Contributions by Hon. Fadhili Ally Liwaka (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema kubwa ya kuendelea kuwepo hapa tukiendelea kulijenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu pia kwa heshima kubwa na unyenyekevu, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kaka yangu Mheshimiwa Joel Nanauka. Mosi, kwa kazi nzuri aliyoanza nayo ya kuitumia Wizara hii ambayo ni mpya; na la pili, kwa uwasilishaji mzuri ambao umebeba mapana na maono makubwa kwa ajili ya vijana wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni mpya, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kuianzisha makusudi ili kuweza kulipa nguvu Taifa la vijana walio wengi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivi ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, anaweza asituone kwenye gari lake analopanda, anaweza asituone kwenye meza yake pale ofisini, anaweza asituone kwenye majukwaa mbalimbali ndani na nje ya nchi, lakini tunafikiri pamoja na yeye, tunawaza pamoja na yeye, tunaamua pamoja na yeye na tuongoza pamoja na yeye. Kwa lugha nyepesi, vijana wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuko pamoja naye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa ya vijana kuweza kulitumikia Taifa hili iliasisiwa tangu kuanzishwa kwa Taifa hili, lakini tumekuwa na vipindi kadhaa ambavyo tumekuwa tukiitazama fursa rasmi ya vijana kuweza kushiriki moja kwa moja kwenye kuleta matokeo chanya. Hii ni kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na dunia inavyokwenda sasa, na pia vijana wameongezeka, uhitaji umeongezeka, na tumekuwa na mahitaji makuwa ya kuingia kwenye maeneo mahususi ili kulijenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ni ukweli usiopingika kwamba hata kama tukiwa na nguvu ya kiasi gani, hatuwezi ku-satisfy mahitaji ya vijana kwenye soko la ajira tukawamaliza wote. Hiyo haiwezekani, lakini sisi kama nchi tunaweza kuwa na mipango mikakati na mwelekeo utakaowezesha vijana wetu kupata unafuu wa kuwa katika majukumu ya kila siku. Jambo hili ndilo dira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina makundi mbalimbali ya vijana, na mimi nimekuwa muumini ninayeamini kwamba ni lazima tukatae dhana ya kuamini kwamba liko kundi la vijana linahesabika kama bomu. Makundi yote ya vijana nchi hii ni fursa, makundi yote ya vijana nchi hii ni ya uzalishaji, makundi yote ya nchi hii ni tegemeo la Taifa kwenye usalama wa nchi, uzalishaji na mwelekeo wa free country. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makundi haya yote Serikali imedhamiria kuyaweka kwenye mwelekeo wa kuleta matokeo. Kundi la bodaboda tunalifikia, makundi ya machinga tunayafikia, makundi ya wachimbaji tunayafikia, makundi ya wakulima na wajasiriamali wote wenye ngazi ya ujana na kuelekea utu uzima kazi hii inafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba sisi tuko tayari kabisa kumsaidia na kumshauri. Tunamwombea kwa Wizara zote zilizoko nchini zimfungulie milango aingie kwenye kila Wizara anayotaka. Wizara hii ni kama mtoto wa mwisho ambaye anaita kaka kushoto; anageuka, dada kulia, anageuka; mama mbele, anageuka. Atakwenda Wizara ya Madini kuna fursa za vijana afunguliwe milango ili vijana wapate manufaa. Tunayo Wizara ya Kilimo, kuna irrigation schemes nyingi nchi hii, afunguliwe milango ili vijana wapate fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua ziko Wizara nyingi. Wizara ya Michezo ina wasanii, ina wacheza mpira, na ina wanamitindo. Hawa wote wako chini ya uratibu na usimamizi wa Wizara hii ya Maendeleo ya Vijana. Kwa hiyo, tuko hapa kuunga mkono Wizara hii, na pia kuondoa hofu kwa vijana, kwamba sasa wamepata mwarobanini wa masuala yao kuweza kujadiliwa kwa kina na kupatiwa utatuzi unaoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nishauri maeneo machache. Eneo la kwanza ni eneo