Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mabula Johnson Magangila (3 total)

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi ya kuongeza pale ambapo Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Ninaomba nikusaidie kidogo, jina langu ni Mabula Magangila kutoka Jimbo la Msalala, Mkoani Shinyanga, Wilaya ya Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, kwetu sisi Wanamsalala kwanza kabisa, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi njema kabisa ambazo anafanya kwa Taifa letu. Kwetu sisi siyo tu hotuba, kwetu sisi Mheshimiwa Rais amegusa maisha ya Wanamsalala, lakini kabla ya Wanamsalala ninaomba nisemee sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ni Rais ambaye amekusudia kuleta mageuzi makubwa kwa sekta binafsi. Ni Mheshimiwa Rais huyu ambaye ameingia madarakani nchi yetu ikiwa inakusanya shilingi trilioni 18, leo hii tunakusanya shilingi trilioni 32, mapato haya hayatoki nje ya wafanyabiashara ni Rais huyu ndiye aliyeboresha mazingira na kuweka mazingira wezeshi ya wafanyabiashara. Rais huyu ndiye aliyekataa kamatakamata ya wafanyabiashara, ni Rais huyu ndiye aliyeweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa vibali katika sekta yoyote unayotaka kufanya biashara, ni Rais huyu ndiye aliyethubutu kutunga sera nzuri kabisa, hasa katika sekta ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumza hapa Awamu ya Sita ndiyo ambayo migodi mingi mipya imeanzishwa. Wachimbaji wadogowadogo na wanaojifunza kuchimba wamechimba, wanaojua kuchimba wanachimba, wenye leseni wanachimba, wanaotaka kushirikiana na wenye leseni wanachimba, awe ni mtu ambaye anataka kwenda kuokota ukwale, wale akinamama wanapata dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu hii ya Sita umeanzishwa mgodi pale Sengerema, Mgodi wa Nyanzaga. Ni katika Awamu hii ya Sita umeanzishwa mgodi kule Kabanga Nickel ambao unamilikiwa na Tembo Nickel, katika Awamu hii ya Sita. Leo hii tayari pilot plant ya madini ya uranium imekamilika, Awamu hii ya Sita, lakini kwenye graphite tayari tuna Faru Graphite, tuna Lindi Jumbo tayari uzalishaji umekwishaanza. Ni Rais huyu ndiye ambaye ameruhusu haya yote yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya yote kufanyika katika sekta hii binafsi naomba Wizara ya Fedha, haya mambo yote aliyoyafanya Mheshimiwa Rais kwa utashi wake Bunge hili tukubaliane yawekewe sasa Sheria kali, ili yasije tena yakabadilika na kupeleka huzuni kubwa kwa wafanyabiashara. Tungependa kusudio hili la Mheshimiwa Rais la kuboresha sekta hii binafsi na kuifanya Serikali yake kuwa ni sekta wezeshi na siyo sekta inayo-control na kuzuia maendeleo ya Watanzania. Tukatunge sera nzuri, tuweke Sheria nzuri za kuendelea kuweka hali hii ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia isichezewe na mtu yeyote atakayekuja hata baada ya yeye kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya madini, tumeweza kuanzisha migodi mipya, lakini ni migodi ambayo ilifanyiwa utafiti miaka mingi nyuma, twendeni sasa kupitia Wizara yetu ya Madini, Mheshimiwa Rais amekusudia kuweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi, ili kukuza sekta binafsi. Twendeni tukaweke vivutio hivyo, tukaongeze utafiti. Kampuni nyingi za utafiti, hasa zinazomiliki leseni kubwa za utafiti ziliacha kutafiti. Tunapoacha kutafiti tunaua matarajio ya kuwa na migodi mingine mikubwa kama Geita, kama Barrick, North Mara na Bulyanhulu, ambayo ilitafitiwa miaka mingi nyuma. Twendeni tukae na hawa wawekezaji, tuangalie ni kwa namna gani tutawavutia watafiti migodi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii sisi Msalala tunanufaika na mwekezaji mmoja tu, Bulyanhulu, ambaye ameweza kutuchangia CSR ya kujenga barabara ya lami kutoka Kahama kwenda mpaka kule Kakola, kilometa 71, shilingi bilioni 101. Hivi leo hawa wawekezaji wetu tukiwavutia zaidi, wakatafiti migodi mingine, wakaanzisha migodi mingine, tukafungua migodi mingine mikubwa zaidi kwa kushirikiana na wachimbaji wetu wadogowadogo