Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. John Francisco Nzilanyingi (5 total)

MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi nyingine ili niweze kupata kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni nini mpango wa Serikali wa kupambana na uvuvi haramu ambao unatajwa ndicho chanzo cha uhaba wa samaki na hivyo kupelekea viwanda vingi vifungwe?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika majibu ya Serikali, pamoja na jitihada ambazo inafanya za kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, Serikali bado haioni kwamba tutaendelea kuwa na changamoto ya upungufu wa samaki kwa sababu viwanda vyetu havitumii samaki aina ya sato ambaye ndiye hasa anafugwa kwenye vizimba vya samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri. Katika swali la kwanza, Serikali inatambua uzito wa changamoto ya uvuvi usiozingatia sheria na athari kubwa ambazo uvuvi huu umeleta katika uchumi wetu na ndiyo maana mpaka sasa tunaendelea na jitihada mbalimbali na mipango ya kupambana na uvuvi huu haramu ikiwemo kuunda Mamlaka ya Uvuvi ambayo iko katika hatua mbalimbali na Mamlaka hii itapewa nguvu ya kisheria na kikanuni ya kupambana na uvuvi huu haramu.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea na doria mbalimbali za ulinzi kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi letu la Ulinzi wa Wananchi ili kuhakikisha tunaendelea kupambana na uvuvi huu usiozingatia sheria. Serikali pia inaendelea kushirikisha jamii zetu katika kulinda rasilimali hizi za uvuvi kupitia BMU zetu ambazo tunazo katika mialo yote nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kutoa elimu kwa wavuvi wetu lakini pia tunaendelea kudhibiti uingizwaji na uuzwaji wa zana mbalimbali ambazo zinachochea au kuchangia katika uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, tunatambua pamoja na kwamba Serikali na kwa jitihada za Mheshimiwa Rais, tunaendeleza programu mbalimbali za kuwezesha Watanzania yakiwemo makundi mbalimbali ya vijana, wanawake na vyama vya ushirika kushiriki katika uvuvi kupitia uvuvi wa vizimba. Hata hivyo bado tunatambua kwamba uvuvi huu hauwezi kuwa mbadala wa uvuvi wa asili.

Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, ndiyo maana tunaendelea na jitihada mbalimbali za kupambana na uvuvi usiozingatia sheria, kuu zaidi ikiwa ni uundwaji wa Mamlaka hii ya Uvuvi ambayo utaratibu wake katika Mpango wetu wa Serikali unaendelea vizuri. Tunawaomba tu Waheshimiwa Wabunge kwamba pindi tutakapokamilisha taratibu zetu za kiserikali na kuleta mpango huu wa uundwaji wa Mamlaka hii, basi watuunge mkono ili tuweze kuipa nguvu hii ya kisheria na kikanuni kupambana na uvuvi huu usiozingatia sheria. Ninashukuru sana. (Makofi)
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini ninaomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ninaomba kufahamu, huo upembuzi yakinifu unahusisha kitu gani na utakamilika lini? Kwa sababu tarehe 28 Machi, 2024, Serikali ilisaini mkataba na mkandarasi anayeitwa Taifa Civil Mining Limited, mkataba ambao ulikuwa na zaidi ya thamani ya bilioni 29.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Serikali, wananchi wa Nyamagana, nikiwemo mimi mwenyewe kama mwakilishi wao, ninapata mkanganyiko wa nini ambacho kinaendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu, ilhali Serikali tayari imekwishasaini mkataba.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; toka Serikali isaini mkataba huo, haijawahi kupeleka hata senti tano. Hivi ninavyozungumza, kwa taarifa nilizonazo, mkandarasi ameanza kuondoa vifaa vyake site. Ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili mkandarasi aweze kuendelea na kazi ya ujenzi wa uwanja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Nzilanyingi kwa ufuatiliaji wake wa karibu kwenye uwanja wetu huo wa Mwanza, lakini yeye Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla. Kiko kilio kimoja ambacho wamekuwa wakikitoa kwa muda mrefu, ni lini uwanja wa Mwanza utapewa hadhi ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia maombi hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan, amepokea kilio hicho na amefanya usanifu, ametuelekeza kama sekta chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa tumefanya tathmini ya kina na kubaini kuwa, iko haja kubwa ya kuufanya uwanja kuwa wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, sasa mambo mazuri yanahitaji pia subira, nini kinafanyika kama nilivyosema? Mambo matatu; la kwanza Jengo lilopo kwa sasa, linatosha abiria karibu 400,000 – 500,000. Tunataka tufanye usanifu ili tuweze kujenga jengo kubwa litakaloweza kubeba abiria zaidi ya milioni mbili na laki tano. Ili ndani ya jengo, tuweze kuweka taasisi zote muhimu ambazo ni sifa na takwa muhimu kwenye uwanja wa kimataifa; Uhamiaji, Afya, pamoja na Maliasili na vitu vingine vingine. Mbili, runway; ili uwanja uweze kuwa wa kimataifa, ule upana wake hautoshi. Tunaongeza kutoka meta 45 mpaka meta 60 na ku-maintain urefu uliopo wa takribani meta 3,800.

Mheshimiwa Spika, la tatu, ni taa. Ule uwanja uliopo awali tulifikiri pengine zile taa zingetosha, lakini baada ya tathmini ya kina, inaonekana kabisa kwamba zile taa hazitatosha kwa sababu zilijengwa miaka ya 1970. Hivyo basi, tunataka tubadilishe taa zilizopo na kuweka za kisasa. Kwa sababu hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wote waweze kuwa na subira.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameuliza kwamba Serikali haikupeleka fedha ni kweli na jengo lililopo linafanya nini? Jengo lililopo sasa ambalo tulikuwa tumeshaanza ujenzi ambao tunashirikisha sekta binafsi tutalitumia kwa ajili ya general aviation. ndege ndogo, wale watu wa premium, ukiwa na ndege yako, utatumia jengo hilo. Lengo ni jema tu, kuhakikisha kwamba tunaupa hadhi ya kimataifa na inayostahili uwanja huo ambao unasafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nchini kwetu minofu ya samaki, maliasili pamoja na utalii, kwa maana ya utalii kwa ujumla na kadhalika. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi. Hitaji la Uwanja wa Ndege wa Njombe ni kubwa sana kutokana na uchumi wa Njombe, lakini ni mradi wa kimkakati, pia ni ahadi Rais, ni lini sasa ujenzi wa uwanja huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mwanyika kwa ufuatiliaji wake wa karibu sana juu ya Uwanja wa Ndege wa Njombe. Yeye na Wabunge wenzake wa Mkoa wa Njombe wanafanya kazi nzuri. Serikali imetambua na kuthamini umuhimu wa uwanja wa Njombe kama nilivyosema kwenye kubebea mazao kama vile parachichi na kadhalika na kwa sababu hiyo, Serikali inakwenda kujenga uwanja mkubwa. Ni hatua gani tuko mpaka sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, tayari tulikuwa kwenye hatua ya kwanza ya kutafuta eneo, kwa sababu eneo la pale mjini halitoshi. Tayari viongozi wa mkoa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wanashirikiana. Hatua ya pili tunayokwenda sasa ni kwa ajili ya kufanya usanifu ili tuweze kujua kiasi gani kinachohitajika uwanja utakaojengwa uweze kwenda sawasawa na hadhi ya Mkoa wa Njombe.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Mwanza ni jiji ambalo linakuwa kwa kasi sana na ukuaji wa jiji hili linaenda sambamba na ongezeko la watu jambo ambalo linapelekea kuwa na foleni kubwa sana. Naomba kufahamu kutoka Serikalini, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ni lini sasa tender ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mwanza kwenda Usagara itatangazwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jiji letu la Mwanza lina malango makuu mawili kwa maana ya njia ya Usagara Mjini pamoja na ya Mwanza - Kisesa. Ujenzi wa barabara hizi unapaswa kwenda sambamba kwa sababu ni barabara ambazo ni mapacha na yanategemeana sana kwa ukuaji wa uchumi wa jiji letu. Naomba kufahamu, tunavyoendelea na mchakato wa upande wa Mwanza – Usagara, ni lini sasa Mwanza - Kisesa nayo itawekwa kwenye mchakato wa kutangazwa ili iweze kujengwa kwa kiwango cha njia nne? Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi nimesema tuko kwenye hatua za mwisho na kama tuko hatua za mwisho ni kwamba, tulishatangaza tender na mkandarasi alishapatikana. Tunachofanya sasa hivi ni majadiliano ama negotiations, kulingana na ukweli kwamba sisi tunakuwa na engineer estimate, yaani makadirio. Sisi tunategemea hiyo barabara itakwenda, itajengwa kwa kiasi gani na mkandarasi anakuja na bei zake ambazo tuko kwenye majadiliano ili tukikubaliana na sisi tutakuwa tuko tayari kumpa hiyo kazi ya kuanza ujenzi.

