Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. John Francisco Nzilanyingi (1 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nipate fursa ya kuchangia kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu. Jambo la kwanza, ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kuwa sehemu ya Bunge hili Tukufu, Bunge la Kumi na Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimshukuru sana Dkt. Samia chini ya uongozi wake ndani ya chama kwa kuona kuwa nami ninafaa kuwa sehemu ya kuwakilisha Wananyamagana kwa kipindi hiki cha miaka mitano. Mwisho na kwa umuhimu niwashukuru sana wananchi wakazi wa Jimbo la Nyamagana kwa namna ambavyo alinipa imani na hata wanavyoendelea kushirikiana na mimi. Kwa wanavyonitia moyo inanipa faraja ya kusonga mbele katika kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo; Mpango wote huu ambao umewasilishwa kwetu na Wizara ya Mipango pamoja na Wizara ya Fedha; tunafahamu kuwa chini ya uongozi wa Wizara hii ya Profesa Mkumbo amefanya kazi nzuri sana; na katika hili ninampongeza. Wizara ya Fedha pia imejikita katika kutuandalia mambo ambayo kwa kweli kama yatatekelezwa basi tutegemee kuona uchumi wa Taifa letu unapaa kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Wabunge mtakubaliana nami, kwamba mpango huu tunaouzungumza unahitaji fedha, ndipo tutapowagusa Watanzania, hususan kundi la vijana. Nimejaribu kupitia mpango huu takriban kila ukurasa kijana wa Kitanzania ameguswa. Ajira ambazo tunazungumza kwenda kuzitengeneza ni ajira kwa ajili ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanikiwa kuufanikisha mpango huu ni lazima tuwe na fedha. Katika hili ninaomba nishauri katika maeneo makubwa matatu. Kwa sababu ninatoka kwenye kanda ya ziwa kwenye Jimbo la Nyamagana, wananchi wa Jimbo la Nyamagana walinituma nije niseme hapa, niishauri Serikali. Kwa muda mrefu sana kwa nature ya Mkoa wetu wa Mwanza tunao uwanja wetu wa ndege, ambao kama ungeweza kukamilishwa kujengwa na kupewa hadhi ya kimataifa, ninataka niwahakikishie, Serikali yetu na Taifa letu litapata fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiutazama uwanja wetu huu wa Mwanza, kutoka Mwanza kwenda Serengeti si zaidi ya kilometa 140 peke yake; lakini Uwanja wetu huu wa Ndege wa Mwanza ndiyo uwanja nambari moja unaoongoza kwa kusafirisha dhahabu kutoka kwenye Taifa letu. Uwanja huu unahudumia kanda ya ziwa yote. Hii inaonesha ni kwa namna gani kukamilishwa kupewa hadhi ya uwanja huu kuwa wa kimataifa uchumi wa Jiji letu la Mwanza na Taifa kwa ujumla utapaa kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niishauri Serikali kwamba, mwaka juzi ilisaini mkataba kwa zaidi ya bilioni 29, lakini cha kusikitisha mkandarasi sasa kwa taarifa nilizonazo na kwa macho yangu tayari anaondoa vifaa site, maana yake hakuna matumaini. Wanamwanza wanauhitaji sana uwanja huu kwa ukuaji wa uchumi wao. Niwahakikishie uwanja huu ukikamilika na ukiwa wa kimataifa tunakwenda kutengeneza ajira nyingi sana kwa vijana wakazi wa Mkoa wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili uwanja huu tukiupa kipaumbele Taifa letu litakwenda kuongeza fedha za kigeni kutokana na watalii tutakaowapata. Kwa kuonesha msisitizo, wakati Serikali inatangaza mpango wa kuupa hadhi Uwanja wetu huu wa Kimataifa wa Mwanza wenzetu wa Shirika la NSSF walikuja kuweza. Tunayo hoteli pale eneo la Kapri Point ambapo Serikali ya Tanzania imelaza zaidi ya bilioni 