Contributions by Hon. Dr. Emanuel Qambaji Nuwas (4 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana. Pia ninapenda kuanza kwa andiko moja kutoka Waraka wa Kwanza wa Yohana 02:14 ambao unasema, “Nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu mna nguvu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu lina vijana wa kutosha 34% ya population ambao wana nguvu na tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa na kizazi ambacho kina nguvu ndani ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana ambao Biblia inasema tunawaandikia, na kwa kuwa wana nguvu; Biblia inasema kwamba, pia wamejaa Neno la Mungu. Nami ninasema, wamejaa pia maarifa, ujuzi na uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunasema kwamba hawa vijana wetu ni rasilimali na ni fursa kwa ajili ya nchi yetu na wao wenyewe. Kwa hiyo, ninapenda kuanza na andiko hilo na kusema kwamba tutambue rasilimali hii kubwa ambayo nchi yetu imejaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba pia hawa vijana wetu wanachangia asilimia kubwa sana ya nguvu kazi, zaidi ya 55%. Kwa hiyo, kama nchi kwa kweli ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutambua kundi hili la vijana ambao ni zaidi ya 34%, kwa kuliundia Wizara kabisa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana wetu wametawanyika, wapo vijijini na mijini. Vilevile, wana elimu tofauti, wengine wamemaliza darasa la saba, wengine hawajamaliza, wengine wapo Form Four, wengine vyuo, ngazi mbalimbali za elimu. Lazima tuwatambue na kuwapa fursa sawa za kuweza kuwaendeleza na kuweza kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutambua mchango huu, Rais amefanya kazi kubwa, ndiyo maana ametoa ajira 12,000, ajira 5,000 sekta ya afya na 7,000 sekta ya elimu. Bado tumesikia juzi katika mwaka unaokuja zaidi ya 45,000 watakwenda kuajiriwa katika mwaka unaokuja. Kwa kweli ni mchango mkubwa sana ambao Serikali inaendelea kutambua nguvu kazi hii ambayo inakwenda kutumikia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kuunga mkono Wizara hii na kazi ambayo inaifanya. Ninapendekeza mambo machache. Jambo la kwanza, katika kupitia tumeona kuna vitengo vingi sana, lakini ningependa kupendekeza kwamba mahitaji ya vijana yanabadilika muda hadi muda, hivyo kuwepo na kitengo cha utafiti na ubunifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya vijana yanabadilika sana, na vilevile vijana wetu ni wabunifu na wana talanta mbalimbali. Kuwe na kitengo ambacho kitatengewa fedha ili tuweze kutambua mahitaji ya vijana kadiri muda unavyokwenda, na pia umri wao unavyobadilika na mahitaji yao kutoka eneo hadi eneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo hiki pia kitatambua namna ya rasilimali fedha inayotengwa itakavyogawanywa. Mahitaji ya kijana wa Ilala ni tofauti na mahitaji ya kijana wa Nkasi na mahitaji ya kijana wa Nkasi ni tofauti na mahitaji ya kijana wa Mbulu. Kwa hiyo, tuweze kuona tusije tukaweka kwenye kapu moja, tuone namna ambavyo tutatambua mahitaji yao na kitakachotusaidia ni utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua umri unawatofautisha, lakini pia jiografia inaweka tofauti ya mahitaji, elimu walizonazo pia inaweka tofauti ya mahitaji yao, na pia hata na jinsia. Kwa hiyo, ningependekeza kuwe na kitengo hicho na kitengewe fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vijana kwa kuwa wana nguvu, wana uwezo na wana maarifa, lakini wana upungufu, tunahitaji kuwajengea uwezo; lakini je, tunahitaji kuwasikiliza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Waziri, ameanzisha vijana platforms. Ninaomba zile vijana platforms ziende mpaka ngazi ya kata. Zikifanyika katika ngazi ya halmashauri, changamoto ni kwamba wapo vijana ambao hawawezi kufika, ama kwa sababu ya miundombinu, ama kwa sababu ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mpaka