tutapata CSR kiasi gani; hata hizi pesa tunazohangaika kutafuta, kwa ajili ya miradi yetu ya TARURA inawezekana TARURA na wenyewe wakajenga barabara nyingi za lami kuliko za moramu. Twendeni tukaimarishe sekta binafsi tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, ili tuhakikishe tunapa pesa nyingi zaidi, kwa ajili ya ku-finance miradi yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Msalala kwa kumchagua Mheshimiwa Rais kwa kishindo. Mimi Mbunge wao ninawaahidi sitawaangusha, sisi kule tunasema jambo moja tu, Msalala moja, maendeleo kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Niungane na wenzangu kuwapongeza sana Wizara ya Madini, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Kiruswa. Kwa kweli hotuba hii ya leo ni nzuri sana na kwa kweli inatoa matumaini makubwa sana kwa wachimbaji wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kahama ambapo kwa madini ni mkoa wa kimadini, katika leseni 1,640 leseni 840 zinapatikana Jimbo la Msalala za wachimbaji wadogo. Katika leseni 70 za utafiti, leseni 32 zinapatikana Jimbo la Msalala, lakini Jimbo la Msalala lina kata 18, kata 12 ni za wachimbaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Msalala ukizungumzia kwenye uzalishaji wa madini katika mkoa wa kimadini wa Kahama, tunazalisha mpaka kuanzia mwezi wa saba mpaka mwezi wa tatu tani 1.7 zimezalishwa katika mkoa wa kimadini wa Kahama, tani 1.3 zimetoka Msalala. Kwa upande wa makusanyo Serikalini, Serikali imekusanya shilingi 135,000,000,000 katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama, shilingi 110,000,000,000 zimetoka Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia adha wanazopitia wachimbaji katika Jimbo la Msalala, endapo zikitatuliwa wanaweza kuzalisha mara mbili ya hiki ambacho tumekusanya. Katika Jimbo la Msalala tunazalisha miezi minne kwa nusu uzalishaji hasa katika msimu wa mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake barabara zetu kule hazipitiki, ukiangalia tunazo barabara kama saba ambazo hizi peke yake ndizo zinazochangia haya mapato yote ambayo tumeyaleta hapa. Barabara hizo ni Segese - Jomu, Lunguya namba tisa, Nyambula - Chela na Masavi – Chela. Hizi barabara zikiweza kupitika misimu yote tunakwenda ku-double huu uzalishaji ambao tunaufanya kwenye Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto ambazo zimeibuka. Tunaishukuru sana Wizara ya Madini kwa kuendelea kusimamia sekta hii, lakini tuna changamoto za wenye mashamba, wachimbaji wadogo wenye maduara, lakini wenye leseni. Tayari suluhisho limekwishapatikana kwa wachimbaji wenye maduara pamoja na wenye leseni, lakini tunaomba sasa sheria yetu iende ikawatambue wenye mashamba, ili mtu anapoomba leseni kwenye mfumo ikiwezekana apewe kwa 80%, 20% ibaki kwa wenye mashamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sisi hapa kwa wachimbaji wakubwa, tuna 16% inabaki kwa ajili ya Taifa letu. Kwa nini kwa wachimbaji wadogo tusiweke angalau 20% au hiyo hiyo 16% ibaki kwa wenye mashamba? Ili mtu anavyokwenda kuwekeza, either lile eneo liwe la kwake amelinunua ama aende akaingie ubia na wenye mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwezekana wenye mashamba waunde vikundi ili wamiliki pamoja leseni ili kuondoa migogoro. Sasa hivi tunayo migogoro kwenye maeneo yetu. Tunao mgogoro Mheshimiwa Waziri anaufahamu, mgogoro wa Busulwangili unaendana na hizi hizi changamoto. Mgogoro wa Mwakata unaendana na hizi hizi changamoto, kwamba unakuta anayeomba leseni, anaomba leseni akiwa Dar es Salaam hajui leseni anayokwenda kupatiwa tayari kule walishaanza kuchimba miaka miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akija kupewa leseni huku yeye anakwenda pale, anavyoanza kuwafukuza; mtu alikuwa anapata mgao kama mmiliki mwenye shamba, anapata mgao wa shilingi 200,000,000 au shilingi 300,000,000 kila mgao unapofanyika, wanauza mawe, kila mgao unapofanyika anapata mgao, leo unakwenda kumkadiria heka moja shilingi 800,000 kwa sheria ya ardhi. Lazima mgogoro