Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Chief Thomas Mgonto Kitima (4 total)

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Ikungi Mashariki, kuna visima vingi vilichimbwa, lakini maji hayajaweza kusambazwa katika maeneo mbalimbali. Mfano mzuri ni Kijiji cha Misule, Kata ya Misughaa. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi wale wa Kata ya Misughaa, Kijiji cha Misule wanaweza kusambaziwa maji na wanaweza kupata hayo maji ili waweze kuwa na imani ya Serikali yao kwa maana ya kumtua mama ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa maeneo ya Misughaa, kwanza kabisa Serikali itachimba visima na baada ya kuchimba visima tunafanya pump test na baadaye tunajiridhisha na que ya maji. Tukishajiridhisha na que ya maji, maana yake sasa ndiyo tunafanya usanifu wa kutengeneza mtandao unaoendana na maji ambayo yanazalishwa pale. Kwa hiyo, tukishajiridhisha, baadaye sasa tunayafikisha kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bajeti ya kwanza ilikuwa kuchimba visima, bajeti ya pili ni kusambaza baada ya kujiridhisha na uwingi wa maji yaliyopatikana katika visima. Ninamtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwa vile tumekamilisha uchimbaji wa visima na pump testing imeishafanyika. Sasa tuko kwenye mchakato wa kuingiza katika bajeti ya kuhakikisha kwamba sasa tunaenda kujenga mtandao wa maji ili maji yawafikie watumiaji na wananchi wa Misughaa. Ninakushukuru sana.
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunavyozungumza ni takribani wiki ya nne wananchi wa Kata ya Mang’onyi katika Jimbo la Ikungi Mashariki hawana maji kabisa, na sababu kubwa ni kwamba motor imeungua na pa kubadilishwa mpaka iende Dar es Salaam. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu hawa wa Mang’onyi ili waweze kupata huduma ya maji kwa haraka? Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Mbunge hujasikika vizuri, naomba utaje hilo eneo ambalo maji yamekatika kwa muda ili Mheshimiwa Naibu Waziri asikie.

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunavyoongea ni takribani wiki ya nne wananchi wa Kata ya Mang’onyi katika Jimbo la Ikungi Mashariki hawana huduma ya maji, na sababu ambayo inazungumzwa ni ile motor kwamba imeungua na ili ibadilishwe lazima ipelekwe Dar es Salaam.