ngazi ya kata, tuwasikilize vijana hawa, wana mawazo, wana maoni, wana ujuzi, wana vitu vyao, tuwasikilize ili tuweze kuwagawanyia fursa kulingana na mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, pamoja na hayo, tunajua kwamba ili kutengeneza fursa za ajira, tunahitaji kutazama mambo kadha wa kadha. Moja ni mafunzo ya ujuzi kwa vijana wetu. Hawa vijana wapo makundi mengi sana. Wapo wenye elimu ya darasa la saba, wasio nayo, wenye Form Four, wenye Diploma, wenye Degree na wana mahitaji ya ajira pamoja na fursa za uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutazame kwa kuhakikisha kwamba tunatengeneza mwongozo wa mafunzo ambao utawakamata vijana wote hawa ambao utakwenda kuwasaidia kuwapa ujuzi na kuwapa maarifa kulingana na sekta zao na eneo ambalo wanafanyia kazi au eneo ambalo wanahitaji kujiendeleza. Kwa hiyo, tunaweza tukaandaa short courses au short contents ambazo zitawasaidia vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba suala la ujasiriamali na kuwajumuisha vijana katika maeneo yale ya upatikanaji wa fedha. Tunajua kuna elimu tofauti, tunajua kwamba wanahitaji mitaji, lakini ninaomba tuwe na mwongozo wa kuwasaidia vijana hawa katika eneo hili la ujasiriamali, na kuwajumuisha katika upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kujiendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja, tunahitaji mazingira wezeshi kwa ajili ya kuwawezesha vijana wetu. Kwa mfano, bodaboda tumewapa vijana, na tumewakopesha katika zile 10% na wapo watakaokuja kukopa, lakini vilevile wengine watakwenda kwenye kilimo. Wanapopita barabarani, kuna changamoto za kuadhibiwa kwa sera fulani fulani hasa za kukamatwa na kupigwa faini, na wanapopigwa faini tunawarudisha nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria kwa mfano kijana ambaye anabeba gunia moja, anachajiwa labda shilingi 20,000 au 30,000 ya faini njiani. Tayari umeshamfilisi; iwe ni bodaboda, iwe anafanya shughuli za ujasiriamali katika kilimo. Kwa hiyo, tuone sera zetu na mazingira yetu yawe wezeshi kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna taasisi ambazo zinaajiri, tuone namna ambavyo tunaweka incentives; iwe ni tax incentives kwa zile taasisi ambazo zitaajiri vijana, iwe pia ni kwa kupata access to the capital incentives, tuweze kuona namna ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie mambo mawili ya mwisho. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, tumepata shilingi bilioni 200 na tunashukuru kwamba vijana wengine wamependekeza kuwa na benki, Wizara itazame, lakini ninapendekeza namna ambavyo fedha hizi zitawafikia vijana, tuone routs ziwe tofauti tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona ile cheque wakati inakabidhiwa inakwenda CRDB Bank, lakini tuone benki ambazo zipo katika halmashauri zetu ziweze kutoa fursa ili vijana wetu waweze kupata hizi fedha katika maeneo wanapoishi bila kuingia gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuishauri Serikali katika eneo moja. Eneo lingine ni suala la kuweza kutengeneza mazingira ya vijana kutimiza masharti.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa hawana NIDA, wala hawana leseni ya biashara. Katika ngazi za halmashauri na ngazi ya kata tuone namna ya kuwa na ofisi moja ambayo itawahudumia vijana hawa kwa wakati, na pia kwa urahisi ili kuweza kutimiza masharti ya mikopo na kuweza ku-access hizi fursa ambazo tunazitengeneza kupitia Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai, hadi kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo kwa mpango mzuri ambao amewasilisha kwa ajili ya maendeleo ya kilimo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kilimo ni mama na baba wa Wizara zote; kwa sababu katika kilimo tuna ajira, tunapata nishati, biashara, afya, maana madawa yote nayo yanatokana na mimea, lakini vilevile katika kilimo tunapata lishe pamoja na chakula. Kwa maana ya ajira, tunaona zaidi ya 80% ya wananchi wetu wanapata ajira kupitia sekta hii ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kusema mambo mawili; la kwanza, hii Wizara ni Wizara ya kimkakati kama ilivyo Wizara za Uchukuzi na Nishati. Ningeomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe anaongea na hawa, kwa sababu tunapojenga SGR, tunapoboresha bandari, ni lazima tuhakikishe kwamba bidhaa zitakazopita katika barabara, katika SGR na bandarini ziwe ni bidhaa zinazotokana na kilimo chetu. Kwa hiyo hii Wizara ni Wizara muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, ninapenda kuishauri Serikali kwamba, bajeti ya upande wa umwagiliaji itoke nje ya bajeti ya kawaida kwa sababu ni eneo la kimkakati. Vilevile, eneo la uzalishaji wa mbolea, tunaona uzalishaji upatikanaji wa mbolea ni kiasi cha 83% ambacho si kiwango kinachotakiwa; lakini bado zaidi ya 60% inatoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajua kwamba kule duniani tuna mgogoro wa kivita kati ya nchi nyingine; hivyo kutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa mbolea katika mwaka unaokuja kama ambavyo tunaona kwenye mafuta. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara iweze kuweka mpango mkakati wa mapema wa kuhakikisha kwamba mbolea zitaendelea kupatikana katika msimu unaokuja kwa ajili ya kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande pia wa uzalishaji wa mbegu, bado pia mbegu zetu haziwi za kutosha. Ningeomba Wizara nayo itenge fedha maalum kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu. Moja ya eneo ambalo ninapenda kuchangia, amechangia Mheshimiwa Mbunge mmoja; tuna tatizo la uwepo wa mbegu feki katika majira yale ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaumiza sana mkulima pale ambapo ananunua mbegu 15,000 au elfu kumi na ngapi, anapokwenda kupanda acre zote zinakuwa haziwezi kuota. Lazima udhibiti uwepo na namna ya pekee ni kuongeza uzalishaji wetu wa ndani kwa upande wa mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande pia wa mbolea, tunajua kwamba mbolea ambayo tunayo hapa nchini bado katika nyakati za kilimo kuna wafanyabiashara wachache wanatumia zile fursa. Ninaishauri Serikali kwamba, wale wauzaji na wale mawakala wawe wanaweka bei za mbegu na bei za mbolea kwenye milango, ili mkulima anapofika aone kabisa haitaji kuuliza na iwe ya wazi. Hii itajenga uwazi katika kupata mbolea, lakini pia mbegu kwa bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kwenye eneo la mazao machache. Zao moja ni dengu ambalo liko kwenye stakabadhi ghalani. Hakika imekuwa changamoto kwa wakulima wengi. Kwanza, hawapati mbegu nzuri, wanatumia zile zile ambazo walipanda mwaka jana; lakini pili, masoko yao si ya hakika kwa sababu maghala yako machache sana na wakulima hutumia umbali mrefu sana kusafirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na ninashauri tuweke soko huria, lakini hao wanaonunua miongoni mwa wakulima waishie kwenye sehemu ya stakabadhi ghalani. Tusitengeneze mazingira ya changamoto kwa wakulima wetu ambao wengi ni wadogo wadogo na wengi wanatumia gharama kubwa sana. Ninaomba tutengeneze soko huria kwenye eneo hilo. Wale wanaotaka kuuza kwa mfumo wa uhuru wauze lakini wote waishie kwenye stakabadhi ghalani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia kwenye eneo la zao la vitunguu maji pamoja na karoti ambalo bado ni changamoto, wengi wanauza kwa mfumo wa lumbesa. Hata leo ukienda kwenye soko la mazao haya kwenye mkoa wowote, bado lumbesa ni changamoto. Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo, ninaomba Mheshimiwa Waziri wetu alisimamie hili kikamilifu ili wakulima wapate faida ya mazao yao wanayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la mahindi ambalo hakika linalimwa sana katika mkoa wangu na katika jimbo langu ambalo ninaliongoza; mahindi mwaka huu tumepata bahati na tunaona tutapata mazao ya kutosha. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu. Tunaomba Serikali itusaidie kupitia NFRA, kwanza kuweza kutoa bei nzuri ili kuwasaidia wakulima ambao wamenunua mbegu na pia wamenunua mbolea. Vilevile, kufungua mipaka mapema ili tupate bei nzuri ambayo itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la mwisho ni eneo la umwagiliaji. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia, tumepata skimu tatu, tumepata mabwawa mawili. Ninaomba Serikali iweze kukamilisha mradi huu. Tumepata pia visima sita katika kata zetu na zitaenda kusaidia kuongeza wigo wa kilimo cha umwagiliaji ambacho ni kilimo cha hakika sana. Nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa ajili ya mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ni eneo la mradi wa BBT. Tunaomba BBT ishuke katika halmashauri ambako ndiko vijana wako na ndiko mashamba yaliko. Tushushe chini ili vijana wengi wakajiajiri kule ili waweze kuzalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumze kwamba, kilimo bila vifaa na teknolojia haiwezekani. Matrekta na power tiller tunashukuru tumesikia kwamba yatakuwepo na yatakopeshwa. Masharti yawe nafuu na yaweze kusambazwa hasa katika maeneo ya vijijini ambako ndiko wakulima waliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kukushukuru sana na kusema ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa mia. (Makofi)
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa nafasi na afya njema kuweza kuwepo leo na kuweza kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu. Pia, ninapenda kutoa shukrani kwa wanananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini ambao wamenipa kura za ndiyo, na kumpa Mheshimiwa Rais Samia kura za kutosha asilimia kubwa sana. Ninapenda kuwapa shukrani za dhati na kwamba nipo hapa tayari kwa ajili ya kuwawakilisha katika miaka mitano ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge letu tarehe 14 Novemba, 2025, ambayo tunaendelea kuichangia au kuitolea maoni mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunajua kwamba Mheshimiwa Rais wetu, kipenzi chetu na mama yetu ambaye ni hodari sana amesherehekea siku ya kuzaliwa kwake na amesema leo ni 27 ya kijani. Ninaomba tuendelee kumuunga mkono kuhakikisha kwamba tunashiriki zoezi la upandaji miti ambalo linakwenda kuboresha mazingira katika maeneo yetu tunayoishi na tuwape hamasa wananchi wetu ambao tunawawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa ustahimilivu wake, ujasiri wake na ushupavu wake kuipitisha nchi yetu katika kipindi kigumu cha misukosuko na leo ikiwa tulivu hasa kwa kadhia iliyotokea tarehe 29 na tarehe zilizofuata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tumeona katika hotuba yake upendo wa kweli na ujasiri wa kweli na ustahimilivu wa kweli hasa kwa kuhakikisha kwamba anaendelea kutambua walioathirika kwa kuwapa pole, na vilevile kuwaalika katika azma nzima ya kuja pamoja kama Watanzania kwa njia ya maridhianno na kuendelea kuongea kwa pamoja na kutatua changamoto zetu kwa njia ya majadiliano. Hii ni tunu muhimu sana kulindwa hasa kama jamii moja ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Uchunguzi, na pengine tuendelee kusubiri majibu yake ili tuweze kuyapokea yale yatokanayo na kuendelea kujenga nchi yetu kwa mustakabali wa kizazi chetu cha sasa na kinachofuata.