utaibuka tu kwa namna yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumza Jimbo la Msalala lina kata 18, kata 12 ni za wachimbaji. Hizo kata zote zikiwa na migogoro hilo jimbo litakuwaje? Tutakaa kila siku tunatatua migogoro kwenye hilo eneo. Niombe tuwatambue wenye mashamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine, Mheshimiwa Waziri ninaomba sasa leseni hizo ambazo tumezifuta, tukawagawie vijana wetu na akina mama ili waweze kuendeleza leseni hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanafasihii. Kwanza kabisa, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wa Wizara ya Maji kwa miradi ambayo imetekelezwa katika Jimbo la Msalala, yenye thamani ya shilingi bilioni 32.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wananchi wa Msalala wanampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa fedha hizi nyingi ambazo ametuletea jimboni kwetu. Mheshimiwa Waziri amekuja na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni, tukawaambia tunayo miradi yetu ambayo bado haijakamilika. Mradi wa Nduku, Busangi, ambao unatakiwa utoke Nduku, Busangi, ufike Ntobo, makao makuu ya halmashauri. Tunaomba mradi huu uweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa Mangwi, Ilogi, ambao unatakiwa utoke Mangwi, Ilogi, ufike Lunguya. Wananchi wa Lunguya wanausubiria sana mradi huu uweze kukamilika. Tunao mradi wa Mwamboku, Magongwa, ambao haujawahi hata kuanza, lakini wananchi wanausubiria kwa hamu sana, ili uweze kutatua kero ya maji katika Kata ya Kashishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa Vijiji 21, ambao huu unakwenda kugusa kata tisa. Kata tano ni ambazo zina vyanzo vya maji ya visima virefu, ambapo tayari visima virefu vipo. Kwa hiyo, ni ukamilishaji tu wa usambazaji wa maji katika visima hivyo. Unazungumzia Kata ya Ikinda, Kata ya Shilela, Segese, Mega na Chela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi ambao, pamoja na kimya cha Mheshimiwa Waziri cha kukamilisha mradi ule ambao ulianza, sisi katika Jimbo la Msalala bomba la Ziwa Victoria limepita kwenye jimbo letu. Tunavyo vijiji tisa ambavyo vinapitiwa na bomba la Ziwa Victoria, ambapo mradi huu unagusa kata nne; Kata ya Mwalugulu katika Kijiji cha Sungamile, Kata ya Mwakata, Kata ya Isakajano, Vijiji vya Matinje na pia, unagusa Mradi ambao unatakiwa ukamilike wa vijiji viwili ambavyo viko kwenye Kata ya Isakajana, ambavyo ni Jana yenyewe pamoja na Butondolo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Msalala, Serikali ikikamilisha Mradi huu wa Vijiji 21 unakwenda kuwa na vijiji 75 kati ya vijiji 92 vya Jimbo la Msalala. Kwa kweli, atakuwa ametusaidia sana katika jitihada za kumtua ndoo mama kichwani. Miradi yetu hii mingi ni ya kufikisha maji kijijini. Gharama za kuvuta maji kufikisha majumbani bado ni gharama kubwa sana. CBWSOs zetu tayari zinafanya vizuri sana kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi baada ya kutufikishia maji haya kwa kiwango hiki, kuanzia mwezi wa Saba mpaka leo hii, kaya 428 zimeshaunganishwa maji, lakini bado gharama ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe CBWSOs zetu ziendelee kutekeleza miradi midogo midogo ya kusogeza maji kwa wananchi, ili gharama ya kuvuta maji kutoka kwenye bomba kufikisha kwenye kaya za wananchi wetu ipungue na hiyo ndiyo maana halisi ya kumtua ndoo mama kichwani. Badala ya kwenda kuchota maji kwenye DP na kuleta nyumbani, tunataka wananchi wetu wachote maji majumbabi mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa gridi ya Maji ambao tunasema, tutatoa maji Ziwa Victoria, lakini tunayo mikoa ambayo hata ukichimba maji chini unakutana na chumvi. Upi mpango wa Wizara wa kuvuna maji ya mvua ya kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunao Mradi wa Lita za Ujazo Milioni Nane ambao ni wa Bwawa la Maji ya Mvua ulioachwa na Buzwagi, pale Kahama. Tunapeleka maji yale kwenye tenki letu la maji, pale shule.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana na ninaomba kuunga mkono hoja.