Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Mhe. Dickson Nathan Lutevele (5 total)

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali. Kwanza kabisa niishukuru Serikali kwamba Halmashauri ya Mji wa Mafinga ni moja kati ya miji ambayo ilipata Mradi wa Maji wa Miji 28 na mradi huu ilikuwa ukamilike mwezi Juni mwaka uliopita, lakini mpaka sasa hivi mradi huu uko 28% tu ya utekelezaji wake. Ninaomba kauli ya Serikali, je, ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Mafinga waweze kupata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kaka yangu Mwenezi wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo hilo ambaye ameanza kwa kasi kubwa sana, na mwezi mmoja tu uliopita nilikuwa naye kwenye ziara katika jimbo lake, na tulipitia baadhi ya miradi, na mradi ambao ameuongelea ni mradi unaotekelezwa na Jandu Plumbers ambapo ni kweli ulikuwa unasuasua, lakini tuliwaita wakandarasi tukakaa tukakubaliana warudi site waweze kuendelea kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaamini kwamba kwa kadiri fedha ambavyo zitakuwa zinapatikana tutahakikisha tunamwezesha mkandarasi aweze kukamilisha huu mradi kwa wakati. Ninashukuru sana.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wafanyakazi hawa wa Kiwanda cha SPM - Mgololo walishinda kesi ya msingi mwaka 2007 na katika kesi hiyo ya msingi Mahakama iliamuru wadai hawa walipwe kwa pande zote mbili, kwa maana ya mwekezaji kwa wale wafanyakazi wachache aliokuwa amewachukua, lakini na Serikali iwalipe wale wafanyakazi 760 ambao walikuwa hawajapewa barua ya kusitishiwa ajira yao na wala hawaendelei na kazi; kwa maana kwamba walikuwa wameachwa hewani. Mahakama ikaamuru kwamba walipwe tokea mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; sasa je, Serikali haioni kama ipo haja ya kuumaliza huu mgogoro ili Watanzania hawa ambao walifanya kazi kubwa ya uzalishaji katika kiwanda kile, katika kujenga nchi yetu na wao wakapata haki yao ambayo wameitumikia kwa muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Rais wetu mpendwa kupitia Bunge hili alisema anatamani wakati anaondoka, angeacha tabasamu kwa Watanzania. Serikali haioni kama ipo haja ya kuumaliza huu mgogoro kwa kuona ni namna gani wanawafidia wafanyakazi wale ambao kwa kipindi kirefu sasa wanaisubiri hii fedha na kiwanda kile kilikuwa kikifanyiwa kazi na Watanzania kutoka nchi nzima na wanashindwa kuondoka Mgololo kwa sababu wamefanya kazi muda mrefu, hawana fedha na hawajapata mafao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi na utu ndiyo kaulimbiu yetu na tabasamu la utu katika utumishi ni moja ya malengo ambayo tunayafanyia kazi chini ya maelekezo yake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wetu. Kwa muktadha huo, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lutevele, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaingia hapa kwa sababu yenyewe ndiyo ilikuwa mmiliki wa kiwanda hiki kabla ya ubinafsishwaji wake. Kimsingi ninaomba nikiri kwamba madai haya chimbuko lake ni kupunguzwa kazi kwa baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hiki na mwekezaji ameshalipa madai ambayo yanayomhusu kwa upande wake. Uhakiki ulifanyika kwa upande wa Serikali katika dhana ile ile ya kuacha tabasamu la utu na tayari Serikali ilifikia tamati kwa kupata kiwango cha fedha ambacho ni malipo stahiki kwa watumishi wa kiwanda hicho. Serikali ilitoa fedha hizo katika mwaka 2017 na 2018. Hata hivyo, wafanyakazi hao walikataa kuchukua kiasi hicho kwa madai kwamba ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, Serikali imeshtakiwa na suala hili bado liko Mahakamani na kinachogombewa hapa ni kwamba, kiwango ambacho kimetoka ni kidogo, lakini nia ya Serikali ni kumaliza mgogoro huo ili wananchi hawa wapate haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Mafinga tulipata mradi wa stendi ambayo ilikuwa ikamilike kujengwa mwaka uliopita, lakini mpaka sasa tunaambiwa kwamba, wakandarasi wapo kwenye hatua za drawings. Sasa naomba nipate kauli ya Serikali kwamba, ni lini stendi hii itajengwa kwenye Mji wa Mafinga ambao mpaka sasa hatuna stendi ya kisasa na tunaihitaji sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, Serikali iliweka mpango kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa katika Mji wa Mafinga na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Villa, amekuwa akifuatilia mara kwa mara. Ninaomba nimhakikishie kwamba, kama alivyosema, tayari tuna mkandarasi, lakini kazi haijaanza na tunajua kuna sababu ambazo zimesababisha mkandarasi kutokamilisha kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mafinga tuko kwenye hatua za kuhakikisha mkandarasi anarejea kazini, anaanza kufanya kazi hiyo, ili kukamilisha ujenzi wa sehemu hiyo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kazi hiyo itafanyika.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, naishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini nilikuwa na swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na utaratibu baada ya upembuzi yakinifu kufanyika, kuchelewesha sana mkandarasi kuanza kazi. Stand hii, sisi Halmashauri ya Mji wa Mafinga mpaka sasa hatuna stand. Pale ambapo mabasi yanasimama ni kandokando ya barabara, eneo ambalo limekuwa na ajali nyingi sana, lakini kwa sisi Wana-Mafinga pia, stand hii tunaisubiri kama moja kati ya vyanzo vya mapato kwa sababu mji wetu una msongamano mkubwa sana wa magari, lakini hatuna stand.