Kwa hiyo, hatua ya kutangaza tulishakamilisha, tuko kwenye majadiliano na mkandarasi ambaye tunadhani anaweza akatujengea hiyo barabara na tukishakamilisha, maana yake tutakuwa tunaanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala lako la pili kwamba ziende sambamba na nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, Jiji la Mwanza linakuwa sana, lakini kama nilivyosema kwamba, inategemea na uwezo wa kibajeti kwa wakati huo.

Kwa hiyo, kwa sasa tumeamua kwamba, kwanza tuanze na hiyo na kama fedha Serikali itapatikana na ndiyo maana tumeshasanifu na hata wakati tunafanya marekebisho ya pale Mabatini, tumejenga katika mtazamo huo huo wa njia nne, ambazo tunaamini barabara itakapoanza kujengwa, basi itafuata utaratibu huo huo. Kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba, tutaijenga pia hiyo Barabara ya Mwanza-Kisesa kwa njia nne. Ahsante.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali miwili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu ya Serikali swali langu la kwanza hali ya barabara kwenye Jimbo la Nyamagana kutokana na uharibifu ulioletwa na madhara ya mvua ni mkubwa sana, maeneo ya Mahina, maeneo ya Luchelele, maeneo ya Lwanchima maeneo ya Igogo, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mpango wa Serikali wa kwenda kufanya kazi kwa haraka ili tuweze kuwanusuru wananchi kwenye maeneo yao ili barabara ziweze kupitika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya Mkuyuni Mahina - Mandu kwenda mpaka Nailipichi yenye urefu wa kilometa 10.5, imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Tarehe 19 Disemba ya mwaka 2024 Waziri wa TAMISEMI alikuja kuitembelea barabara ile na akaahidi kutoa fedha ili ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami uweze kuanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ...

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, toka Waziri wa TAMISEMI amekuja sasa yapata zaidi ya miaka mitatu. Ni nini kauli ya Serikali juu ya uanzaji wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 10.5 ili iweze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Nyamagana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie tu kwamba Serikali inatambua kwamba tuna changamoto ya uharibifu mkubwa wa baadhi ya barabara katika Jimbo la Nyamagana zikiwemo barabara za Mahina, Luchelele na nyingine ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie tu kwamba tayari tumeshapokea taarifa rasmi ya tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya mategenezo ya barabara hizo na hivi sasa Serikali inaendelea na hatua za mwisho za kuandaa utaratibu wa fedha ili kupelekwa fedha katika maeneo yote yenye uharibifu wa barabara, zikiwemo barabara za Jimbo la Nyamagana kwa ajili ya matengenezo ya dharura na ya kawaida ili ziweze kupitika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Nzilanyingi, kwamba tunafahamu na tuko katika hatua za kupeleka fedha ili barabara hizi ziweze kujengwa na kuweza kupitika vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili kuhusiana na barabara hiyo ya Mbuyuni yenye urefu wa kilometa 10.5 kufanyiwa usanifu, maana yake ni hatua ya mwanzo kuelekea kumpata mkandarasi na baadaye kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo. Kwa hiyo, kauli ya Serikali ni kwamba kama ambavyo tumedhamiria na kufanya usanifu tutaendelea kujiandaa kwa maana ya kutafufa fedha na kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo ipo kwenye mpango. (Makofi)