la viwanda. Utakubaliana na mimi kwamba nchi zote duniani ziliweza kufanya mapinduzi ya viwanda vidogo na vikubwa, walisaidia sana kupunguza ombwe la vijana waliokosa ajira. Kwa wale ambao wanasafiri kwa barabara ya kusini kuelekea Mkoa wa Lindi, wataona unapopita Mkuranga pale kuna viwanda. Ukipita usiku, ukipita mchana utaona idadi ya watu wanaokwenda kiwandani kupishana ili kufanya shughuli za kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lile linawezekana, na Wizara hii ina nguvu ya kufanya hivyo. Sisi tunaamini, kwamba kwa uwezo wa Waziri aliyeteuliwa, maarifa yake, uweledi wake, exposure aliyonayo, hawezi kuchoka kutafuta namna ya vijana kuingia kwenye soko la ajira kupitia viwanda mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena eneo la pili katika ushauri, bado ninasisitiza eneo la kutazama juu ya kodi na mlolongo wa tozo nyingi katika shughuli za vijana. Vijana wanaoanza kutengeneza ujenzi wa Taifa hili wanaanza na mitaji midogo sana. Wanachohitaji wao ni fursa ya kufanya shughuli zao ili kufikia miradi mitaji mikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema kwenye Bunge hili, tupunguze baadhi ya tozo na baadhi ya kodi kwenye fursa za vijana kwenye ajira zao ikiwemo waendesha bodaboda. Tulishaomba na ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, alifanya kongamano kubwa ambalo lilikuwa na mgeni rasmi Mheshimiwa Waziri Mkuu. Vijana walileta hoja zao. Moja ya hoja kubwa waliyoleta ni pamoja na tozo hizi nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunao Wamachinga, bado ninaamini kwamba tunaweza kukusanya kidogo tukapata kingi na kila kijana akawa motivated kufanya kazi ya kiuchumi. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, tufanye mapitio vizuri kabisa ili kwenda kuona kundi lile la machinga tunapotaka kukusanya kutoka kwao, tunakusanya kwa namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hoja ya vitambulisho ilikuwa ni hoja nzuri na ilisaidia kupata kwa usahihi na kwa wingi, tuifikirie, lakini kama iko njia nyingine kupitia makundi na kupitia platform walizoziweka, basi ninamwomba Mheshimiwa Waziri, tushirikiane kwenye hili ili kuona fursa zao kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaelekea kumaliza mchango wangu. Sasa nchi hii imejengwa vizuri sana, na moja ya jambo kubwa ambalo watu wanalipigania ni siasa na maendeleo. Hata hivyo, na mtanisaidia, imekuwa tofauti kidogo. Wako wenzetu wengine wameichagua siasa kuyatia masikio ya vijana kauli zenye maumivu badala ya kauli zenye matumaini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo hapa kuwaomba vijana wa nchi hii, kwanza wawe na imani na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia. Pili, wajue kile tunachokifanya ni kwa ajili yao. Kwa bahati nzuri, niruhusu niseme kwa heshima kubwa sana, kwamba kaka yangu Mheshimiwa Ado Shaibu, yuko hapa ndani mtu ninayemheshimu sana, kwa sababu yupo kwenye chama kikubwa cha kisiasa chenye kusika ndani na nje, basi mimi na yeye na Wabunge wengine tusaidiane, tunapotoka nje kwenye platform zetu tuwaambie vijana juu ya kauli zinazoleta matumaini na siyo kuwalazimishia maumivu ambayo nchi haijachagua kuyafanya. Moja kati ya hayo, ni kutokuwatenga na mipango, sera na mwelekeo wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Spika, na mimi ninaungana na Wabunge wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema kubwa hii ya uzima, lakini ninatumia fursa hii adhimu sana kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, leo tuko hapa kama Taifa tukiwa na matumaini makubwa wakati ambapo Bunge letu linakwenda kupitisha bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa unyenyekevu mkubwa sana na heshima kubwa, kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiyo amekuwa askari wa mstari wa mbele mwenye kupambania, kuyaishi, kuyainua na kuyahuisha