweli wananchi wa Tanga waliyapokea kwa hali ya juu, walikuwa ni wengi. Hii ni mikakati maalum ya Wizara ya Fedha kuhakikisha ya kwamba wananchi wanapata elimu ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, maadhimisho haya yameanza muda kidogo, tangu mwaka 2021. Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na mikoa mingine imeendelea kunufaika na elimu hii.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, zaidi ya mikoa 16 mpaka sasa hivi tumeweza kufikisha huduma hiyo ya fedha, kuwapa elimu ambapo zaidi ya wananchi 64,000 ikiwemo wanawake 40,000 na wanaume 24,000 wamepata elimu hii kuhusu elimu ya fedha. Vilevile, zaidi ya halmashauri 94 nazo tumepita kuhakikisha kwamba wanapata elimu ya fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika uwekezaji wao, katika uwekezaji na kuingia sasa kuwekeza kwenye mambo yetu ya kifedha ikiwemo uwekaji akiba, mikopo, uwekezaji, bima, Bima-amana, kodi, hati fungani na mengineyo mengi, kwa sababu sisi kama Wizara ya Fedha tumejipanga ipasavyo. (Makofi)

SPIKA: Ahsante!

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, lililenga zaidi kwamba sasa sisi kama Wizara ya Fedha tumejipanga kwa namna gani kuhakikisha kwamba wale wanaokiuka taratibu zilizowekwa sasa wanaweka riba kubwa ili kujinufaisha wao.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, katika mkakati ambao tumesema kwamba tumeandaa rasimu ya kusimamia mikopo ya kidijiti ambayo inatarajiwa kuanza mwaka 2026 na 2027, sisi kama Wizara ya Fedha tumejipanga kuhakikisha ya kwamba taasisi zote zinazotoa mikopo zinafuata taratibu zote. Yeyote anayekiuka tayari tumeshaanza msako huo kuhakikisha kwamba tunasitisha leseni na kufunga kabisa, kwa sababu anakiuka taratibu ambazo Serikali imeziweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nyongeza tu kwa niaba ya Waziri wa Fedha, tunaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kuongeza juhudi zaidi katika udhibiti wa mikopo hii, kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao sasa wanatuamini na Serikali yetu hii ya Awamu ya Sita wanapata mikopo ambayo sasa inawanufaisha na wala si ile wanayoiita ‘Kausha Damu’ na sisi tumejipanga kuhakikisha kwamba tuko pamoja kuwasaidia wananchi kwa sababu ndiyo wananchi wetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ya kwamba tathmini ilifanyika na bado kuna maboresho yamefanyika, lakini bado kumekuwa na malalamiko makubwa kwa wanawake wa Dodoma Vijijini kwamba mikopo hii haiwafikii na pia kumekuwa na mchakato mrefu sana wa upatikanaji wa mikopo hiyo. Je, ni lini Serikali itakuwa na njia mbadala kwa ajili ya wanawake wa vijijini kupata mikopo sawa na wanawake wa mijini ambao wapo karibu na hizo fursa?

Mheshimiwa Spika, lingine pia kumekuwa na huo mchakato mrefu...

SPIKA: Mheshimiwa hujauliza maswali mawili?

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, hili ni swali la pili la nyongeza.

SPIKA: Sawa, endelea.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mchakato mrefu wa upatikanaji wa huduma hii ya mikopo, kwamba, wanawake wengine wamekata tamaa kabla hawajafikia kupata mikopo. Swali, je, ni lini Serikali itakuja sasa na one stop centre ambapo mwanamke huyu akienda atakuta na atapata pale pale katiba, cheti, tax clearance, service levy na huo mkopo ili kunusuru wanawake kukata tamaa ku-process mkopo huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninaomba niyajibu maswali yote mawili kwa pamoja kwa sababu yanaingiliana.

Mheshimiwa Spika, wote tutakumbuka kwamba mara baada ya kuanzisha utoaji wa mikopo awamu mpya, kwa maana ya baada ya kuachana na utaratibu wa zamani, Serikali ilizigawa halmashauri zetu katika makundi mawili. Kundi la kwanza likiwa na halmashauri 174 na kundi la pili, ikiwemo Dodoma, likiwa na halmashauri 10. Halmashauri 174 tumeendelea kutoa mikopo kupitia utaratibu ulioboreshwa, lakini halmashauri hizi 10 pia tulisema tutoe mikopo kupitia benki ili tuweze kuona kama tutafanikiwa, kama ambavyo Mheshimiwa Rais alikuwa ametamani ifanyike, hatimaye tuweze kufanya utaratibu wote utumike kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, sasa katika mikoa 10, maeneo 10 ambayo tulipanga kufanya kupitia benki ni pamoja na Jiji la Dar es Salaam, kwa maana ya Mkoa mzima wa Dar es Salaam, Dodoma, Songea Manispaa, Newala, Bumbuli, Siha, Mbulu pamoja na Itilima na Nkasi; huku kote tumeendelea kutoa kupitia utaratibu wa benki.

Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita tumekaa na benki hizi tatu ambazo tulikuwa tumezipa kazi hii; Benki za CRDB, NMB na Uchumi Commercial Bank; kwa ajili ya kufanya tathmini na kuona maeneo ambayo yamekuwa kikwazo kwa watu wetu.

Mheshimiwa Spika, msisitizo wetu na namna ambayo tumekubaliana na maelekezo ambayo tumepeana ni kwamba, mabenki ni sharti yazingatie kwamba wananchi ambao tunataka wakopeshwe mikopo hii, ni wananchi ambao hawawezi kukidhi masharti ya kibenki. Ndiyo maana tumesaini MoU ya kuhakikisha kuwa wanapewa kwa mazingira hayo hayo waliyonayo. Mheshimiwa Rais anataka watu wote wapate mikopo, hata wasiokopesheka kwenye benki. Kwa hiyo nisisitize tena kwamba tutayasimamia haya ili kuhakikisha hakuna ucheleweshwaji wa utoaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, jana tumejibu swali hapa na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amelitolea maelezo marefu na ya kina, kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na TAMISEMI wamewezeshwa. Kwanza pikipiki zaidi ya 98 ili waweze kuwafikia wananchi wetu kwenye vikundi vyao mahali walipo; na pia Serikali kupitia TAMISEMI tumekuwa tukitenga fedha kwenye OC zetu. Kila tunapopeleka OC tunapeleka na fungu kwa ajili ya Mafisa Maendeleo ya Jamii kuweza kuwafikia watu wetu. Niwaelekeze mikoa yote kupitia ma-RAS wetu wahakikishe kuwa hapawi na usumbufu wote kwa wananchi kupatiwa mikopo hii.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la watu wenye ulemavu linapigiwa kelele sana kwa sababu ya ukubwa wa tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu population ya walemavu inazidi kukua hasa baada ya ajali nyingi za bodaboda na vitu vingine. Je, Serikali haiwezi ikahama kufikiria kuhusu mikopo ya kuwawezesha wananchi wake, ikaenda sasa hata kufikiria ruzuku ili hawa wanawake ambao wana ulemavu waweze kupewa ruzuku, kwa maana hata muda wa kufanya hizo biashara hawana. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Neema kwa wazo zuri na ushauri mzuri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa watu wenye ulemavu wananufaika kupitia asilimia mbili, na ukiangalia trend ya mikopo hiyo kwa kiasi kikubwa fedha zile zimekuwa zinawatosheleza kwa sababu waombaji hawajawa wengi, lakini tunajua kuna gap ya elimu. Tunaendelea kuwaelimisha na kuhamasisha watu wenye ulemavu wapate hiyo mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la ruzuku tumelipokea kama Serikali, tutalifanyia tathmini na kuona namna nzuri ya kwenda nalo. (Makofi)
MHE. DKT. NEEMA W. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu ni hili hapa. Je, ni vipi na ni lini Serikali itafanya impact assessment kuona matokeo ya mikopo hii inayotolewa kwa wanawake inawa-transform kweli wanawake? Yaani inawabidisha kabisa wanawake; au tutakumbana na njia nyingine mbadala, labda badala ya kutoa hii mikopo kidogo kidogo kwa kila mwanamke labda tuje na kujenga viwanda ambavyo vitaweza kuajiri vijana wanawake na watu wenye ulemavu, ni lini itafanya impact assessment ili tuone matokeo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Neema ameongea jambo la muhimu sana la kufanya impact assessment kuona namna ambavyo mikopo hii imesaidia kuwakomboa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya tathmini, na tuna ushahidi wa maendeleo ya biashara hizi kwa baadhi ya vikundi. Viko vikundi ambavyo vilianza na mikopo ya milioni tano kwa mfano, lakini wakakuza biashara zao na kukopa shilingi milioni 50, shilingi milioni 60 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kuna mwendelezo mzuri wa baadhi ya vikundi ku-graduate kutoka kukopa kidogo kidogo na kufanya biashara ndogo na baadaye wanaanzisha viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali kama za kilimo na bidhaa nyingine. Kwa hiyo, tunaamini kwamba mikopo hii inaleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la kufanya impact assessment tumelichukua ili tujue, tufanye kwa ujumla wake tangu tumeanza mpaka sasa tuweze kuona mwelekeo wa tija katika mikopo hii na kuweka mipango mizuri zaidi ya kuboresha tunakoelekea mbele. (Makofi)
