Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Mshamu Ali Munde (7 total)

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze tu majibu ya Serikali, lakini nataka kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki zetu zinazoitwa commercial banks zinategemea vitu viwili katika kufanya biashara, kwa kutumia consumers’ loan na Government Bond, kwa sababu hivi vitu vyote vina security kwao. Kwa Serikali kuacha watumishi ambao wamekuwa wakitumikia miaka yao 55, 60 mpaka 65, amekuwa akifanya kazi za Serikali, kwa sababu tunaamini kabisa watumishi wa Serikali siyo wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mshahara wake ndicho kitu pekee ambacho anakitegemea ili aweze kupata mkopo aweze kujenga nyumba, apate mkopo aweze kutengeneza maisha yake ya kujikimu kwa ajili ya kustaafu. Je, Serikali ina kauli gani ambayo itawasaidia watumishi hawa kuanza kuwa-motivate katika kufanya kazi, na pia kuwasaidia kwamba watapokuwa wanastaafu, wawe na maisha bora ya kujikimu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Sanga, anauliza maswali haya bila shaka ni kutokana na kwamba wafanyakazi hawa ni dada zetu, ni kaka zetu na wengine ni wanetu. Kwa hiyo, maisha yao na matumaini yao ya kuishi kwa kufanya kazi, mwisho wa siku yawe na faida kwao. Serikali itaendelea kuandaa mazingira wezeshi ya kifedha kwa watumishi kama ambavyo imekuwa ikifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliunda mfuko maalum wa Advances Fund kupitia Tangazo la Serikali Na. 709 lililotoka mwaka 2018 likisomeka kama “Advances Fund Establishment Order.” Lengo kuu la kuanzishwa mfuko huu ilikuwa ni kuwezesha utoaji wa mikopo kwa watumishi wa umma kwa masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Advances Fund huwa inatozwa kwa gharama ya jumla ya asilimia nne, ambayo kimsingi huwa ni kwa ajili ya services charges na bima tu ya huo mfuko. Mpango huu unawahusisha wafanyakazi au tuseme watumishi wa umma, kwa maana ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na utekelezaji wa utaratibu huu, Serikali ilielekeza taasisi nyingine za umma kuanzisha mifuko yao ya ndani ya utoaji mikopo kwa watumishi wao kwa lengo la kuhakikisha wanapata mikopo yenye masharti nafuu na hivyo kuwezesha kuimarisha ustawi wa uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2021 hadi Januari, 2026 watumishi hao wamekopeshwa zaidi ya shilingi bilioni 497, lakini kwa kipindi cha mwaka 2025/2026 pekee watumishi wamekopeshwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 74.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo, watumishi hao wataendelea kuishi kwa matumaini na watastaafu wakiwa wanawezeshwa na Serikali, na bila shaka mpango huu utaendelea kufanyika na jitihada nyingine za kuwezesha wafanyakazi waweze kuwa na maisha mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninamshukuru sana Naibu Waziri kaka yangu Mheshimiwa Munde kwa majibu mazuri ya Serikali pamoja na mikakati ambayo imewekwa kwa ajili ya ulipwaji madeni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Serikali inaendelea kutekeleza upatikanaji wa ajira milioni nane ambazo zimeainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi mpaka kufikia mwaka 2030 na pia niwapongeze sekta binafsi ambapo zinavyoongeza kuongeza ajira za vijana wa kike na kiume katika kutekeleza Ilani hiyo ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza. Serikali ina mpango gani katika kusimamia madeni hayo yasiongezeke hasa ya wazabuni na wakandarasi wazawa ili kuendelea kulinda mitaji yao na wao hao kuendelea kulinda ajira za vijana wa kike na wa kiume, lakini pia na kuhakikisha madeni ya watumishi yanalipwa na madeni ya watumishi hayaongezeki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Edward Mwakyembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli madeni ya wazabuni na wakandarasi pamoja na watumishi ni kero ambayo Wizara imeipata, lakini pia kupitia Wabunge mbalimbali jambo hili limekuwa likiongelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuliona hilo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kesho siku ya Jumatano, tarehe 20 Mei itakutana na Wizara ya Fedha katika kutafakari na kuhakikisha kwamba madeni hasa hasa ya wazabuni na wakandarasi wa ndani yanaweza kulipwa ili uchumi uweze kuzunguka lakini pia vijana ambao wamefanya kazi kwenye miradi hiyo waweze kupata kujikimu na kuinua vipato na uchumi wa mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la madeni Serikalini ni suala ambalo limeumiza watu wengi sana, kwanza kwa sababu uhakiki wa madeni hauna kipindi maalum kwamba uhakiki wa madeni utafanyika ndani ya mwaka mmoja, ndani ya miaka miwili, ndani ya miaka mitatu. Kwa