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa ahadi zake alizozitoa na ambazo ameshaanza kuzitekeleza. Tunaona leo Bima ya Afya kwa Wote inaanza na hasa tunaona upendo wa Rais kwa kuyazingatia makundi ambayo yako kwenye hatari ya kukosa matibabu wakati wanapougua kutokana na changamoto ya kiuchumi hasa wazee wetu wa miaka 60 kwenda juu, watoto wadogo na wakinamama wajawazito ambao tumeona wanaathirika kwa vifo vingi pamoja na wale watoto wachanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo bado nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameifanya na uwekezaji mkubwa ambao ameweka kwenye sekta ya afya kwa kuhakikisha kwamba vifo vya wakinamama wajawazito vimepungua zaidi kwa asilimia kubwa sana na vifo vya watoto wachanga na bima ya afya inaendelea kupunguza tatizo hili katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi mikopo kwa wajasiriamali na hii tayari ameshaanza kuitekeleza kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 10.5. Hii imeendelea kuwa ni hatua kubwa na muhimu ya Mheshimiwa Rais kutekeleza ahadi zake alizoahidi kwa Watanzania wakati wa uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii mikopo ya wajasiriamali ambayo ameitoa kupitia benki mbalimbali imekwenda kuwazingatia wazee/wakinababa wengi ambao wamekuwa wakilalamika katika mikutano yetu mbalimbali kwamba mbona vijana na wakinamama wamepewa kipaumbele? Je, wazee wanazingatiwa wapi? Ninaona hii mikopo imewakumbuka. Kwa hiyo, tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ameleta hoja hii na amewazingatia wazee wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia kwa ajira ambazo amezitoa kwa walimu na watumishi wa sekta ya afya. Tunaamini elimu yetu itaimarika. Pia, huduma za afya zitakwenda kuimarika katika maeneo ya vituo vyetu vya afya, zahanati, hospitali zetu za wilaya, hospitali za mikoa na za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niweze kuchangia kwenye sekta ya kilimo kwa uchache. Sekta yetu ya kilimo ni sekta muhimu sana na ni sekta ambayo inatulisha Watanzania wengi lakini pia imeajiri Watanzania wengi. Tunashukuru Mheshimiwa Rais amesema kilimo ni uwekezaji na ni biashara kama biashara nyingine. Maana yake ipate msukumo wa pekee hasa katika kuitengea bajeti na vilevile katika kuiwekea utaalamu wa kutosha ili wananchi waweze kufaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha umwagiliaji Mheshimiwa Rais amekizungumzia kwamba ataenda kuongeza ekari za kilimo cha umwagiliaji kutoka 3.46 milioni hadi milioni sita. Hii ni hatua kubwa sana na itakwenda kuajiri vijana wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ninapenda kushukuru kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini. Tumepata visima sita ambavyo vimechimbwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakwenda kuajiri wakulima katika zaidi ya ekari 300, lakini vilevile tumepata bwawa kubwa ambalo litakwenda kuwasaidia wakulima wa kilimo cha umwagiliaji kwa vitunguu maji, vitunguu saumu, mahindi na mazao mengine na itakwenda kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda pamoja na kuajiri vijana walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la kilimo tunaona Rais amesisitiza umuhimu wa uwepo wa mikopo kwa ajili ya wakulima. Tuna Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo na pia tuna Benki ya Ushirika. Kwa hili kwa kweli tunaipongeza Serikali, lakini tuna maombi hapa kwamba benki hizi zishuke kwa wakulima ambao wengi wako vijijini na ziweze kuwafikia. Hizi benki bado ziko mijini hazijawafikia wakulima walio wengi na hasa wale walio katika maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia, tumepata ruzuku kwenye maeneo ya mbolea, lakini pia na mbegu. Bado maeneo mengi yamepata kwa bei nzuri sana hasa ile elekezi ya Serikali, lakini tunajua bado tunao wauzaji wa mbegu hizi na wauzaji wa mbolea ambao bado wanaihujumu Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba usimamizi uendelee kuimarishwa ili kuhakikisha kwamba ruzuku ambayo Serikali imeweka kwenye mbolea na mbegu inaweza kuwafikia wakulima bila kuibiwa hasa na matajiri ambao wana tamaa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba katika eneo hili la kilimo Serikali hasa Wizara yetu ya Kilimo iendelee kuboresha uwekezaji katika eneo la