90. Mtu pekee aliyekuwa amelengwa kulala kwenye hiyo hoteli ya zaidi ya bilioni 90 alikuwa ni mtalii, tukiamini kwamba uwanja ukikamilika watalii wengi watapita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo fedha ya Serikali zaidi ya bilioni 90 imelala pale na Wanamwanza hawayaoni matumaini ambayo wangetamani wayapate. Kwa hiyo, ninaomba nishauri Serikali iweke jitihada za haraka kwamba kwenye mpango huu wa mwaka mmoja wa miaka mitano na miaka ishirini na tano iliyosalia tuhakikishe kuwa jambo hili tunalibeba kama la dharura kwa sababu tutapata fedha ambazo zitakuza Uchumi na zaidi ya yote tutatengeneza ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Shirika letu la Ndege la Air Tanzania. Mapato linayoyapata kwa mwaka zaidi ya 75% yanazalishwa na Kiwanja cha Ndege cha Mwanza. Ni namna gani Serikali inaweza ikaonesha commitment ya kwamba hata kwa namna ambavyo shirika letu la ndege; maana bila Mwanza nina hakika haliwezi kujiendesha; kwa sababu kama ni 75% tafsiri yake ni kwamba Air Tanzania ipo kwa ajili ya Mwanza kabla ya kuwaza kwingine kokote kwa sababu ndipo mapato hasa yanakotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye sekta nyingine ya uvuvi. Mkoa wetu wa Mwanza na Jimbo la Nyamagana Mungu ametupa neema ya kipekee sana. Tunalo ziwa ambalo hawajapewa kwingine kokote kule. Ukiangalia ziwa hili kama Serikali hatujalitumia ipasavyo. Miaka ya 2000 wataalam wetu walikaa chini wakawaza wakaleta samaki aina ya sangara akaja akapandikizwa. Kulitokea mfumuko mkubwa sana wa ujenzi wa viwanda vya Samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza Mwanza tumebaki na viwanda saba peke yake. Kupitia viwanda vile tulitengeneza ajira, pia Serikali ilipata fedha na wananchi mmoja mmoja uchumi wao ulikuwa sana. Mimi ni shuhuda kwa sababu niko pale mjini. Wapo watu maarufu ambao wana majina ya samaki, samaki ambao walikuwa wanatoka ndani ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niiombe Serikali kwa msisitizo mkubwa sana. Serikali yetu kwa mipango ambayo nimeisoma kwenye mpango huu, kama ikiamua kwa dhati, ikaamua kutekeleza kama ambavyo imejielekeza basi Ziwa letu Victoria linaweza likawanufaisha Watanzania wengi na tukatengeneza ajira kwa vijana wetu walioko ndani ya Mkoa wa Mwanza na Jiji letu la Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili, ninataka niiombe Serikali, kwamba tuondokane na uvuvi huu wa kizamani. Uvuvi haramu unaofanyika kule ndiyo umesababisha kupotea viwanda zaidi ya 16 kwa sababu ya kukosa malighafi ya samaki. Serikali ni lazima ije na mpango mkakati wa kuhakikisha inawaza ni kwa namna gani tunakwenda kufanya transformation kwenye sekta ya uvuvi ili tutengeneze ajira tupate fedha za kigeni; na zaidi ya yote Taifa letu la Tanzania lipate fedha za kutosha, fedha ambazo zitatengeneza miradi mingi ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande kingine ambacho ningependa nichangie ni kuhusu barabara. Mpango huu uliowasilishwa na Profesa Kitila Mkumbo ni wa kisayansi sana, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, muda umekwisha.

MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia; kwa sababu ya muda; Dkt. Samia Suluhu Hassan popote alipo atembee kifua mbele kwa sababu kazi nzuri ameifanya. Miradi inatekelezwa kule kwetu Mwanza, barabara zinajengwa. Katika yote, ninaomba nimhakikishie kwamba Wanamwanza wanamuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)