MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Mariam anaishukuru Serikali kwa kujengwa kwa Uwanja huu wa Mkapa ambao unabeba watu wengi kwenye mechi mbalimbali zikiwemo mechi za Simba na Yanga na hivyo kuingiza mapato makubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kugawa sehemu ya mapato haya na kuyaelekeza kwenye huduma za jamii katika Jimbo la Temeke? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Uwanja wa Mkapa na Uhuru unafanyiwa huduma mbalimbali ikiwemo kutengeneza bustani pamoja na usafi, lakini pamoja na huduma nyingine. Nini mpango wa Serikali kuwapa kazi hizi vijana wa Temeke wakiwemo vijana wenye ulemavu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Stella Ikupa, kwa niaba ya Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Temeke ambaye anafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuwapigania wananchi wa Temeke na ninamwombea Mungu aendelee kumtia nguvu na amtie moyo kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa Temeke wanapata kile ambacho walitarajia wakati wanamtuma kuwa Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu maswali haya mawili mazuri ya nyongeza la kwanza lilikuwa kuhusiana na mgao. Mara nyingi Serikali haiandai matukio yanayofanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, yenyewe inatoa miundombinu hii kwa waandaaji ambao kwa mfano mechi za Simba na Yanga timu mwenyeji ndiyo ambayo inakuwa inakodishwa uwanja huu. Mapato yanayopatikana hugawanywa kwa utaratibu maalum ambao umekubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 18% ya mapato hayo inakwenda kwama kodi ya ongezeko la thamani, asilimia tatu inakwenda kwa BMT, asilimia Nne inakwenda kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, 15% inakwenda kama gharama za ukodishaji wa uwanja na asilimia Saba kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli ile na asilimia Sita inakwenda kwa Chama cha Soka cha Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wote hawa moja ya mambo wanayoyafanya ni kuhakikisha wanarudisha kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazofanyika Tanzania na hasa kwa Manispaa ya Temeke ambayo uwanja huu umewekwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachofanya kwa sasa ni kuhakikisha tunaendelea kuimarisha makusanyo haya ili kiwango ambacho kinagawiwa kwa wadau hawa ambao nao hurudisha kwa Manispaa ya Temeke na maeneo mengine mbalimbali kwa ajili ya huduma hasa za michezo kinaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasimamia utaratibu wa kuhakikisha tunaendelea kukusanya mapato haya ili yawe na manufaa na tija kubwa zaidi kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwenye swali lake la pili, kuhusiana na huduma mbalimbali. Katika hili Serikali imetoa zabuni kwa makampuni ambayo yanatoa huduma mbalimbali zinazofanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa wakati wa matukio yanayotokea pale. Tumetoa zabuni kwa makampuni ya ulinzi na makampuni ya usafi hali kadhalika. Kampuni za ulinzi tunao walinzi 25 pale, lakini tunao vijana 40 ambao wanafanya shughuli za usafi na wote hawa ni wakazi wa Manispaa ya Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kuhusiana na kutenga kwa ajili ya watu wenye ulemavu moja kwa moja, hili ni wazo zuri na ninaomba nilichukue kwa ajili ya mashauriano na wenzangu kuona kama miongoni mwa vikundi vya wajasiriamali ambapo sasa hivi tunavyo vikundi vinne pale, kila kimoja kikiwa na wanachama 50, tuone kama tunaweza kutenga vikundi ambavyo vitakuwa vya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali panapokuwa na matukio kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. (Makofi)
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kutokana na changamoto ya kupasuka kwa mabomba, changamoto ambayo inasababisha upotevu wa maji, Serikali inaonaje ikaanzisha namba maalumu ya kuripoti changamoto hiyo? Kwa sababu mara nyingi mimi nimekuta maji yanamwagika na ukiuliza wahusika wanasema hawajui mahali pa kuripoti. La kwangu ni hilo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella Ikupa unaweza ukarudia swali lako na Waheshimiwa Wabunge tunaomba tupunguze sauti ili muuliza swali na mjibu swali waweze kusikilizana.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya kupasuka kwa mabomba, changamoto ambayo inapelekea upotevu wa maji, Serikali inaonaje ikaanzisha namba maalumu kwa ajili ya kuripoti changamoto hiyo inapotokea? Kwa sababu kuna maeneo ukipita ukakuta maji yanamwagika kutokana na kwamba bomba limepasuka ukiuliza wahusika wanasema kwamba hawajui wanaripoti wapi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni swali muhimu sana na linajenga msingi imara wa ushirikishwaji wa wananchi pale wanapoona kuna miundombinu imepata changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tayari tuna hizo namba isipokuwa naona kwamba tutabadilisha namna ya kuhakikisha kwamba namba hizi zinafahamika kwa wananchi. Lengo ni kwamba tuweze kushirikiana kutoa taarifa pale ambapo mabomba yanakuwa yamepasuka na kuweza kuokoa maji yanayopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea ushauri wa Mheshimiwa Stella na kwa umuhimu wake, ahsante sana.