kuongeza thamani katika mazao ambayo wakulima wetu wanazalisha ili tuzalishe ajira na bidhaa ambazo zinaweza kwenda kuuzwa na zikaweza kuongeza ajira, kutengeneza malighafi kwa ajili ya viwanda, vilevile kuongeza kipato kwa wakulima wetu, lakini pia kuongeza kodi kwa ajili ya Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachangia eneo la mifugo kwa ufupi sana. Tunajua kwamba nayo ni sekta muhimu sana na wananchi wangu wa Jimbo la Mbulu Vijijini ni wakulima na wafugaji. Mwaka jana, 2025 mwishoni tulipata adha kubwa sana kwa wafugaji wengi sana kupoteza mifugo hasa kutokana na ukame, vilevile magonjwa yatokanayo na kupe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kusema kwamba Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ameelekeza kwamba tuendelee kujenga kuelekea katika ufugaji wa kisasa ambao unakwenda kusaidia katika uongezaji wa eneo la ufugaji na vilevile kuhakikisha maji yanapatikana kwa ajili ya mifugo. Pia, kuhakikisha kuna majosho ya kutosha katika maeneo ya ufugaji na chanjo kupatikana. Vilevile, kuhakikisha tunakuwa na mifugo iliyo bora ambayo inafugwa na wafugaji wetu ili iwe na tija hasa kwa ajili ya soko la ndani na soko la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua yako maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya wafugaji, lakini yapo maeneo ambayo hayatajatengwa. Yale maeneo ambayo yametengwa, tunaomba Serikali iweze kusaidia sasa kuweka miundombinu muhimu hasa majosho, pia, kuhakikisha supplies mbalimbali kwa ajili ya kusafisha ng’ombe, kuchanja ng’ombe na kuwapa utaalam unaofaa ili tuweze kupata mazao yaliyo bora hasa katika eneo hili la mifugo. Vilevile, wafugaji wakumbukwe katika eneo la mikopo kwa sababu ni wazalishaji muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niende kwenye eneo la barabara. Ninashukuru sana kwamba Mheshimiwa Rais amezungumza katika hotuba yake na ametoa dhamira ya kweli na hakika kwamba kuna haja ya kuongeza bajeti katika eneo la barabara hasa kwenye TARURA. Vilevile, ninaomba na TANROADS nayo ikumbukwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ni miundombinu muhimu sana hasa katika maendeleo kwa sekta zote na kwa maeneo ya vijijini, wakulima, wafugaji na wajasiriamali hawawezi kuzalisha na kufikisha mazao yao katika masoko bila kuwa na barabara iliyo imara, nzuri na inayopitika majira yote ya mvua na masika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba bajeti ya eneo hili iongezwe na hasa katika jimbo langu. Ninaomba sana ile barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mbulu – Garbabi (kilometa 25), Labay – Haydom (kilometa 25), lakini vilevile kutoka Dareda – Dongobesh, Haydom – Mogitu na Haydom – Singida. Hii ni miundombinu muhimu sana kuunganisha mikoa na wilaya na wananchi wetu watakwenda kufaidi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa upande wa umeme tumepata vitongoji 9,000 na jimbo langu limepata vitongoji 59 na vingine vinaendelea kupata kwa kuwa uhitaji ni mkubwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha, malizia.
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana. Ninapenda kukushukuru wewe na ninashukuru kwa hotuba nzuri ya Mheshimiwa Rais, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. Awali ya yote, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kuwezesha Wizara yetu ya Maji kupata bajeti nzuri ili kuweza kutekeleza miradi ya maji. Vilevile, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika kuhakikisha kwamba tunamtua mama ndoo na tunawatua ndoo Watanzania wa maeneo ya vijijini na mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumpongeza pia Meneja wangu wa RUWASA mkoa, lakini pia na wilaya kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini wanapata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuipongeza Wizara kwa maono ambayo hasa yametokana na