maisha yetu Watanzania kwenye eneo hili la ulinzi na usalama, hususan katika eneo la majeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe utakuwa shuhuda na Wabunge wenzangu watakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na kipaumbele kisichotia shaka juu ya usimamizi wa ulinzi katika maeneo ya mipaka na jamii zetu zinazozunguka. Amekuwa akitumia sera na maono yake katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na Jeshi imara lililojikita katika masuala yenye ubobezi kwenye eneo la ulinzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba uniruhusu pia nimpongeze sana kaka yangu na ndugu yangu Waziri wa Ulinzi, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na hapa ametoka kuzungumza Mheshimiwa Kingu kwamba sambamba na kubeba jukumu zito la kuihudumia Wizara hii, lakini bado amebeba sura na taswira inayoakisi namna ambavyo kiongozi anayesimamia vyombo vya ulinzi anavyopaswa kuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na amefika mbali akachukua maandiko yaliyobeba unyenyekevu ndani yake na kubeba nia ya mtu sahihi anayepaswa kuwapigania na kuwapambania wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Nyansaho si mgeni kwetu, kwa sisi vijana wa rika yetu tumemsoma sana alipokuwa PSSSF, tumemsoma alipokuwa Azania, tumemsoma alipokuwa TIC, lakini tumemsoma alipokuwa TANESCO alipofanya kazi kubwa ya kurudisha matumaini kwenye eneo la umeme, na leo hii sishangai, sipati bumbuwazi nikimwona akiwa anatekeleza wajibu wake vizuri kwenye eneo hili nyeti na uti wa mgongo wa Taifa letu katika nyanja zote za kiuchumi, jamii na suala zima la kiusalama lenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, toka Jeshi letu limeundwa tangu kuvunjwavunjwa kwa jeshi la wakoloni na nchi yetu kupata uhuru na kuamua kujisimamia wenyewe na kuunda Jeshi la Wananchi wa Tanzania, jeshi hili halijawahi kutuangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama yako mataifa duniani yanaweza kufikia mwisho wa dunia, yakawekwa mbele ya hukumu, yakaulizwa tuambieni katika nchi na ardhi niliyowapa, mbele za Mungu, nini mliwahi kujivunia? Ukiacha ardhi, ukiacha maji, ukiacha uoto wa asili na mimea tuliyopewa pamoja na wanyama, jambo pekee tunalojivunia Watanzania ni kuwa na Jeshi imara, lenye nguvu, uzalendo na uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika namna ya kibinadamu unaweza ukajiuliza, je, kama mimi nisingezaliwa Tanzania, neno amani na utulivu unaojengwa na jeshi imara ningeweza kuuona wapi?
Mheshimiwa Spika, ninataka nikiri mbele ya Bunge lako Tukufu kuwa, sisi Watanzania, sisi Wabunge, kama vile jeshi linavyotulinda kwa silaha, kwa akili na maarifa, ndivyo sisi wananchi na Wabunge tunavyowalinda wao kwa maombi, imani na maarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jeshi letu limefanya kazi kubwa sana, limepambana katika maeneo ya ndani na nje ya nchi. Limejenga hehsima katika diplomasia ya Ulinzi, limejenga heshima katika uzalishaji mali, limejenga heshima katika masuala ya usalama. Kwa unyenyekevu mkubwa sana na heshima, ninaomba niwapongeze sana wasimamizi wa vyombo hivi. Ninampongeza sana Afande CDF Jacob Mkunda kwa kazi kubwa ya usimamizi anayoifanya na utulivu alioutengeneza kwenye jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ninampongeza Jenerali wa JKT kwa kazi kubwa anayoifanya ya ku-recruit vijana wetu, kuwatengeneza, hatimaye leo tunapoliona Jeshi la Tanzania tunaiona JKT iliyoandaliwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, mimi nina maeneo machache sana ya kuweza kuchangia na kutengeneza ushauri wangu. Eneo la kwanza, ukiachana na shughuli za ulinzi wa mipaka, uzalishaji mali, lakini sisi sote tutakuwa mashahidi, tumeliona jeshi letu likishiriki katika masuala ya kijamii, masuala ya kuokoa, masuala ya kutengeneza comfort kwa watu na masuala yote yanayohusu majanga.