Je, nini kauli ya Serikali, ni kwa uharaka upi kwenye kuhakikisha kwamba stand hii, pindi tu upembuzi utakapokuwa umekamilika, tunapata mkandarasi na stand hii inajengwa kwa sababu Wana-Mafinga wameisubiri stand hii kwa muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Dickson Nathan Lutevele, Mbunge wa Mafinga Mjini, amefuatilia mara kadhaa kuhakikisha kwamba ujenzi wa stand ya kisasa ya mabasi ya mji wa Mafinga inafanyika. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini kwamba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba stand hiyo inajengwa mapema iwezekanavyo na ndiyo maana tayari tumeshafanya hatua za awali za usanifu na upembuzi yakinifu na tuko hatua ya pili ya mtaalamu mshauri ambaye anakamilisha kazi yake mwezi Mei mwaka huu, kwa maana ya mwezi huu mwishoni. Tutahakikisha baada ya ukamilishaji huo, tunaendelea na taratibu zetu za Serikali pamoja na Benki ya Dunia ili kutoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

Kwa hiyo, kauli ya Serikali Mheshimiwa Mbunge ni kwamba dhamira yetu ni kuhakikisha tunaanza ujenzi mapema iwezekanavyo baada ya hatua hizi kukamilika.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninaomba nimwulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa teknolojia hii ya AI ndiyo inayoongoza dunia kwa sasa, na mara nyingi fursa kama hizi zinawapata tu vijana wa mjini, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuhakikisha kwamba teknolojia hii mnazunguka hasa vijijini ikiwemo maeneo ya mikoani kama Mafinga kwa ajili ya kuwafundisha vijana wote ili waweze kupata fursa hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwafikia vijana katika maeneo ya mikoa mbalimbali, ndiyo sababu nimeeleza kwamba tumeanza utaratibu wa kujenga vitu vya ubunifu nchini. Tumeanzia na mikoa ambayo nimeitaja, Mikoa ya Lindi, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, na Zanzibar, na tutaendelea hatua kwa hatua kuwekeza katika mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali wa Kimataifa. Kwa mfano, tunashirikiana na International Telecommunication Union (ITU), wanafanya mradi na Tume ya TEHAMA. Huu mradi unaitwa ITU IA For Good Sandbox. Mradi huu unatekelezwa kwa vijana wote nchini bila kujali ni wa mjini au wa vijijini, kwa lengo la kuwapa uwezo wa kutengeneza mifumo ya AI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inalitambua hilo, na pia inashirikiana na UNESCO kuwekeza katika maeneo haya. Hili litahusisha watumishi wote wa Serikali walio mjini na maeneo yote ya nchini, vijijini na kila sehemu kwa kuwajengea uwezo wa eneo hili la akili mnemba.