Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aisha Msantu Mduyah (2 total)

MHE. AISHA M. MDUYAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na sina swali la nyongeza, lakini naiomba tu Serikali iharakishe mchakato huu kwa maslahi mapana ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Aisha kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Namhakikishia tumepokea ushauri na tutaendelea kuufanyia kazi kwa haraka, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AISHA M. MDUYAH: Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze na kuishukuru Wizara ya TAMISEMI, kwa majibu yao mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na aina nyingi za ulemavu, kuna baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wanashindwa kufikia masomo yao ya elimu ya juu kutokana na hali zao. Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuhakikisha kwamba wanafunzi hawa wanapatiwa vitendea kazi pamoja na walimu bobezi kwa masomo ya amali ambayo yataweza kuwafanya wenyewe waweze kujitegemea hapo baadaye? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Aisha Msantu Mduyah, amekuwa msemaji imara sana wa watu wenye ulemavu, lakini na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa vitendo na inatekeleza taratibu, lakini pia miundombinu ya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata fursa nzuri zaidi ya kusoma na kujifunza ili waweze kufikia malengo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie kwamba suala la watu wenye ulemavu ambao wanahitaji viwezeshi wanahitaji miundombinu yote imewekwa kwenye utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba wanafikia kwenye ngazi wanazopenda na kusoma taaluma ambazo wanaweza kuzifikia kwa mujibu wa matakwa yao, na Serikali ikaendelea kuhakikisha pia tunapata walimu na vitendea kazi kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kusoma kwa ufanisi zaidi. (Makofi)