Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Mshamu Ali Munde (4 total)

MHE. HARAN N. SANGA aliuliza: -

Je, lini wafanyakazi wa Tanzania watapunguziwa riba ya mikopo na kufikia asilimia saba au nane?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge wa Kigamboni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na sera za uchumi wa nchi yetu, riba za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha nchini kwa wateja mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi huamuliwa na soko (market determined). Hivyo, Serikali inaona kuwa kuelekeza taasisi za fedha kuweka viwango vya riba vya asilimia saba au kiwango chochote mahususi au maalumu kwa ajili ya wafanyakazi itakuwa inakinzana na maelekezo ya sera za soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kuwa swali hili lina msingi wa kwamba taasisi za fedha, maeneo pekee ambayo yanapata faida kwa kukopesha ni kwa watumishi ambao mishahara yao kukatwa ni rahisi. Hata hivyo, taasisi ya fedha inaweza kuweka kiwango cha riba kwenye mikopo ya wafanyakazi au mkopaji yeyote kufikia asilimia saba au pungufu ya hapo, kama itaona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wafanyakazi au mkopaji yeyote anaweza kukubaliana na taasisi ya fedha na kupata kiwango cha riba cha asilimia saba au pungufu kwa kadri itakavyowezekana. Vilevile, wafanyakazi kupitia waajiri wao wanayo fursa ya kuwasiliana na benki husika na kukubaliana riba wanayoweza kutoza wafanyakazi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Edward Mwakyembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kugharamia ulipaji wa madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2025/2026, shilingi bilioni 700 zilitengwa ambapo hadi Februari, 2026 jumla ya shilingi bilioni 477.6 zimetolewa. Kadhalika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 800 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kugharamia ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa suala la madeni ya wakandarasi na wazabuni linadhibitiwa, Serikali inaendelea kutoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kupitia waraka mbalimbali za utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti katika mwaka husika. Maelekezo ya Serikali ni kama yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafungu kutenga bajeti kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi, lakini pia Maafisa Masuuli kutumia mifumo ya kudhibiti matumizi hali kadhalika kuhakikisha kuwa mchakato wowote wa ununuzi unaanzishwa baada ya kujiridhisha uwepo wa bajeti na uhakika wa upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka vivutio maalumu vya kikodi kwa vijana wanaoanza biashara ili kuchochea ajira na kukuza uchumi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Lutengano George Mwalwiba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni swali No. 1,425. Kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Lutengano kwa kuwapambania sana wananchi wake wa Jimbo la Busekelo, na kwa namna anavyowasimamia. Pia ninafahamu Mheshimiwa Lutengano amekuwa akiwatetea sana vijana hata wakati akiwa anahudumu kwenye nafasi ya ukurugenzi kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo tulikuwa wote huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatekeleza mikakati mbalimbali ya kikodi inayolenga kukuza biashara ndogo ndogo, hususan za vijana, na kuhamasisha uingiaji wao katika uchumi rasmi. Miongoni mwa mikakati hiyo, ni utekelezaji wa Mfumo wa Kodi ya Makadirio (Presumptive Tax Scheme) unaolenga walipakodi wadogo wasiokuwa na kumbukumbu sahihi za mapato au vitabu vya hesabu, ambapo masharti yake ni mepesi na yanatabirika ili kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili biashara zao na kuanza kulipa kodi kwa hiari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha utaratibu wa kipindi cha neema (grace period) kinachowaruhusu wafanyabiashara wapya kufanya biashara bila kulipa kodi kwa muda wa miezi sita tangu kuanza biashara. Hatua hizi zinalenga kuwapa wajasiriamali nafasi ya kukuza biashara zao bila mzigo wa kodi katika hatua za awali. Hii itaongeza ubunifu, kuvutia wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi kuingia kwenye mfumo rasmi, na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali kwa njia endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kutoa vivutio maalumu vya kikodi kwa vijana ili kuchochea uanzishaji wa biashara na ajira, ikiwemo msamaha wa kodi na viwango pungufu, huku ikiendelea kufanya tathmini ya athari zake ili kuhakikisha usawa, ufanisi wa sera, na uendelevu wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 na maboresho yake ya mwaka 2024, Serikali pia inatoa ahirisho la kodi ya mapato (Corporate Income Tax) kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo kwa biashara mpya (start-ups), hatua inayolenga kusaidia biashara changa kukua na hatimaye kuwa walipakodi wakubwa na endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DANIEL A. TLEMAI K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Mkoa wa Kikodi katika Wilaya ya Karatu? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, lililowasilishwa na Mheshimiwa Daniel Awack, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakupongeza sana kwa kazi nzito na nzuri unayoendelea kuifanya na pia kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi wa Karatu kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo. Hii dhana ya jimbo langu, jimbo langu, Karatu ninaona haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa Mkoa wa Kikodi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Karatu, hufanyika kwa kuzingatia vigezo vya kiutawala na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kiasi cha mapato kinachokusanywa, idadi ya walipakodi, rasilimali zilizopo, pamoja na mahitaji ya huduma katika eneo husika. Lengo kuu ni kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongeza ufanisi na kusogeza huduma kwa walipakodi, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezipandisha hadhi baadhi ya wilaya za kikodi kuwa mikoa ya kikodi, ikiwemo Mkoa wa Kikodi wa Ilala, Kinondoni, Temeke, Kariakoo, Kahama, Tegeta na Pemba. Wilaya hizo zilizopewa hadhi ya mikoa ya kikodi, zina wastani wa jumla ya walipakodi, kwa mfano Ilala ni 906,399, Kinondoni 734,984, Temeke 563,568, Kariakoo 67,996, Kahama 82,054, Tegeta 136,164, na Pemba walipa kodi 28,076.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika katika mwaka 2023/2024 na 2024/2025 wilaya hizo zilikuwa na wastani wa mapato ya kodi shilingi bilioni 862 kwa Ilala, shilingi bilioni 774 kwa Kinondoni, shilingi bilioni 190 kwa Temeke, shilingi bilioni 136 kwa Kariakoo, shilingi bilioni 25.89 kwa Kahama, shilingi bilioni 101 kwa Tegeta na shilingi bilioni 16.36 kwa Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muundo wa kikodi wa sasa, Wilaya ya Karatu inatambulika kama Wilaya ya Kikodi, chini ya Mkoa wa kikodi wa Arusha, ndani ya Idara ya Kodi za Ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Aidha, Wilaya ina jumla ya walipakodi 4,672 ambao kwa kiasi kikubwa wanachangia ukusanyaji wa mapato ya kodi kutoka katika vyanzo za utalii, madini na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika, takwimu zinabainisha ukuaji wa asilimia tisa nukta nne nane wa mapato ya kodi katika wilaya hiyo, kwa kuzingatia makusanyo yenye jumla ya shilingi bilioni 10.07 kwa mwaka 2023/2024 na shilingi bilioni 11.12 kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huu, Serikali kupitia TRA, itaendelea kutathmini na kufuatilia kwa karibu ukuaji huu wa mapato, ongezeko la idadi ya walipakodi na shughuli nyingine za kiuchumi katika Wilaya ya Karatu, ili vigezo vya kupewa hadhi ya Mkoa wa Kikodi vitakapokamilika, hatua stahiki ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kutafuta rasimali muhimu za kufanikisha suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha inatambua kwamba, swali lako linalenga kudumisha na kuimarisha mapato ya kodi ya nchi hii kwa kupanua wigo na kuimarisha ufanisi wa vyanzo vilivyopo. Ninakupongeza kwa hatua hiyo, lakini Wizara ya Fedha itaendelea kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mkoa wa Kikodi kwenye Wilaya ya Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.