Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SAMIRA K. AMOUR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kipekee kabisa ninapenda kukupongeza kwa kunipatia nafasi na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia jioni ya leo kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza Waziri wetu wa Nishati na dada yangu Naibu Waziri kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini na maendeleo kwa Watanzania kwa ujumla. Kipekee kabisa ninapenda kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi, mwaka 2024 alizindua mkakati wa nishati safi ya kupikia. Jambo hili liliinua matumaini mapya na mazuri yanayoonyesha namna wananchi wa kawaida, hasa vijijini, watakavyokwenda kunufaika na mkakati huu ifikapo 2034. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijikite kuchangia nishati safi ya kupikia. Sote ni mashahidi, tumeona Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ni kinara wa kuhamasisha matumizi safi ya nishati ya kupikia. Hii ni ishara tosha kwamba anatujali wanawake wa Tanzania. Kwa hakika tunapika kwa haraka, familia zetu zimeweza kula kwa wakati na tunaendelea na majukumu mengine ya kukuza uchumi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuishauri Serikali yangu, tumesikiliza vizuri hotuba na Bajeti ya Nishati kwa mpango mkakati mzuri waliouweka ili kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia. Ninaomba nishauri; tuweke mikakati bora, tujikite zaidi kushughulikia, kama jinsi tunavyoweza kupata mafuta katika vijiji, kwenye wilaya, ukiwa na shilingi 2,000 unapata mafuta ya taa, basi vivyo hivyo tuboreshe tuweze kupata gesi. Tuingie makubaliano na sekta binafsi, wale ambao wana filling stations waweze kuuza na gesi, pale mwananchi wa kijijini atakapokuwa na shilingi 2,000 au 3,000 aweze kupata kilo moja ya gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kagera ninapotoka, kwa wanawake wa kijijini kabisa, mwanamke wa Nkwenda huko, mwanamke wa Kituntu, kumwambia kwamba kanunue gesi ya shilingi 25,000 inakuwa ni mtihani sana. Akipata unafuu wa kuweza kununua gesi kwa bei ndogo kutokana na fedha yake aliyonayo tutafikia malengo yale Dkt. Samia Suluhu Hassan anayotamani kuyaona kwa kila mwananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kusema; Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara. Kama tunavyosikia sasa hivi kuna ruzuku ya mitungi ya gesi. Ninaomba nishauri Serikali yangu, pindi wanapohitaji kugawa hiyo mitungi ya gesi basi vyema tukashirikishwa sisi Wabunge wa Viti Maalum, kwa sababu ndiyo tunaojua wanawake wanaohitaji hiyo mitungi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Dkt. Samia Suluhu Hassan akiendelea kuhamasisha. Hata jana amekutana na makundi ya mamalishe na babalishe. Hiyo yote ni ishara kwamba amedhamiria na anatamani kuona kila Mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kusema; Wizara ya Nishati imejipanga vizuri, ninawapongeza sana. Tunaona sasa hivi kama ni umeme tunaenda kupata umeme kwa kila kitongoji. Ninapenda kuwashukuru sana; lakini niwaombe Wabunge wenzangu tushirikiane na Mheshimiwa Waziri wetu. Anajituma sana na maendeleo tunayaona. Bajeti ina matumaini kwa kila Mtanzania. Ninaomba tumpitishie bajeti yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa nafasi ya kutoa mchango wangu. (Makofi)