Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Chief Thomas Mgonto Kitima (2 total)

MHE. THOMAS M. KITIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itahakikisha kila kijiji nchini kinapata mawasiliano ya kimtandao na kuwepo kwa minara ili kurahisisha mawasiliano hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Thomas Mngoto Kitima, Mbunge wa Jimbo la ikungi Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa huduma za mawasiliano ya uhakika katika kila kijiji nchini kama msingi wa kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hasa katika zama hizi za uchumi wa kidijiti. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Sekta Binafsi, imeendelea kupanua miundombinu ya mawasiliano ikiwemo ujenzi wa minara ya simu, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo bado kuna changamoto ya mawasiliano ya simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa Mpango Mkakati Mahsusi wa Ujenzi wa Minara kwa Kipindi cha Miaka Mitano (2025 – 2030). Mpango huu unalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vijiji vyote nchini vinapata huduma za mawasiliano mbadala ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya mawasiliano na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mpango huu, mwezi Disemba, 2025 Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, ilikamilisha Mradi wa Awamu ya Nane ya Ujenzi wa Minara 758 nchini. Utekelezaji wa awamu ya tisa ya ujenzi wa minara 636 unaendelea na utakamilika mwezi Disemba, 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, UCSAF inaendelea na awamu ya 10 ya ujenzi wa minara 287 ambayo mikataba yake ilisainiwa Disemba, 2025. Hatua hii inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za Mawasiliano katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na kuboresha huduma kwa wananchi.
MHE. THOMAS M. KITIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji nami naomba kujibu swali la Mheshimiwa Thomas Mgonto Kitima, Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki:-

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Dira 2050 utaanza rasmi tarehe 01 Julai, 2026 kufuatia kufikia ukomo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo yam waka 2025 tarehe 30 Juni, 2026. Utekelezaji huu ni baada ya kuzinduliwa kwa Dira 2050 tarehe 17 Julai, 2025 na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kuandaa nyenzo mbalimbali za utekelezaji wa dira hiyo, zikiwemo: -

(i) Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (Long Term Perspective Plan);

(ii) Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031;

(iii) Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo;

(iv) Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo; na

(v) Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja wa 2026/2027 (Annual Development Plan).

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa nyenzo hizo, Serikali itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 sanjari na kutoa elimu kwa umma kuhusu mfumo na utaratibu utakaotumika katika utekelezaji wa dira hiyo, pamoja na mipango ya maendeleo ya miaka mitano na ya mwaka mmoja. Aidha, utekelezaji wa nyenzo hizo utafuatiliwa na kupimwa kidijitali kupitia mfumo wa e-Delivery (Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mipango na Miradi ya Maendeleo) kwa lengo la kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na upatikanaji wa taarifa na takwimu za utekelezaji kwa wakati halisi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.