Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Mhe. Dickson Nathan Lutevele (3 total)

MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza: -

Je, lini malipo ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Karatasi (SPM Mgololo) yatafanyika, ukizingatia kuwa ni ya muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara ninaomba nijibu swali namba 35 kutoka kwa Mheshimiwa Dickson Nathan Lutevele, Mbunge wa Mafinga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Southern Paper Mills Ltd. (SPM) ilibinafsishwa mwezi Februari, 2004 kwa mwekezaji aitwae RAI Group kutoka Kenya. Baada ya ubinafsishwaji, wafanyakazi wapatao 760 wa kiwanda hicho walifungua Shauri Na.162/2017 la madai katika Mahakama Kuu Tanzania Divisheni ya Kazi dhidi ya Serikali wakidai mafao ya utumishi wao kabla ya kubinafsisha kiwanda hicho. Suala hili la madai ya wafanyakazi hawa bado lipo ngazi ya Mahakama.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stand ya kisasa ya mabasi Halmashauri ya Mji wa Mafinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dickson Nathan Lutevele Villa, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mapango wa kujenga stand ya kisasa ya mabasi katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga katika Kata ya Kinyanambo kupitia Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Miji (TACTIC) Awamu ya Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ulikamilika mwezi Februari, 2026 na taarifa ilishawasilishwa kwa timu ya uratibu wa miradi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Halmashauri ya Mji wa Mafinga. Kwa sasa Mtaalam Mshauri Kampuni ya Botek Bosphorus Consulting Corporation kwa kushirikiana na kampuni ya Building design Authority (P) Ltd wanaendelea kufanya usanifu wa mwisho ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya usanifu kukamilika, hatua itakayofuata ni kutangaza zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi mjenzi. Pindi taratibu hizo zikikamilika, ujenzi wa stand ya mabasi katika mji wa Mafinga utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa Kodi ya 30% katika export ya Mazao ya Misitu ambayo imeua kabisa Viwanda?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya marekebisho ya Sheria, kulikuwa na usafirishaji mkubwa wa mazao ya misitu nje ya nchi yasiyochakatwa au yaliyochakatwa kidogo na ni mfano wa magogo na Veneer sheets. Hivyo, mwaka 2025 Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Usafirishaji wa Bidhaa Nje ya Nchi, Sura 196 ili kutoza ushuru kwa kiwango cha 30% au shilingi 150 kutegemeana na kiwango kitakachokuwa kikubwa kwa kila kilo moja ya vinia inayotambulika kwa Tariff Heading 44.08 inayosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya marekebisho hayo ili kulinda viwanda vya ndani katika kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za viwanda vyetu vya ndani vinavyotengeneza bidhaa za mbao ikiwemo plywood na marine board. Pamoja na marekebisho hayo, Serikali pia ilifanya marekebisho kwa kuongeza ushuru wa forodha kwa marine board zinazoingizwa nchini kutoka 25% hadi 35% ili kuviongezea viwanda vyetu vya ndani ushindani dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imepokea changamoto aliyoieleza Mheshimiwa Mbunge kuwa hatua hii imeathiri baadhi ya Viwanda. Viwanda vinavyoweza kuathirika ni vile vinavyochakata mazao ya misitu bila kufikia hatua za mwisho za uzalishaji wa bidhaa za misitu kwa matumizi yaliyokusudiwa. Hivyo, Serikali inaendelea kujielekeza kwenye kutafuta suluhu ambayo haitaleta athari hasi kwenye sekta hii ndogo kutokana na hatua zinazochukuliwa ili kuilinda sekta hii muhimu katika uchumi wetu, na pia kwa kuhakikisha kuwa kuna uongezaji thamani wa mazao ya misitu kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Fedha ili kuona namna ya kurekebisha kodi hii pale itakapothibitika kuwa inazuia ukuaji wa viwanda badala ya kuvilinda, ili kuhakikisha mnyororo wa thamani wa misitu unamnufaisha mwekezaji na Taifa kwa ujumla.