Mheshimiwa Spika, jeshi hili limefanya kazi kubwa pale Hanang, ndugu zangu wa Hanang watakuwa mashahidi namna jeshi lilivyofanya kazi yake vizuri. Jeshi hili limefanya kazi kubwa tulipopata majanga Kariakoo, watu wote wanajua na tunafahamu. Jeshi hili limesimamia ujenzi pale Msomera kwa nguvu kubwa, uwezo mkubwa na weledi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo kusema kwamba mashaka yetu juu ya matumizi ya maarifa ya kijeshi hayaishii kwenye medani ya vita. Bado tunayapeleka kwenye medani ya maisha ya kijamii. Sasa tuna maeneo mawili ambayo niliomba kuchangia.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni juu ya vijana wa Tanzania ambao wanamaliza kidato cha sita. Kwa sasa utaratibu tulionao ni wa kuwachukua vijana waliomaliza kidato cha sita kwenda kujitolea kwa mujibu wa sheria, lakini tunawaacha vijana wengi sana huko mtaani. Kwa kadri tunavyoona uwezo wa jeshi na namna wanajeshi wanavyokuwa, basi ni ombi langu na ninaamini Serikali yangu sikivu itaweka bajeti ya kutosha kupitia Wizara ya Fedha, ili vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wasiende kwa mafungu, waende wote wanapokuwa wamemaliza, ili tukajenge Taifa la wasomi wenye uzalendo, ili tukajenge wataalamu wenye kuijua nchi hii, ili tukajenge wataalamu wasomi watakaokuja kulipigania Taifa hili kwa jasho, damu na nyama yao yote. Hilo ni eneo langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, amezungumza vizuri Mheshimiwa Dkt. Jafo na nilimpenda aliposema jeshi letu limebeba heshima na matumaini. Kama kuna jambo la mwisho na ni tumaini kwa Watanzania, pale wanapomwona mwanajeshi kwenye jambo gumu, hapo wanakuwa wamemaliza matatizo yao yote.
Mheshimiwa Spika, wako wazee wetu wamepigana Vita vya Kagera, wako katika maeneo mbalimbali nchini. Wako kila wilaya na kila jimbo la Mbunge hapa. Ninaiomba sasa Wizara, ninashauri namna ya kufanyia kazi hili jambo.
Mheshimiwa Spika, kwenye kila wilaya kuna Kamati za Usalama, ninaomba tuwatumie Wakuu wa Wilaya waliopo na Wakuu wa Vikosi vya Mgambo walioko kule, kuwabaini wazee waliobakia ambao wamepigana kulipigania Taifa hili katika kuliokoa dhidi ya mashambulizi ya Idi Amin. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale Kagera walifanya kazi kubwa sana. Sasa hawa wazee wanadai madai yao, na mimi sina mashaka Mheshimiwa Waziri katika jambo hili, tukilichukua vizuri tukaliweka kwenye utaratibu, wazee wetu hawa tutapata manufaa, tutajua namba yao na tutasaidia kuwaokoa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie fursa hii adhimu sana kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na uzima iliyotuwezesha sote kuweza kukutana kwenye jengo hili Tukufu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uniruhusu kipekee kabisa na kwa shukrani za unyenyekevu kutoka ndani ya sakafu ya moyo wangu kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Nachingwea kwanza kwa kukubali, kuridhia na kunichagua mimi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nachingwea. Pili, kwa kumchagua kwa kura nyingi na za kishindo, na za heshima Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tatu, kwa kushiriki na kuendesha vizuri zoezi la Uchaguzi Mkuu toka katika kipindi cha kampeni mpaka siku ya kupiga kura wakiwa wamejijengea utulivu wa kuchagua viongozi waliowapenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu moja kwa kuchaguliwa kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimeisoma na nimeipitia hotuba aliyoitoa Bungeni tarehe 14. Katika hotuba ile Mheshimiwa Rais amejielekeza katika vipaumbele, ameonyesha umadhubuti, ameonyesha nia na amefungua mwanga wa Tanzania kubwa tunayoitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweka vipaumbele mahususi na amejipambanua kutokana na mwelekeo wa nchi ya dunia ya sasa inavyotakiwa kwenda kwa kuzingatia masuala mtambuka mbalimbali