Mheshimiwa Rais ya kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji. Katika hili tuna uhakika kwamba mahitaji yetu ya maji, ambayo ni takribani cubic meter bilioni 42 ambayo ni sawa na 37% ya maji safi na salama yaliyoko chini ya ardhi, lakini pia na juu ya uso wa ardhi; ambayo kwa kweli tuna uwezo isipokuwa tunachohitaji ni miundombinu na hasa usambazaji na kikubwa ikiwa ni bajeti lakini pia na mpango. Kwa hiyo, ninaomba niitie moyo Wizara kushikilia jambo hili na kulitekeleza kikamilifu. Hata kama itachukua miaka ya kutosha, lakini tuweze kuiona ikitekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishukuru Wizara kwa miradi ya maji ambayo imeweza kuletwa katika Jimbo la Mbulu Vijijini, lakini miradi mingi bado haijakamilika. Niiombe Wizara ikamilishe miradi hii. Hasa nitangulize kwa kutaja Mradi wa Dambia ambao utahudumia vijiji 21. Mheshimiwa Waziri ametutengea 500,000,000 lakini hadi sasa mkandarasi anadai takribani bilioni 1.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nilitamani nishike shilingi yake, ila kwa kuwa ameongeza bajeti ninaomba nisiishike shilingi yake wala mshahara wake. Ninaomba akamilishe lile deni, tupate na bilioni hizo ili mradi ule uweze kukamilika kwa ajili ya kuhudumia Kata za Bashay, Endamilay, Eshkesh, Dongobesh na Idachini, zikiwa ni vijiji 21. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nipende kushukuru pia Vijiji vya Laghangesh, Mangisa, Getesh, Esqaroda, Gitultaqao; lakini pia Multuru, Diomat na Endagao vitapata maji. Kwa kweli nipende kuleta shukurani za dhati kutoka wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ipeleke fedha hizi ili miradi hii iweze kukamilika na wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilete maombi machache kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini. Tuna Kata ya Masyeda ambayo ina Kijiji cha Endanyawish. Ni kijiji kikubwa sana ambacho kina wakulima na wafugaji. Tumechimba takribani visima vitano lakini havina maji. Ninaomba Mheshimiwa Waziri aitazame kata hii na kijiji hiki ili kiweze kupata maji. Tuna maji katika Bonde la Endagichan ambayo ni kata, tunaweza tukayachimba na kupeleka kule. Ninaomba nilete ombi hilo rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mji wa Dongobesh ambayo ni makao makuu ya halmashauri tuna maji ambayo ni machafu kutokana na kutokuwa na chujio na pia bado hayatoshelezi mahitaji ya mji. Niiombe Wizara itusaidie bajeti ili tuweze kupata chujio ili wananchi takribani 20,000 wanaokaa katika Mji wa Dongobesh wapate maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru pia Wizara kwa kukubali kuongeza upatikanaji wa maji kwenye mji huu kwa kuleta maji kutoka Mradi wa Dambia na hivyo ninaamini ndani ya miezi mitatu ijayo wananchi wa Dongobesh wataweza kushukuru kupata maji na kubaki salama katika mji huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kata ya Maghan ambayo ina chanzo cha maji kilichochimbwa mwaka 1975, wakati huo ikiwa na wakazi kama 500, leo tuna wakazi 15,000 na bado inategemea chanzo hiko kimoja. Niombe tuweze kupata chanzo kingine. Kwa bahati nzuri kata hii ina bonde zuri sana ambalo lina maji mengi. Tukipata visima viwili tayari wananchi hawa ambao ni takribani 15,000 watakuwa wamepata maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi ya mabwawa. Jimbo langu hili lina takribani kata tano, ambazo Mheshimiwa Waziri akitutengea bajeti maeneo yapo ya kuchimba mabwawa na kuyatengeneza ili wananchi waweze kupata maji. Ninaomba Kata za Masqaroda, Maghang, Gidhim, Eshkesh, Haydom, Masonyagwe, Labay, pamoja na Basoderer wachimbiwe mabwawa ili wapate maji safi na salama kwa ajili ya nyumbani na mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru sana na ninaomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwa ajili ya wananchi wetu kupata maji safi na salama. Ahsanteni sana. (Makofi)