MHE. AISHA M. MDUYAH aliuliza:-
Je, lini Serikali itaridhia na kuanza utekelezaji wa Itifaki ya Afrika kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (African Disability Protocol)?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kukamilisha taratibu muhimu kabla ya kuridhia na kuanza kutekeleza Itifaki ya Afrika kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu Barani Afrika (African Disability Protocol). Hadi sasa Serikali imeshafanya mapitio ya kisera na kisheria na tayari imeshakusanya maoni ya wadau kutoka kwenye vyama na mashirikisho ya watu wenye ulemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, likiwemo Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA). Vilevile, maoni ya Serikali zote mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yamekusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua hizo muhimu kukamilika, tayari rasimu ya itifaki imeshaandaliwa na wakati wowote kuanzia sasa itawasilishwa kwenye vikao vya maamuzi, kabla ya kuwasilishwa Bungeni kwa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambayo inalipa Bunge mamlaka ya kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. AISHA M. MDUYAH aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawekea Miundombinu wezeshi Wanafunzi wenye mahitaji maalum ili wasome fani wanazozipenda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisha Msantu Mduyah, Mbunge wa Viti Malaam, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mkakati wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022 - 2026 na Waraka Namba Tatu wa mwaka 2025 kuhusu mfumo wa Kitaifa wa kuzifanya shule kuwa Jumuishi mwelekeo wa Serikali ni kuzifanya shule zote za msingi na sekondari zilizopo kuwa jumuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali kuzifanya shule za msingi na sekondari kuwa jumuishi, ni pamoja na kuhakikisha kuwa miundombinu inayojengwa inakuwa rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuhakikisha kuwa bajeti ya Serikali inajumuisha fedha ya ununuzi wa vifaa wezeshi na vifaa visaidizi kwa watoto wenye mahitaji maalum, kutoa ajira kwa walimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kutoa mafunzo kwa walimu wa elimu maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa kuna shule maalum 44 za msingi na moja ya sekondari, vitengo maalumu 815 kwa shule za msingi na shule za awali na msingi jumuishi 20,889 na sekondari ni 6488. Vilevile, shule jumuishi 53 za sekondari za bweni Kitaifa na tatu za kutwa zinapokea wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao wana changamoto kubwa zaidi nchi nzima. Serikali itaendelea kuboresha shule za msingi na sekondari ili ziwe jumuishi zaidi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, ahsante. (Makofi)