Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Catherine Canute Joachim (2 total)

MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuendeleza utalii wa tiba nchini ili kuboresha huduma za afya na kuongeza mchango wa sekta ya afya katika pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Joachim, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza utalii wa tiba nchini Serikali inatekeleza mpango wa uboreshaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi wenye vipaumbele vifuatavyo; uboreshaji wa miundombinu kwa kujenga mipya na kukarabati iliyochakaa, kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa (PET/CT Scan, Angio Suite, Cathlab na CT Scan), kuwajengea uwezo watumishi katika utoaji wa huduma kwa kuwaendeleza kitaaluma, kuanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi, kuziwezesha hospitali zetu kupata ithibati za kimataifa na kuzitangaza huduma zinazotolewa na hospitali hizo nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Februari, 2026 jumla ya wagonjwa 3,018 raia wa kigeni walipatiwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali za Rufaa za Mkoa, Kanda, Hospitali Maalum Taifa, hivyo kuongeza mchango wa sekta ya afya katika ukuzaji wa pato la Taifa. Aidha, Serikali imetoa ufadhili wa masomo wa Samia Health Super-Specialization Program ambapo jumla ya wataalam 1,483 wanafadhiliwa kusomea fani za ubingwa na ubingwa bobezi katika nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM aliuliza: -

Je, Serikali imepata matokeo gani katika kupunguza uchafuzi wa mazingira tangu kuanza kwa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki mwaka 2019?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Catherine Canute Joachim, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto za uchafuzi wa taka za plastiki na athari zake, Serikali ilipiga marufuku uingizaji nchini, uzalishaji, usambazaji, uhifadhi, usafirishaji nje ya nchi na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia tarehe 01 Juni, 2019. Matokeo ya katazo hilo ni pamoja na:-

(i) Kupungua kwa zaidi ya 95% ya uzalishaji na uingizaji wa mifuko ya plastiki nchini, ambapo imechangia kupungua kwa uzalishaji wa taka za plastiki katika maeneo mbalimbali nchini;

(ii) Kuongezeka kwa kiwango cha uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya plastiki kutoka chini ya 40% mwaka 2018 hadi kufikia zaidi ya 85% mwaka 2026;

(iii) Kupungua kwa takribani 60% ya taka za plastiki katika maeneo ya fukwe za bahari na maziwa ambapo hatua hii imepunguza hatari kwa viumbe wa majini;

(iv) Kupungua kwa gharama za kuzibua mitaro ya maji machafu kwa wastani wa 30% mpaka 40%, kwani mifuko ya plastiki ilikuwa chanzo kikuu cha uzibaji wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu ninaomba nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuzingatia katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki la mwaka 2019 kwa ajili ya kulinda afya na kuhifadhi mazingira yetu kwa maendeleo endelevu ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.