Je, Serikali inatoa kauli gani ili hawa watu wa Mang’onyi waweze kupata maji ukizingatia ni kwamba ni kata ambayo ina wawekezaji wakubwa ambao wanasaidia maendeleo katika Jimbo zima la Ikungi Mahariki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na namshukuru sana kaka Mheshimiwa Thomas, Mbunge kutoka Ikungi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa changamoto hii na kwa Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tatizo dogo la motor haliwezi kuwafanya Watanzania wakose huduma ya maji safi na salama. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kutumia fursa hii kumwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, hili suala alifuatilie haraka sana ili wananchi hawa waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wizara ya Maji hatuwezi kushindwa kutekeleza jambo dogo kama hilo. Nimtoe hofu, hili jambo tumelipokea na tutalifanyia kazi na uhesabu kwamba hili tatizo limeisha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. kwa kuwa karibia kata nyingi hazina mawasiliano, Mfano vijiji katika Kata ya Mang’onyi, Ntuntu, Misuhaa, Kikio ambapo kuna maeneo kama Mnane, Kundi, pamoja na Makumi, ambao hawana kabisa mawasiliano; na hata mimi nikienda kwenye ziara huwa nikifika huko ni kama nipo gizani, au nimepotea na siwezi kupatikana; je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwapatia hawa watu mawasiliano kwa kuwajengea minara, hasa hasa katika maeneo yenye huduma za kijamii kama shule ili yawepo mawasiliano na iweze kufanya miradi ya Kitaifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kijiji ninachotoka kinaitwa Siuyi na nikiwa kijijini huwa ninalazimika kwenda kijiji cha jirani ambacho kinaitwa Makiungu, ili tu nipate mawasiliano. Mara nyingine huwa ninalazimika kutokufika kijijini, nilale mjini ili mradi tu nisikose taarifa za Kitaifa. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais ana jambo la Kitaifa, kwa hiyo, ninalazimika kukaa mjini ili tu niweze kupata mawasiliano, kwa kuwa kijiji ninachotoka hakuna mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaona umuhimu hiki Kijiji cha Siuyi kipate mawasiliano ya kutosha? Kwa kuwa mimi Mbunge wao ninatoka pale, wakiona hata Mbunge hana mawasiliano, itakuwa siyo jambo zuri. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara tumepokea changamoto ya Mheshimiwa Mbunge. Ninaomba nimwelekeze Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF aende jimboni kwa Mheshimiwa kufanya tathmini ya kina kuhusu tatizo hili la mawasiliano na kuchukua hatua za dharura kulifanyia utatuzi kwa kadri itakavyowezekana. (Makofi)
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dira hii inasema kwamba itawahusisha wananchi wote, kwa maana uchumi jumuishi na tunapoenda kuianza tarehe 01 Julai, 2026. Wananchi watahusikaje kwa sababu hakuna elimu ambayo imetolewa kwa umma ambayo itawafanya wawe sehemu ya mpango huu na sio wasindikizaji. Je, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wananchi wote kabla hatujaanza kutekeleza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni kwa namna gani miradi ambayo itatumika kama benchmark ama miradi ya kielelezo tunapoanza kuitekeleza dira hii tutaanza nayo mwezi Julai, ili wakati tunaendelea basi tuwe tunafanyiana assessment kupitia hiyo miradi ambayo tunaenda kuanza kuitekeleza tutakapoanza kutekeleza dira hii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nipende kumpongeza sana Mbunge wa Ikungi Mashariki, Mheshimiwa Thomas Kitima, kwa kuendelea kupambania sana wananchi wa jimbo hilo, lakini pia kama mjumbe makini katika Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza; niseme kabisa moja ya majukumu ya Wizara yetu ya Mipango na Uwekezaji kupitia Tume ya Taifa ya Mipango kwanza ni kuratibu na usimamizi wa uchumi, kupanga mipango ya maendeleo, pamoja na kutekeleza mipango ya maendeleo ambayo tayari imeshakwisha kuidhinishwa. Hii ni pamoja na kukusanya, kuchakata pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo tayari imeidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, mimi niseme ni Naibu Waziri wa Fedha, na sisi kama Wizara ya Fedha, kwanza tumejidhatiti kuhakikisha kwamba Dira hii ya 2050 inatimizwa kwa 100%. Sisi tuko tayari kuhakikisha kwamba fedha ya aina yoyote ambayo inahitajika kulingana na mpango huu wa Dira ya 2050, tuko tayari kupeleka katika Wizara ya Mipango na Uwekezaji, kuhakikisha kwamba maono sasa ya mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi hii unafikia dola za Kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, lakini pia wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja kufikia dola za Kimarekani 7,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa namna hiyo nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Mbunge wa Ikungi Mashariki, sisi kama Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, tuko tayari kuhakikisha kwamba mipango yote ambayo imo ndani ya Dira ya 2050 inatekelezwa bila kikwazo chochote kwa ukamilifu wake.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ameuliza sasa ni kwa namna gani elimu kwa umma tunaenda kuifikisha huko. Kwanza niseme kabisa jambo hili la elimu kwa umma sio jambo la Serikali pekee yake, bali ni jukumu letu sisi kama Serikali, lakini pia na Wabunge wote ambapo tutakapokuwa tunakwenda kwenye majimbo yetu, ni lazima tuhakikishe ya kwamba tunatoa elimu kwa umma ili umma sasa uelewe kwamba Dira hii ya 2050 imebeba maono gani.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Dira ya Maendeleo ya miaka 25 kuanzia Julai 01, Dira ya Maendeleo 2050, kwanza na yenyewe kwa ukubwa wake, hatuwezi kuwakwepa sekta binafsi. Nazo tumezijumuisha kuhakikisha kwamba sekta binafsi zina-play role kubwa kutekeleza utekelezaji wa Ilani ya Dira ya Maendeleo 2050. Pia wenzetu wa Wizara ya Mipango, wana mpango mkakati mzuri sana wa kutoa elimu kwa umma kupitia platform mbalimbali ikiwemo makongamano, social media na vyombo vingine ambavyo vitahakikisha kwamba elimu ya utekelezaji wa Dira 2050 wananchi wanaielewa vizuri ili na wao waipokee kwa ajili ya utekelezaji wa dira hiyo.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuwasilisha