Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. John Francisco Nzilanyingi (4 total)

MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi kufufua Viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza ajira na mapato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, ninaomba kutumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kumsaidia kama Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Ninamuahidi kwamba nitafanya kazi hii kwa weledi, nguvu, bidii kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijaalia.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa John Fransisco Nzilanyingi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango kabambe wa kuendeleza Sekta ya Uvuvi wa mwaka 2021 – 2037 ambapo kipaumbele ni kuendeleza, kuanzisha, kuimarisha na kufufua viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nchini ili kufikia kwenye uchumi wa viwanda unaoongozwa na sekta binafsi kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha viwanda vyetu vinafanya kazi kulingana na matarajio ya Serikali, Wizara ipo katika hatua za maamuzi kulingana na taratibu za Serikali kuanzisha Mamlaka ya Uvuvi kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kupambana na uvuvi usiozingatia sheria ili kuongeza upatikanaji wa samaki na hivyo kuwezesha viwanda vyetu kupata malighafi za kutosha. Kwa hatua za awali Wizara imeweka maboya 32 yenye thamani ya shilingi milioni 224 kwa ajili ya kulinda mazalia ya samaki katika eneo la Luchelele - Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi, Wizara imeanzisha Dawati la Mitaji na Uwekezaji kwa lengo la kufuatilia kwa ukaribu changamoto zinazoikabili Sekta Binafsi (vikiwemo viwanda hivi vya samaki), kuzitafutia ufumbuzi na kuongeza uwekezaji na uchangiaji kwenye pato la Taifa ili kufikia azma ya Serikali ya kuelekea kwenye Uchumi wa Viwanda. Aidha, mipango mingine ya Wizara ni pamoja na kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa vizimba ili kuwezesha upatikanaji wa samaki kwa wingi. Mpango huu utasaidia kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda. Ninashukuru sana.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege Mwanza utakamilika ili uwe na hadhi ya Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Serikali wa kufanya maboresho makubwa ya Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ili kuwa cha kimataifa umeanza. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaohusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, upanuzi wa eneo la maegesho ya ndege na ujenzi wa barabara za kiungio unaendelea.

Mheshimiwa Spika, ujenzi utaanza mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya njia nne kutoka Mjini – Usagara na kutoka Mjini – Kisesa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa John Francisco Nzilanyingi, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa barabara za kutoka Mwanza Mjini hadi Usagara na kutoka Mwanza Mjini hadi Kisesa kwa ajili ya ujenzi wa njia nne kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hizi utafanyika kwa awamu ambapo kwa sasa Serikali iko katika hatua ya mwisho ya manunuzi ya kumpata mkandarasi atakayejenga barabara ya kutoka Mwanza Mjini hadi Usagara yenye urefu wa kilometa 25 kwa njia nne kwa kiwango cha lami. Kwa sehemu ya Mwanza Mjini hadi Kisesa, tayari Serikali imejenga sehemu ya meta 500 kwa njia nne sambamba na ujenzi wa Daraja la Mabatini. Ujenzi wa sehemu iliyobaki utaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.

MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa John Francisco Nzilanyingi, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya mara kwa mara ya barabara za vijijini na mjini ili kuwezesha shughuli za usafirishaji kufanyika kwa urahisi kote nchini ikiwemo katika Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya fedha za barabara katika Jimbo la Nyamagana imeongezeka kutoka shilingi bilioni 3.47 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 6.49 mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya barabara zinazoendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sasa katika Jimbo la Nyamagana ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mwananchi - Mahinakati kilometa 0.3, Mwananchi - Bugurika kilometa 0.16, Igelegele - Mahinakati, Buhongwa - Lwanchima (kilometa 3.8) ambazo kwa pamoja zinagharamia jumla ya takribani shilingi milioni 853.28. Aidha, ujenzi wa barabara ya Buhongwa - Lwanchima (kilometa 3.8) umetekelezwa kwa shilingi bilioni 5.9 kupitia mradi wa TACTIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025 Serikali imeendelea na ujenzi wa barabara ya Kishiri - Fumagila (kilometa 1.5) kwa shilingi milioni 304.99 na katika mwaka wa fedha 2026/2027 zimetengwa fedha kiasi cha shilingi milioni 83.93 ujenzi wa barabara ya Bugayamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti ya kujenga barabara za pembezoni kwa awamu katika Jimbo la Nyamagana zikiwemo barabara za Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima. Ahsante.