yanayoijenga dunia ya leo katika masuala ya kimaendeleo katika maeneo ya teknolojia, huduma za jamii, hali za vijana na mambo ya usalama wa nchi. Mheshimiwa Rais kila kitu amekiweka vizuri. Naomba kutumia fursa hii kumpongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba hotuba hii aliyoitoa hapa Bungeni ndiyo itakuwa dira, itakuwa mwelekeo na ndiyo itakuwa tochi itakayotuangazia Watanzania kuyaelekea maendeleo ya kweli katika siku zote za kuitumikia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba Mheshimiwa Rais amejipambanua wazi kabisa, lakini ninaomba uridhie niweke jambo moja kutoka katika kitabu kitakatifu. Kwa wale wasomaji wa Biblia watakubaliana na mimi kwamba baada ya Musa kuwachukua Wanaisraeli kutoka nchi ya utumwa alipowapeleka kwenye nchi yao ya utawala na kuishi, Musa ndiyo alikuwa kiongozi aliyetumainiwa, aliyetegemewa na ambaye alionekana ndiyo mustakabali wa Taifa la Wanaisraeli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Biblia inaeleza na hadithi iko wazi kabisa Musa naye alikufa sambamba na kuwa alipendwa na alihitajika. Wakati Musa anawaacha Wanaisraeli ni kama Taifa ambalo liliulizana nani anakuja kuwa Musa wa pili atakayetuvusha na kutupeleka kwenye nchi ya asali iliyoahidiwa. Mungu akamwinua mtu anaitwa Joshua akamwambia wewe ninakupa kazi ya kuwachunga kondoo wa Israeli na wafike kwenye nchi ya asali na maziwa wakiwa salama na wenye furaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimsoma vizuri Joshua katika maandiko matakatifu anasema wakati anapokea nafasi ya uongozi hata yeye mwenyewe alibaini kwamba wako watu wanaweza wasielewe na kuamini kuwa ni Joshua mwenye nguvu atakayevusha wana wa Israeli ndipo Mungu akamwambia Joshua uwe hodari na moyo wa ushujaa, usiogope wala usifadhaike kwa kuwa Bwana Mungu wako yuko pamoja nawe kila uendako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niyachukue maneno haya niyaweke katika fikra, mwelekeo, mtazamo na dhima ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba amepokea kijiti kutoka kwa Musa na wakati anapokea inawezekana yako mashaka lakini kwa kazi, huduma na mwelekeo aliouonesha katika kipindi cha miaka minne mpaka sasa inatosha kabisa kutupa matumaini ya kuvuka bila mashaka yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, basi na Watanzania wenzangu kama leo dunia itatuamsha na kuuliza Rais wa Tanzania anapenda nini? Jibu nitakalolitoa nikiwa nimeamka anaipenda nchi yake kuliko kitu chochote. Kama leo dunia itaniuliza unajivunia nini kwa Rais wako, nitawaambia nitajivunia kuwa na Rais aliyewatoa watoto wa kimaskini kutembea umbali mrefu kufuata elimu kwa kuwajengea mabweni na shule karibu na maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama dunia itaniuliza kwa nini unamsemea Rais wako nitawaambia ninamsemea Rais aliyeendeleza na kufufua miradi mipya ya kimkakati ambayo ingeweza kukatisha tamaa. Nitawapa ushuhuda wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo Busisi, Miradi mikubwa ya Hospitali za Kanda, Hospitali za Mikoa, Hospitali za Rufaa, Hospitali za Wilaya, Zahanati pamoja na Vituo vya Afya ambavyo Dkt. Samia Suluhu Hassan amevijenga kwa nguvu, uwezo na mapenzi makubwa kwa nchi yake ya Tanzania. (Makofi)
MHE. ZAINABU R. KAWAWA: Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.
TAARIFA
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza msemaji, mdogo wangu Fadhili Liwaka, lakini ninataka kumwongezea taarifa kwamba nami pia nitamsemea Mheshimiwa Rais kwa mradi mkubwa wa Bandari ya Uvuvi katika Wilaya ya Kilwa, hii ni bandari ya kimkakati ambayo iko katika 90% na zaidi, hivi karibuni inakaribia kumalizika, lakini ni Bandari kubwa katika ukanda huu wa Nchi za Afrika Mashariki ambayo haijawahi kujengwa popote pale. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, Mheshimiwa Fadhili unaipokea taarifa hiyo?
