MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuendeleza tiba ya utalii, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo imepanga ifikapo mwaka 2050 pato la Taifa linatarajiwa kuwa dola trilioni moja na inatarajiwa kuwa sekta binafsi itakwenda kuchangia 70%, swali langu ninataka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha hospitali za sekta binafsi zinashiriki vipi katika kuchangia pato la Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tunafahamu kwamba nchi ambazo zimefanya vizuri katika utalii wa tiba kama vile Afrika Kusini, India, Morocco na Thailand zimefungamanisha utalii wa tiba na talii nyingine kama vile utaii wa fukwe za bahari, utalii wa tiba mbadala kama wellness program au AUVEDC nilikuwa ninataka kufahamu nini mkakati wa Serikali wa kufungamanisha utalii wa tiba hapa nchini na utalii mwingine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Dkt. Catherine Joachim kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi, lakini kipekee jumuiya yake anayoiwakilisha Jumuiya ya Wazazi Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya afya ambao huo ndiyo umevutia utalii wa tiba na si hivyo tu, tumemsikia Mheshimiwa Rais ameelekeza ipitiwe sera ya PPP ili tuweze kufanya kazi vizuri na sekta binafsi kwa sababu ndiyo ambayo itakwenda kuchangia pato la Taifa kwa 70%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoendelea kutekeleza tiba utalii tunafanya kazi kwa sasa na hospitali saba na kati ya hizo hospitali tano ni za Serikali, lakini tunafanya kazi na hospitali binafsi mbili. Kwa hiyo, Serikali inafanya kazi na hizo hospitali binafsi tayari, tunayo timu ya kitaifa inayoratibu tiba utalii nchini, timu hii imeunganisha sekta zote, kama tunavyofahamu utalii ni suala mtambuka, mtalii anapofika kwanza anahitaji viza, anahitaji asafiri kwa hiyo, Wizara zote zinahusika na tunafanya kazi na Wizara zote kuhakikisha kwamba watalii hawa wanaweza kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tumeshaandaa mwongozo na sasa tupo tunaandika mkakati na upo mbioni kukamilika, mkakati ambao utakwenda kuweka mazingira rafiki sana kwa sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sekta binafsi, mazingira wezeshi tayari yameshawekwa na Awamu ya Sita kwa kuweka miundombinu mizuri, kwa kuweka vifaa vizuri na kuwasomesha Watanzania ambao wanaweza kutoa hizo huduma bobezi. Hivyo, ni jukumu la Watanzania kuchangamkia fursa hii ya kufanya kazi hii ya utalii tiba na sisi tupo kwa ajili ya kuwaratibu na kuwawezesha ili waweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake namba mbili, zipo nchi zinazofanya vizuri, ni kweli kabisa, Singapore, Thailand, India wanafanya vizuri na sisi kama Serikali tunaendelea kujifunza kutoka kwenye nchi hizo. Ni hivi karibuni wataalam kutoka Misri walifika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kwa mara ya kwanza walifanya operation kubwa ya mshipa mkubwa wa moyo kwa maana ya aorta.
Kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri. Hata hivyo madaktari wetu wameendelea kufanya kambi za tiba katika nchi mbalimbali ili kuendelea kujifunza na kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na taasisi zote ili ku-brand. Ili ufanye vizuri katika utalii lazima ujitangaze, unatangazaje? Kwa kwenda na kuhusisha hizo nchi mbalimbali. Katika mkakati huo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kufungamanisha, ndiyo maana umeona tunafanya kazi na Maliasili kupitia Bodi ya Utalii, ndiyo maana unaona sasa hivi ukipanda SGR pamoja na kutangaza mbuga unatangaziwa pia hospitali zetu, unatangaziwa vifaa vyetu, unatangaziwa huduma tunazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakwenda kufungamanisha huduma zetu na tunakwenda kushirikiana na nchi zilizofanya vizuri zaidi ili na sisi tuweze kufanya vizuri katika utalii tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DKT. CATHERINE C. JOACHIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuainisha mafanikio ambayo yamepatikana katika udhibiti wa taka za plastiki. Nina maswali mawili ya nyongeza ambayo yatajikita katika eneo namba nne, lililosemwa na Mheshimiwa Naibu Waziri, kuhusiana na gharama za kupunguza udhibiti wa taka za plastiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza. Kwa kuwa miundombinu ya kukusanyia takataka pamoja na vile vituo vya urejelezaji wa taka za plastiki ni vichache, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza miundombinu hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili litajikita katika ongezeko la viwanda, ambalo tumeona linakwenda sambamba na ongezeko la vifungashio vya plastiki pamoja na chupa ambazo hutumika mara moja. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko hili la vifungashio vinavyotumika mara moja bila kuathiri ukuaji wa viwanda hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Catherine Joachim, Mbunge anayetokana na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi. Ninatambua kwamba Jumuiya ya Wazazi moja ya kipaumbele chake ni kulinda na kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yake ya nyongeza ninaomba niyajibu yote kwa pamoja. Sheria yetu ya Mazingira Sura 191, tuliitungia kanuni Kifungu kile cha 230, kifungu cha 2(f). Kanuni zile ndiyo zilihusu haya makatazo ya matumizi ya mifuko ya plastiki na hususan vifungashio vya plastiki, kwa kutambua umuhimu wa sekta za kilimo ambazo zina mahitaji makubwa ya matumizi ya plastiki, vilevile sekta za ujenzi ambazo zina matumizi makubwa ya mahitaji ya plastiki, sekta za vyakula kwa maana ya vifungashio, viwandani kama alivyotangulia kusema Mheshimiwa Mbunge, lakini vilevile sekta za afya, pamoja na kwenye usimamizi wa taka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni zile ambazo tulizitunga chini ya kifungu hicho cha Sheria ya 230, ziliweza kuruhusu maeneo haya baadhi ya wazalishaji kupewa kibali kwa ajili ya kuzalisha plastiki hizo kwa matumizi hayo ambayo ni muhimu ndani ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho tumekifanya kama Serikali kwenye kanuni zile ambazo tumezitunga, tumeweka pia na wajibu wa wazalishaji wa plastiki hizo, wasafirishaji, wanaohifadhi, wanaosambaza na wanaotumia, tumewapa wajibu wa kuhakikisha pia wanashiriki kwenye kukusanya na kuteketeza taka hizo ambazo zinakuwa zimetokana na bidhaa ambazo wamehusika nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kuimarisha pia miundombinu ya ukusanyaji wa taka hizi. Sheria ile ambayo tuliitunga, Sheria ya Mazingira Sura 191 imezipa Mamlaka za Serikali za Mitaa jukumu la kusimamia taka ngumu. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, pia tunahakikisha pana miundombinu kila mahali, kwenye miji yetu na kwenye majiji yetu kwa ajili ya uhifadhi wa taka hizi ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.