hiyo, wale wakopaji ambao walifanya miradi hii ya Serikali kwa nia njema wamekuwa wakiumizwa kwa interest za mabenki na wengi wamekuwa wakilalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara hii ya Fedha isikae na hao Maafisa Masuuli, kwa sababu hata hicho kinachosemwa kuanzisha miradi mipya baada ya ile miradi mingine kulipwa hakifanyiki. Kwa nini Wizara hii isingekuwa inakaa inawasaidia hawa ambao wanadai kuweza kuongea na mabenki walau kuangalia njia sahihi za kuwasaidia ikiwemo kupatana kwenye suala zima la interest badala ya kutoa maelekezo ambayo kwa kweli yamekuwa akiumiza sana watu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Lucy kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua ni kweli wakandarasi na wazabuni wamekuwa wakiumia sana kutokana na kutolipwa kwa wakati ambazo wamezifanya katika miradi ya maendeleo ambayo inahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakiki kwa sasa kama nilivyotangulia kusema umefanyika kupitia Maafisa Masuuli, lakini pia Wizara za Kisekta na baadhi ya taarifa zilizo nyingi tumeshazipata na ndio maana kesho tuna kikao mahsusi kwa ajili ya kupitia orodha zote za madeni ili tuweze kupanga mkakati ambao utaenda kupunguza kabisa na kama sio kuondoa kwa kiwango kikubwa madeni yote ambayo wazabuni wanaidai Serikali ili mwisho wa siku twende kuangalia miradi mipya badala ya kuhangaika na madeni ambayo mpaka sasa hivi wazabuni na wakandarasi wanadai.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali italipa madeni ya wakandarasi wa Wilaya ya Meatu ambayo yameshafanyiwa uhakiki na kutumwa TAMISEMI na Hazina kwa ajili ya malipo? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nijibu kwa ujumla.

Mheshimiwa Tinnar Chenge ninashukuru sana kwa swali lako lakini niseme wazi kwamba amesema madeni ya Wilaya ya Meatu. Hayo ni madeni jumuishi ambayo haijulikani sasa ni wakandarasi wa Wizara ya Maji au miradi ya barabara au ni miradi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea naye nje ya forum hii ili kupata uhakika na specific hoja yake iko vipi ili tuweze kumjibu kiuhalisia kutokana na swali ambalo atakuwa ametupatia nje ya kikao hiki. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru kwa nafasi.

Swali langu linasema je, Serikali imeweka mikakati gani katika kuongeza uwazi na uwajibikaji kwenye mchakato wa ulipaji wa madeni ya wakandarasi na wazabuni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la dogo la nyongeza la Mheshimiwa Janeth kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema kuhusiana na uwazi na uwajibikaji Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho linapitia taarifa zote za madeni ya wakandarasi na wazabuni. Kamati hiyo wajumbe wake ni Wabunge, Wabunge ambao wanawakilisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa ambazo tunazipeleka sisi kama Wizara ya Fedha inaenda kuwekwa wazi mbele ya Kamati ambayo mwisho wa siku tunaonesha ule uwazi wa kwamba madeni yote ambayo yamehakikiwa, ambayo hayajahakikiwa kiasi gani tunaenda kulipa na mkakati gani tunaenda kuufanya ili kulipa madeni hayo. Huo ndio uwazi na uwajibikaji ambao tunaongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imepitisha vivutio mbalimbali vya kikodi kama Import Duty Exemption, VAT Exemption, Capital Allowance, lakini pia na kuwapa wafanyabiashara na wawekezaji ndani na nje ya nchi the grace period, je, ni kwa nini Serikali inachelewesha kuwaruhusu au kuwapa muda mwafaka wa kutumia zile incentives ambazo wale wafanyabiashara wanakuwa wanataka kuzitumia na wanaruhusiwa kisheria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Je, Serikali ina takwimu ya watu wanaonufaika na vivutio hivi vya kikodi? Kama haina, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba vivutio hivi haviwanufaishi wachache, bali vinawanufaisha watu wengi wakiwemo vijana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vivutio vya kodi katika kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Ni kweli pia kuwa hapo awali kulikuwepo na changamoto zilizosababisha ucheleweshwaji wa utoaji wa vivutio hivyo. Changamoto hizo zilihusisha urasimu wa kiutendaji, ucheleweshwaji wa maamuzi, ukosefu wa utaratibu wa kutosha kati ya taasisi mbalimbali pamoja na mkanganyiko wa tafsiri za baadhi ya sheria na hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kubaini hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali madhubuti kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo TISEZA. Sasa hivi angalau kuna one stop centre ambapo wawekezaji wanaweza wakaenda kuwasilisha maombi yao kuhusiana na vivutio stahiki kwenye sekta ambayo wanaenda kuifanyia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna ushirikishwaji mkubwa wa taasisi kama TCCIA ambayo pia tunaitumia kwa ajili ya kuwaelekeza wafanyabiashara vivutio stahiki katika maeneo ambayo wanaenda kuwekeza. Jambo hili inaelekea baada ya hatua hizo linaenda kupungua, na hivyo vivutio vitatoka kwa wakati, hasa kwa startups kama vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusiana na takwimu, Serikali kweli inatoa vivutio hivyo, hususan kwa vijana. Hata hivyo, kwa sasa hatuna takwimu zinazoonesha asilimia ambayo inatupa picha ya wale ambao wamefaidika na vivutio hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivutio hivyo vimekuwa vikitolewa, lakini mtazamo siyo vivutio, tathmini imekuwa ikitolewa kwa kuangalia mtazamo mpana kuliko kuangalia asilimia ya watu ambao wanafaidika. Kwa mfano, kwa kuangalia ajira na shughuli za kiuchumi katika jamii. Kwa sasa tunafikiri Wizara ya Fedha inaweza ikapata takwimu nzuri zaidi pale ambapo sasa tumeanza kutumia mfumo wa IDRAS ambao unachukua takwimu za walipa kodi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuko na utaratibu wa kuwaelekeza, na hapa nielekeze kwa dhati kabisa wenzetu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, waweze kuanzisha utaratibu. Ninajua upo utaratibu wa mafunzo kwa wafanyabiashara, hasa vijana ambao wanaanza biashara kwa sasa, hasa kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipokuwa na takwimu na vijana hawa wasipopata mafunzo stahiki kwa ajili ya kutumia zile fedha, zile fedha zitakuwa kama zile ambazo Wabunge tulikuwa tukilalamikia hapa, kwamba, fedha za 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri zimekuwa zikienda na maji bila habari kutokana na vijana kuchukua fedha bila kuwa na maarifa stahiki ya kutumia fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni 200 lazima zilete tija kwa vijana. Kwa hiyo, nawaambia na kuwahimiza Mamlaka ya Mapato Tanzania, pamoja na jitihada wanazofanya za kuwapa mafunzo na kutoa vivutio hivyo ambavyo nimeviongelea, watoe mafunzo stahiki kwa vijana, ili mwisho wa siku shilingi bilioni 200 zilete tija kwao. Pia, kama tunavyosisitiza, wawe ni wajasirimali ambao wanakuja ku-graduate kuwa wafanyabiashara wakubwa watakaoleta tija na kuinufaisha nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mapato (TRA) wamekuwa wakikusanya kodi kwa wafanyabiashara wetu kwa kupitia mtaji, kitu ambacho kinawakatisha tamaa wafanyabiashara walio wengi wakiwemo vijana, lakini pia, Serikali kukosa mapato halisi. Je, Serikali iko tayari sasa kukusanya kodi kwenye faida, ili mfanyabiashara aweze kupata moyo na kulichangia Taifa lake kwenye shughuli za maendeleo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu kwa ufupi.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, sijapata swali sehemu ya mwanzo, TRA inafanya utaratibu wa kukusanya kodi kupitia nini?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti Majala.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linasema, TRA mfanyabiashara anapoenda kuchukua leseni, pamoja na TIN, kodi anayokadiriwa ni pamoja na mtaji wake bila kuangalia kwamba, mtaji ule ameupata wapi? Mitaji mingi ya wafanyabiashara wetu wamekopa. Kwa hiyo, TRA inachukua kodi kulingana na mtaji wa mteja alionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalan Kunti ninaenda kuanzisha biashara ya shilingi 4,000,000, kwa hiyo, TRA inapokuja kuni-charge mimi ina-charge kupitia ile shilingi 4,000,000 na siyo faida iliyotokana na shilingi 4,000,000. Kwa hiyo, swali langu, ninataka kujua Serikali mko tayari kuchukua kodi kwenye faida badala ya mtaji wa mteja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huo haupo, na ndio maana hata tunavyoongelea Corporate Tax tunaongelea kodi kutoka kwenye faida. Hoja hii ninaichukua kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge, kama kweli kuna matukio ya wafanyabiashara kulipishwa kodi kutoka kwenye mtaji, kwa sababu, kodi haitakiwi kufilisi biashara hiyo, ndiyo hasa mustakabali wa kodi halisi. Kodi inatakiwa ichukuliwe kutoka kwenye faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoongelea wajasiriamali wadogo, wao wamekuwa exempted kabisa kutolipa kodi, hasa wale ambao wanazalisha fedha chini ya shilingi 4,000,000. Kwa hiyo, hata wale ambao ni zaidi ya shilingi 4,000,000 kitakachotokea ni kwamba, watalipa kodi kwenye faida wanayozalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema wazi pia, tumezungumzia kwamba, wajasiriamali wadogo wana msamaha wa kulipa kodi, lakini pia, uki-graduate kutoka kwenye msamaha, utapata maelekezo wewe kama mfanyabiashara, ni kwa namna gani unakokotoa faida yako ili ihusishwe kwenye kulipia kodi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)