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti kwa dada yangu ninayemheshimu sana na bado ninamwongezea kwamba dunia ikiniamsha juu ya Uchumi wa Bluu nitawaambia ninamsemea Rais aliyethubutu kujenga Bandari za Uvuvi, kujenga meli za usafirishaji za watu na mizigo na aliye tayari kuhakikisha kwamba wavuvi kwenye Ukanda wa Maziwa na Bahari Kuu wanapata mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo na kuweka mwelekeo wangu na mtazamo ambao ninatamani kila Mbunge na Mtanzania auone kwa Rais wetu, ninaomba nijielekeze kwenye mambo matatu ambayo kwenye hotuba Mheshimiwa Rais ameyaweka vizuri na sisi tunahitaji msisitizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nitumie fursa hii sasa kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia niwapongeze Mawaziri waliotoa huduma kwenye Wizara ya Madini. Moja kati ya jambo kubwa ambalo nchi yetu inaweza kujivunia ni uwepo wa rasilimali ya madini, tena madini yenye thamani kubwa sana hata pale nchi yetu inapotoa sauti duniani juu ya kwamba tunayo thamani ya madini ambayo inamezewa mate hatutoi kwa bahati mbaya au kujifurahisha, tunatoa kwa sababu mlio wa mgonjwa, anayeujua ni muuguzi na sisi ndio wauguzi wa nchi yetu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika eneo hili Serikali imeweka mikakati madhubuti; moja, kuhakikisha tunavutia uwekezaji katika eneo hili la madini na tumeona pato la Taifa limeongezeka kutoka kwenye Sekta ya Madini kutoka asilimia 6.8 mpaka 10.1%. Hii ni kazi kubwa sana na imefanywa na sekta pamoja na Wizara ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Mavunde na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ya usimamizi na sisi sote tutakuwa mashahidi tumeona Wizara ikihangaika. Jambo la kwanza ni kuweka utaratibu mzuri wa uwekezaji kwenye eneo la madini, lakini eneo la pili, kuhakikisha Watanzania wanakuwa matajiri kwa kuwa wachimbaji wazuri kupitia maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niungane nao na kuwatia shime kwamba moja ya jambo litakalolitoa Taifa na kusogea mbele zaidi kwenye eneo la Sekta ya Madini pamoja na mikakati iliyoelezwa katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha tunaongeza thamani ya madini, tunafungua kituo cha uzalishaji wa madini East Africa. Hata hivyo, ni sharti letu la msingi na ni muhimu kuwatambua, kuwaelekeza na kuwajenga wachimbaji wadogo nchini ili waweze kupata ngazi ya utajiri na kuwa wachimbaji wakubwa ili tuwe na Taifa lenye thamani ya mali zilizopo hapa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwelekeo wa uchimbaji wa madini nchini unakwenda vizuri kwa sababu tumeona leo tukihesabu idadi ya Watanzania waliopata uwezo wa kujisimamia na kuweza kufanya shughuli za uchimbaji haiwezi kulinganishwa na miaka 15 iliyopita, kwa sasa tumepiga hatua kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninaomba niweke maneno yangu kwenye jambo moja. Nimesoma vizuri hotuba Mheshimiwa Rais na nimeona mwelekeo katika suala la kupambana na kusaidia kuwaondoa wanyama waharibifu ambao ni ndovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka jimbo ambalo 75%, wakati ninaomba kura ya wananchi kila nilipokwenda moja ya hoja niliyokutana nayo ni wanyama waharibifu aina ya Ndovu. Ninafahamu ndovu hawa wanalindwa na sheria maalum ya kimataifa. Ziko nchi ambazo ziliwahi kupitia changamoto kubwa ya wanyama wengi wa aina hii kama vile Sri-Lanka, India, Sierra Leone na nchi zingine nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mahususi ambayo kama nchi tukiamua kuyaweka tunaweza kusaidia kuwaondoa wananchi wetu kwenye adha ya hawa wanyama ambao sio tu wanamaliza mazao ya watu bali wanahatarisha usalama na maisha ya Watanzania kwa sababu wanaua. La kwanza ziko njia ikiwemo zile ambazo zimeainishwa na Wizara. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kuwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)