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa tunatamani kushiriki kwenye huu uchumi jumuishi. Ni kwa jinsi gani Serikali imejipanga kuweza kushirikisha watu kutoka vijijini, wanawake, lakini vijana watakavyoshiriki kwenye huu uchumi shirikishi. Tukizingatia sana viashiria ambavyo vitawekwa kupima kwamba makundi haya maalumu nayo yameshiriki, hasa kupitia kutafutiwa masoko, lakini utumiaji teknolojia mpya, umilikishwaji wa ardhi, siyo hivyo tu, ikiwepo upatikanaji wa ajira zikiwepo ajira zilizo rasmi na ajira ambazo siyo rasmi, ili huu uchumi jumuishi ambao utatokea, usitokee kutoka kwa wawekezaji wakubwa, lakini na sisi watu wa chini ikiwepo wanawake tuwe tumeshirikishwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimshukuru sana Dkt. Neema Majule kwa swali lake la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza swali hili ni lazima kidogo turejee katika Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ambayo imepita ambayo kwa kiasi kikubwa kwanza imefanya vizuri sana. Ambapo mpaka kufikia mwaka 2024, wastani wa pato la mtu mmoja mmoja limeweza kukua zaidi ya mara tatu, kutoka dola za Kimarekani 453 mpaka dola za Kimarekani 1,227 lakini pia umri wa kuishi nao umeongezeka kutoka wastani wa miaka 51 mpaka miaka 68.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo sasa dira hii ya miaka 25 mingine inayokuja, tumejipanga kuhakikisha kwamba makundi yote ya wanawake, vijana, wafanyabiashara, wawekezaji nao wanaenda kuguswa na dira hii ya miaka 25 ambayo tunaenda kuanza nayo tarehe 01 Julai, 2026 mpaka mwaka 2050.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tumejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba makundi hayo ambayo ameyataja, tunaenda kuyagusa kwa kiasi kikubwa na kuyawezesha kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba wanatekeleza shughuli zao za kila siku, ahsante sana.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pia kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, kuhusu vivutio ambavyo Serikali imevi-identify kabisa kwa ajili ya wawekezaji hasa wazawa, lakini kuna sheria za TRA ambazo bado zinakinzana na hivyo vivutio, ikiwepo hiyo tax exemption katika import duty, bado kuna shida lakini pia hiyo tax holiday ambayo amesema kuna grace period, inabidi wasubiri, bado kuna shida. Wenyewe TRA, wanaongozwa tu na sheria zao. Niulize sasa, je, Serikali imejipangaje ku-harmonize vivutio vyake na sheria za TRA? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wawekezaji wengi wageni wameingia hapa kwetu na hivyo wawekezaji wazawa wakiwepo wawekezaji wa kati na wadogo wanashindwa kuhimili ushindani wa uwekezaji wa nje. Je, Serikali imejipangaje kuwaandaa wawekezaji wetu wa ndani, wengi wao wakiwa ni wanawake na vijana, kuhimili ushindani wa kibiashara na wale wawekezaji wa nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Neema Peter Majule, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Mara kwa mara amekuwa akichangia sana kwenye suala la uwekezaji na hususan kuwatetea wanawake wa Dodoma kwenye masuala ya uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, hivi vivutio vimepitishwa na wenzetu wa Wizara ya Fedha, na TRA wamehusika katika kuvipitisha, lakini ninatambua kuna changamoto za hapa na pale katika administration ya hii certificate of incentives ambayo kimsingi sisi kama Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, vilevile tumekuwa tukipokea hiyo changamoto kutoka kwa wawekezaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, tumekuwa tukitatua hizi changamoto, na hivi tunaenda kutengeneza Muswada mwingine wa ile Finance Bill ambayo kimsingi tunakuja kutatua changamoto ambayo kimsingi inawakumba sana wawekezaji wetu hususan wale wanaopewa vile vivutio kwa kupitia ile certificate of incentives.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kweli wawekezaji wetu wa ndani hususan akina mama wa Mkoa wa Dodoma na vijana wakati fulani wanashindwa kushindana kwenye soko la uwekezaji, kwa sababu mbalimbali ikiwepo mitaji na kadhalika. Sisi kama Serikali, sasa hivi tunaenda kuandaa mwongozo mahususi wa incentives kwa ajili ya wazawa tu ambao utatupa way forward ni jinsi gani sasa tunaweza tukawafanya wakawa competitive na vilevile kuweka mazingira rafiki ya wao kupata mikopo na hata ardhi ili waweze kushindana na wawekezaji wanaotoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuuliza, je, Serikali ipo tayari kubaini yale maeneo ya shule ya msingi ambayo ni makubwa, ambayo yana uwezo wa kujengwa sekondari palepale ili kuendana na huu mpango wa elimu jumuishi, yaani shule ya msingi na palepale sekondari?

Mheshimiwa Naibu Spika, samahani; kwa mfano hapa Dodoma, Shule ya Ipagala 'A' ina eneo kubwa sana ambalo hapo hapo ingeweza kujengwa sekondari, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Dkt. Neema ni ya msingi, na Serikali tayari imeanza. Yako maeneo ambayo yana shule za msingi zenye maeneo makubwa, maeneo hayo pia, yametumika kujenga shule za sekondari. Kwa hiyo, zoezi hili tutaendelea kulifanya. Tutapita pia, kwenye Shule ya Msingi ya Ipagala 'A', kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ili tuweze kuona kama kuna uhitaji wa ujenzi wa shule ya sekondari na kama eneo linatosha, basi Serikali itaendelea kuyafanyia kazi.